Posted Jumanne,Agosti27 2013 saa 22:39 PM
Kwa ufupi
- Pamoja na juhudi za Dk Ndalichako za kutoa ufafanuzi kuhusu ukweli wa suala hilo, hakuna aliyekuwa tayari kumpa sikio kutokana na suala hilo kupewa mtazamo wa kisiasa. Wananchi wengi, wakihamasishwa na wanasiasa waliishinikiza Serikali kutafuta chanzo cha hali hiyo.
Leo tumechapisha mahojiano maalumu kati ya
gazeti hili na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta),
Dk Joyce Ndalichako kuhusu suala zima la usimamizi wa mitihani katika
nchi yetu. Sote tutakubaliana kwamba suala la usimamizi wa mitihani
limekuwa katika ndimi za wananchi wengi katika miezi ya hivi karibuni
kutokana na matokeo mabaya ya mitihani ya kidato cha nne ya mwaka 2012
ambapo karibu nusu ya wanafunzi walifeli.
Kilichofuata baada ya kutokea kwa hali hiyo sasa
ni sehemu ya historia, ingawa ni muhimu tukakumbushana tena kwamba hali
hiyo iliibua sintofahamu katika Serikali na sekta nzima ya elimu. Bila
kufanya tafakuri jadidi kuhusu sababu za wanafunzi hao kufeli mtihani
huo, kila upande ulizungumza kivyake, huku Necta ikibebeshwa mzigo
mkubwa wa lawama ambazo kusema kweli haikuzistahili. Moja ya lawama
nzito ni kwamba kufeli huko kulitokana na Necta kubadili ghafla mfumo wa
usahihishaji.
Pamoja na juhudi za Dk Ndalichako za kutoa
ufafanuzi kuhusu ukweli wa suala hilo, hakuna aliyekuwa tayari kumpa
sikio kutokana na suala hilo kupewa mtazamo wa kisiasa. Wananchi wengi,
wakihamasishwa na wanasiasa waliishinikiza Serikali kutafuta chanzo cha
hali hiyo. Hivyo, Serikali iliunda Tume ambayo ilipendekeza kufutwa kwa
matokeo hayo na kuyasanifisha upya, uamuzi ambao ulionekana kwa wengi
kuwa wa kisiasa. Hata hivyo, kiwango cha ufaulu baada ya kupitia upya
matokeo hayo kilipanda kidogo, lakini hakikubadili picha halisi ya
kwamba wanafunzi walioshindwa hawakuonewa na walistahili alama
walizokuwa wamepewa awali na Necta.
Katika kupitia mahojiano yetu na Dk Ndalichako,
wasomaji wetu watagundua kwamba kiongozi huyo bado anaona fahari kwa
kazi iliyofanywa na inayoendelea kufanywa na Necta. Msimamo wake ambao
nasi tunauunga mkono ni kwamba siYo tu siasa hazipaswi kupewa nafasi
katika mchakato wa usimamizi wa mitihani, bali pia tusikubali kufikishwa
mahali ambapo kila mwanafunzi atatakiwa afaulu mtihani hata kama hana
sifa wala uwezo.
Tunakubaliana naye pia pale anapopinga dhana
kwamba Necta inapaswa kushirikiana na wadau wote katika kazi zake. Jambo
hilo haliingii akilini kwani kama alivyosema mwenyewe, taasisi yake
ikifanya hivyo itafika wakati ambao wadau hao watataka washirikishwe
katika kutunga mitihani inayotolewa na Necta. Lazima tukubali kwamba
madhara ya kuingilia masuala ya mitihani ni makubwa mno na tukikubali
wanasiasa waingilie mchakato wa mitihani tutakuwa tunaliangamiza taifa
na kulipeleka kusiko.
Kwa kipimo chochote kile Necta imetoka mbali.
Tukumbuke angalao kidogo Necta ilivyokuwa kabla ya kuteuliwa kwa Dk
Ndalichako kuliongoza Baraza hilo mwaka 2005. Inaonekana wengi tumesahau
kwamba kabla ya kuteuliwa kwake Necta ilikuwa ikisutwa na wananchi kwa
kuendekeza vitendo vya kifisadi na rushwa.
Mitihani ilikuwa ikivuja kwa kiwango kikubwa na
ilikuwa ikiuzwa kama njugu barabarani na kwenye taasisi mbalimbali.
Baraza hilo halikuwa na uongozi wenye sifa za uadilifu na uchapakazi
kama tunavyoshuhudia hivi sasa.
Sisi tuna matumaini makubwa katika uongozi wa
Necta uliopo sasa. Chini ya uongozi huo, Necta sasa inaonekana kama
mfano wa kuigwa na ‘Necta’ nyingine barani Afrika. Kama wasomaji wetu
watakavyong’amua baada ya kusoma mahojiano yetu na DK Ndalichako,
kiongozi huyo ana upeo, ubunifu na mwelekeo wa kuipeleka Necta kule
inapopaswa kwenda iwapo ataungwa mkono.
source :Mwananchi
source :Mwananchi