Tuesday 27 August 2013

Shaaban Robert : Hazina ya lugha ya Kiswahili iliyosahaulika

Aisha Jafary, mtoto wa kaka yake Shaaban Robert akiwa na mwanaye, MwanaAkida Jafary (kushoto). Picha na Burhani Yakub 
Na Burhani Yakub, Mwananchi  (email the author)

Posted  Jumatatu,Agosti26  2013  saa 13:42 PM
Kwa ufupi
  • Nchini India kuna jengo maarufu la Taj Mahal, ni kaburi lenye umbo la msikiti, lililoko mjini Agra. Jengo hilo lilijengwa kwa amri ya Shah Jahan aliyekuwa mtawala wa eneo hilo kwa ajili ya kumkumbuka ya mke wake mpendwa Mumtaz Mahal.  Inakuwaje Tanzania inashindwa kuona umuhimu wa kujenga jengo zuri na la maana kwa kumbukumbu ya Shaaban Robert ambaye ameutumia muda wake mwingi kukiimarisha Kiswahili, lugha kuu inayozungumzwa nchini?


Ni vigumu kuzungumzia historia ya Lugha ya Kiswahili nchini ukaeleweka na wapenda lugha hiyo duniani bila kumtaja marehemu Shaaban Robert, kutokana na ukweli kuwa amekuwa mshairi na nguli katika lugha hiyo.
Mchango wa Shaaban Robert katika lugha ya Kiswahili una thamani kubwa kutokana na riwaya na mashairi yaliyojaa mafunzo na hekima kubwa jambo ambalo limempa heshima na kusababisha azidi kukumbukwa kila muda unavyozidi kusonga mbele.
Jina la Shaaban Robert linafahamika vyema ndani na nje ya mipaka ya Tanzania na kusababisha kazi za vitabu vyake kutumika shuleni pamoja na vyuo vya kati na vya juu nchini na kwingineko Duniani.
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika uhai wake akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizithamini na baadaye kuzitangaza kazi za marehemu Shaaban Robert hadi kufikia kuziingiza katika kumbukumbu ya historia ya Taifa la Tanzania.
Hata barabara ya kwenda Ikulu inaitwa jina lake ‘Barabara ya Shaaban Robert’
Barabara kuu ya kuingia  Ikulu ya Dar es Salaam kupitia Jumba la Makumbusho imepewa jina la Shaaban Robert. Barabara hii ni sehemu tu ya maeneo ikiwamo mitaa ya Jiji la Dar es Salaam na mikoa mingine iliyopewa jina la kumuenzi gwiji huyu.
Shaaban Robert alizaliwa siku ya mkesha wa mwaka mpya mwaka 1909 katika Kitongoji cha Vibambani, Kijiji cha Machui ambacho kipo umbali wa kilomita 10 Kusini kutoka Tanga mjini.
Wazazi wake Shaaban Robert asili yao ni Kabila la Wahiyao, waliotokea  mikoa ya Kusini mwa Tanzania sehemu za katikati ya Lindi na Mtwara iliyokuwa imebobea katika desturi na mila za Uswahili.
Simulizi zinaonyesha upo mkanganyiko kuhusiana na ni namna gani baba yake aliitwa jina la Robert wakati historia inaonyesha Shaaban Robert alizaliwa katika kile kinachoelezwa kuwa ni ukoo wa Waswahili na Waislamu halisi. Shaaban ni jina la Kiislamu, Robert ni la Kikristo.
Mwandishi wa makala haya anasema wakati anafuatilia juu ya mtu huyu, alizungumza na baadhi ya ndugu zake Shaaban Robert, hakuna aliyekuwa tayari kuweka wazi juu ya jina hili na baba yake yaani Robert.
Mmoja wa watoto wake ambaye pia amefuata nyayo za baba yake za umahiri wa utunzi wa mashairi na uandishi wa riwaya, Ikbar Shaaban Robert anasema pamoja na kufuatilia sana hajapata siri hasa ya jina hilo la Robert kupewa babu yake.
Simulizi nyingine zinaeleza kuwa Robert lilikuwa ni jina halisi la baba yake Shaaban Robert lakini simulizi nyingine zinakataa na kueleza halikuwa jina la baba yake mzazi, bali alipewa tu kutokana na yeye mwenyewe kulipenda.

