Kwa ufupi
Awali Bunge hilo, katika vikao vyake vya
Arusha, vilikuwa vikifanyika katika Jengo la Kituo cha Mikutano cha
Arusha (AICC) kwa kukodi.
Arusha. Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki,
(EALA), wameingia katika mpasuko, kutokana na baadhi ya wabunge hao
kupinga kutumia ukumbi wa kisasa wa Bunge hilo uliopo Arusha kwa vikao
vyote, na badala yake baadhi wanataka kuendelea na utaratibu wa kufanya
vikao vya Bunge katika kila nchi wanachama.
Habari za uhakika toka ndani ya Wabunge wa Afrika
ya Mashariki, walioanza kikao cha Bunge la jumuiya hiyo juzi jijini
hapa, zimebainisha kuwa, licha ya Kamati ya Uongozi wa Bunge hilo,
kufikia uamuzi ya vikao vyote sasa kufanyika Arusha, lakini bado kuna
wabunge wanapinga.
Kikao cha kamati ya uongozi kilichoongozwa na
mwenyekiti wake ni Spika wa Bunge hilo, Dk Magreth Zziwa, kiliamua baada
ya kukamilika jengo la Bunge, likiwa na ofisi kwa kila mbunge sasa
vikao vyote vifanyike Arusha ili pia kupunguza gharama.
Awali Bunge hilo, katika vikao vyake vya Arusha,
vilikuwa vikifanyika katika Jengo la Kituo cha Mikutano cha Arusha
(AICC) kwa kukodi.
Katika hatua ya kuonyesha kushawishi wabunge
kuanza kutumia jengo lao jipya kwa mikutano yote, Mbunge wa Bunge hilo
wa Tanzania, ShyRose Bhanji aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutoa
ardhi bure kwa ujenzi wa jengo la EAC lenye ukumbi wa kisasa wa Bunge.
Ofisa Habari za Bunge la Afrika ya Mashariki, Bobi
Odiko, jana alikiri kuwapo mjadala wa kutaka kuendelea kuhamisha vikao
vya Bunge au sasa kufanyika Arusha huku akisema anaamini wataafikiana.
“Ni kweli mijadala inaendelea na leo (jana) kulikuwa na kikao juu ya suala hili lakini naamani mwafaka utafikiwa”alisema Odiko
Source: Mwananchi
Source: Mwananchi