Na Tusipokuwa makini tofauti hizi zitaiua EAC
(email the author)
Posted Alhamisi,Agosti29 2013 saa 22:4 PM
Posted Alhamisi,Agosti29 2013 saa 22:4 PM
Kwa ufupi
- Kiongozi huyo alitoa kauli zisizokubalika kidiplomasia dhidi ya Rais Kikwete ambaye aliamua kuzipuuza, ingawa baadhi ya vyombo vya habari nchini Rwanda vimeendeleza vita ya maneno.
Sasa ni bayana kwamba tofauti zilizopo miongoni
mwa baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),
zimeanza kukuzwa, huku wachambuzi wa masuala ya kidiplomasia wakionya
kwamba tofauti hizo zisipotatuliwa haraka jumuiya hiyo itasambaratika na
kubaki historia.
Sote tunatambua kwamba tofauti hizo zilianza baada
ya Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania kumshauri Rais Paul Kagame
kuzungumza na FDLR ambao ni waasi wa nchi hiyo wanaohusishwa na mauaji
ya kimbari ya mwaka 1994.
Rais Kikwete pia alimshauri Rais wa Uganda, Yoweri
Museveni kuzungumza na waasi wa nchi hiyo ADF, akisema hatua hiyo
italeta amani ya kudumu katika ukanda mzima wa Maziwa Makuu.
Kwa bahati mbaya Rais Kagame alikasirishwa na
ushauri huo. Alisema ushauri wa Rais Kikwete yalikuwa matusi kwa Rwanda
na kusema nchi hiyo haiwezi kamwe kuzungumza na watu waliofanya mauaji
ya kimbari.
Kiongozi huyo alitoa kauli zisizokubalika
kidiplomasia dhidi ya Rais Kikwete ambaye aliamua kuzipuuza, ingawa
baadhi ya vyombo vya habari nchini Rwanda vimeendeleza vita ya maneno.
Tunashawishika kusema kwamba Rais Museveni kwa
kukaa kimya aliukubali ushauri wa Rais Kikwete au alifanya hivyo tu ili
kuepusha kukua kwa mgogoro huo. Wapo wanaosema Rais Kikwete alitoa
ushauri huo kwa nia njema, lakini wakosoaji wake wanasema pamoja na nia
yake hiyo kuwa ya dhati kabisa, angeutoa faragha kwa Rais Kagame au
katika vikao mwafaka vya EAC badala ya kufanya hivyo katika kikao cha
Umoja wa Afrika (AU), kilichofanyika Addis Ababa, wakisema huko hapakuwa
pahala pake.
Hilo hakika ndilo chimbuko la mgogoro
tunaoushuhudia hivi sasa ambao tunadhani umekuzwa kupita kiasi tukitilia
maanani matukio ambayo yamekuwa yakitokea katika siku za hivi karibuni.
Hata hivyo, zipo tetesi pia kwamba Rwanda haikufurahishwa na kitendo
cha Tanzania kukubali kupeleka wanajeshi wake nchini DRC kuungana na
kikosi cha Umoja wa Mataifa (UN), kulinda amani nchini humo kwa lengo la
kuwanyang’anya silaha waasi wa M23 wenye asili ya Rwanda.
Tumelazimika kuandika hayo yote ili kuweka
kumbukumbu sahihi za mtiririko wa mgogoro huo ambao baadhi ya watu
walidhani ungeziingiza nchi hizo mbili jirani katika vita.
Hivi sasa umefanyika mkakati wa kuitenga Tanzania
kiuchumi ambapo juzi marais wa Kenya, Uganda na Rwanda waliungana
kuzindua upanuzi wa Bandari ya Mombasa inayokusudiwa kutumiwa na nchi
hizo kupakua na kusafirisha mizigo. Mkakati huo ulizinduliwa na marais
wa nchi hizo mjini Entebbe hivi karibuni ambapo Tanzania haikualikwa
kama ambavyo haikualikwa juzi wakati wa uzinduzi huo.
Tofauti zinazoendelea kujitokeza hakika sio ishara
njema kwa mustakabali wa EAC. Siku chache zilizopita uliibuka mzozo
miongoni mwa wabunge wa EAC jijini Arusha ambapo wabunge wa Uganda,
Kenya na Rwanda walisababisha kikao cha Bunge kuvunjika ili kumshinikiza
Spika aruhusu kujadiliwa kwa hoja ya vikao vya Bunge kufanyika kwa
mzunguko katika nchi wanachama badala ya Tanzania pekee.
Wabunge wa Tanzania nao walifanya hivyo siku
iliyofuata wakipinga hatua ya wabunge hao kutaka kumshinikiza Spika
kukubali hoja hiyo kinyume na Kanuni za Bunge.
Kwa mwenendo huo sisi tunadhani kuna ajenda ya
siri iliyofichwa chini ya zulia. EAC inachungulia kifo. Zinahitajika
busara kuinusuru. Vinginevyo, historia ya EAC ya mwaka 1977 itajirudia.