Elimu yake aliipata katika Shule ya Msimbazi jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 1922 na 1926, alifanya vizuri shuleni katika masomo yake na kupata cheti za kuhitimu masomo.
Alianza kazi mwaka 1926  akiwa Karani katika Idara ya Forodha ya Serikali ya Waingereza na alipangiwa kazi ya kusimamia shughuli mbalimbali katika Bandari ya Pangani mjini, Pangani Mkoa wa Tanga.
Kwa miaka miwili kati ya mwaka 1944 na 1946, alifanya kazi katika Idara ya wanyamapori na mwaka 1946 hadi 1952 akahamishiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga na baadaye akahamishiwa  idara ya Mipango hapohapo mkoani.
Shaaban Robert alijiunga uanachama wa Kamati ya Kiswahili Afrika Mashariki (East Africa Swahili Committee), Taasisi ya Fasihi ya Afrika Mashariki (East Africa Literature Bureau) na Bodi ya Lugha Tanzania.

Tuzo kutoka kwa Malkia
Katika kuenzi kazi zake za kukiendeleza na kukikuza Kiswahili, Shaaban Robert amewahi kupata tuzo mbalimbali ikiwamo ile ijulikanayo kama ‘The Margaret Wrong Memorial Prize’.
Tuzo nyingine ni ile ya Member of British Empire MBE  na ile ya Malkia wa Uingereza (By Her Highness The Queen of England)
Kwa idadi, Marehemu Shaaban Robert katika uhai wake aliwahi kutunga hadithi nyingi lakini alizoandika jumla yake ni  vitabu 22 vya hadithi fupi, mashairi na insha. Baadhi ya kazi hizi zinatumika kufundishia katika madarasa ya shule mbalimbali ndani na nje ya nchi, vingine vimetafsiriwa katika lugha za Kiingereza, Kirusi, Kichina na Kijerumani.
Shaaban Robert alifariki Juni 22, 1962 akiwa na umri wa miaka 53 na kuzikwa katika Kijiji  cha Machui, Kitongoji cha Vibambani.
Mtu huyu bado anakumbukwa kama ni hazina kwa Taifa la Tanzania na ni tunu ya Mkoa wa Tanga kwani mbali ya kuzaliwa Tanga, karibu maisha yake yote ya kitumishi serikalini aliyatumia akiwa katika ardhi ya Tanga akiwa wilayani Pangani na Tanga Mjini.
Mchango wa Shaaban Robert katika lugha ya kiswahili ni mkubwa hasa katika uhamasishaji jamii ya ndani na nje ya Tanzania kupenda kuizungumza na kuiandika kwa njia ya mashairi, tenzi na riwaya kwani kazi zake zimefika mbali.
Huwezi kuhitimu Kiswahili bila kusoma kazi za Shaaban Robert.

Miongoni mwa kazi ambazo mwanafunzi wa Kiswahili hawezi kuhitimu au kufanyia kazi ni pamoja na kitabu cha Kusadikika, Wasifu wa Siti binti Saad na Maisha yangu.

