Kwa ufupi
- Baraza hilo tayari linatambuliwa ndani ya Katiba ya CCM, lilitokana na mapendekeo ya Kamati ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama iliyoundwa mwaka 2011.
Dodoma. Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete
jana alizindua Baraza la Ushauri linalounda na wenyeviti na makamu
wenyeviti wastaafu na baadaye baraza hilo likamchagua Rais Mstaafu, Ali
Hassan Mwinyi kuwa mwenyekiti wake wa kwanza huku katibu wake akiwa Pius
Msekwa.
Katika hafla ya uzinduzi wa baraza hilo,
iliyohudhuriwa na wazee hao isipokuwa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk
Salmin Amour kwa sababu za kiafya, Rais Kikwete aliwamwagia sifa marais
wastaafu, Mwinyi na Benjamin Mkapa kuwa ni sawa na kamusi ya mageuzi
makubwa yaliyotokea nchini nyakati uongozi wao.
Kuhusu Mwinyi, Kikwete alisema ni mwasisi wa
mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi kwa kuwa aliwezesha taifa kuondoka
katika uchumi wa dola kuingia uchumi soko, huku Mkapa akipokea
mabadiliko hayo na kuyaendeleza katika mfumo wa vyama vingi.
Baada ya uzinduzi huo, wazee hao walikaa kwenye
kikao chao cha kwanza kujadili “mambo ambayo wangeona yanafaa”, ambako
waliwachagua Mwinyi na Msekwa kuwaongoza.
Waliohudhuria uzinduzi huo ni Mkapa, Mwinyi, Msekwa, John Malecela na Amani Abeid Karume.
Baraza hilo tayari linatambuliwa ndani ya Katiba
ya CCM, lilitokana na mapendekeo ya Kamati ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa
CCM, Wilson Mukama iliyoundwa mwaka 2011.
kwa lengo la kushauri namna ya kufanya mageuzi mbalimbali ndani ya chama.
Rais Kikwete alisema wao ndani ya chama , hawana
hofu ya kuwatumia wazee hao kwa njia hiyo kwa kuwa itakuwa njia mwafaka
ya kutoa ushuri wao kwa namna watakavyoona inafaa.
Alipuuza madai kwamba wazee hao wanaondolewa
kwenye vikao vya uamuzi, akisema mbali na mapendekezo ya Kamati ya
Mukama, pia wazee hao walikuwa wanachoka kuitwa mara kwa mara kwenye
vikao.
“Tumekuwa tukiwaita kwenye vikao vyetu na wao
wanahoji, ’kwanini mnatusumbua nyinyi hamuwezi kuamua wenyewe, wanasema
kama kuna jambo la muhimu sana…wanasema ‘sisi tumeshatimiza wajibu wetu
na nyingi timizeni wajibu wenu,” alisema.
Alisema hata kwenye vikao, wastaafu hao walikuwa
wanaona taabu kuzungumza kwa kuhisi kuwa wangeweza kuonekana
wanamwingilia mwenyekiti, jambo ambalo halitakuwapo wakiwa peke yao, kwa
kuwa watakaa na kuamua nini cha kushauri na namna ya kushauri.