Kaburi halina hadhi ya jina lake
Licha ya kuwa na umaarufu, ni jambo la kushangaza kwamba ukifika katika kaburi lake huwezi kuamini kwamba aliyezikwa humo ni mtu aliyezoa umashuhuri duniani kote.
Hadi unafika kwenye kaburi lake hakuna ishara yoyote yenye kuonyesha kuwa unaelekea eneo la kaburi la Shaaban Robert. Ilivyo ni kwamba kwanza unaingia porini na kutokeza mahala palipo na makaburi matatu likiwamo la mshairi huyu maarufu.
Kilichofanyika kwenye kaburi lake ni kujengea marumaru na lina maandishi ya kiarabu, lakini hakuna zaidi ya hilo.
Hali ya familia
Mtoto wa kaka yake Shaaban Robert aitwaye Aisha Jaffary (68) anasema hakuna manufaa yanayopatikana kwa familia ya Shaaban Robert kwa watu kutoka nchi mbalimbali duniani wanaokwenda kuzuru kaburi lake.
“Hakuna ulinzi wala usimamizi wowote katika kaburi lake, watu wanakwenda tu kienyeji kutazama kaburi la Shaaban Robert na kwa kuwa limeachiwa tu waangaliaji hawalipi chochote kama ada kama inavyofanyika kwenye maeneo mengine ya kihistoria,” analalamika MwanaAkida Mwanjovu ambaye ni mtoto wa Aisha.
MwanaAkida anasema wengi wa wasomi wamepanda ngazi za kuwa madokta au maprofesa kupitia kazi za babu yake huyo, lakini wanazuru kaburi lake bila kujali kuwa mazingira yanahitaji kuboreshwa.
Mwandishi wa makala hii wakati akielekea kwenye kaburi la marehemu Shaaban Robert alilazimika kutembea mwendo wa nusu kilomita vichakani kufuata kaburi hilo.
Katika nchi kama India na nyinginezo Duniani, watu maarufu kama hawa hujengewa vizuri ukuta na watu kuingia kwa kulipia kama njia ya kuharakisha maendeleo. Ndani ya jengo la mtu kama huyo huwekwa vitabu au kazi zake nyingine, kwamba wale wanaotembelea wanaweza kununua.

Mfano wa Taj Mahal India


Taj Mahal, ni jengo zuri la kaburi lenye umbo la msikiti, lililoko mjini Agra (India). Mara nyingi huhesabiwa kati ya majengo mazuri duniani.
Taj Mahal ilijengwa kati ya mwaka 1631 - 1648 kwa amri ya Shah Jahan aliyekuwa mtawala wa eneo hilo.
Lilijengwa maalumu kwa ajili ya kumkumbuka mke wake mpendwa Mumtaz Mahal.  Shah Jahan aliwaajiri mafundi 20,000 kutoka Asia ya Kusini na Asia ya Kati walioongozwa na Ali Fazal kutoka Afghanistan.
Taj Mahal imekuwa shabaha ya watalii wengi na tangu 1983 imeandikishwa katika orodha ya urithi wa dunia na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco).
Kama jengo lilijengwa kwa ajili ya kumkumbuka mke tu huko India linaheshimiwa, vipi kaburi la mtu kama Shaaban Robert aliyefanya jitihada kubwa kukikuza Kiswahili linaachwa linajaa nyasi? Ni watawala pekee wenye jibu sahihi.

Serikali na Shaaban Robert
Licha ya ukweli kwamba mtu huyu alikuwa muhimu kwa taifa, hakuna jitihada zinazofanyika ili kuendelea kumuenzi.
Kilichowahi kufanyika ni kwa Ofisa wa Utamaduni Halmashauri ya Jiji la Tanga, Peter Semfuko kuanza ujenzi wa jengo la maktaba ya kuonyeshea kumbukumbu ya kazi za mshairi huyo.
Fedha za ujenzi wa jengo hilo zilitolewa na mfuko wa utamaduni ambao baadaye ulisitishwa hivyo jengo hilo limebaki kuwa gofu kwani halitumiki kwa sababu halikuwekwa samani yakiwamo mashelfu ya kuwekea vitabu.

Wananchi hawana raha
Baadhi ya wananchi walioongea na mwandishi wa makala hii wameonyesha kutokufurahishwa kwao na namna ambavyo Serikali haioni umuhimu wa kujali watu muhimu katika taifa kama Shaaban Robert.
“Kuna barabara, shule na maeneo mengi yanatumia jina la Shaaban Robert, lakini mazingira ya kaburi na hali nzima ya Shaaban Robert mwenyewe kwa maana ya urithi wake ni kama hautiliwi maanani,” anasema Jonathan Moyo, mkazi wa Ubungo.