Kwa ufupi
Wapo vijana wengi nchini ambao wamekumbana na
mitihani ya maisha ambayo kwa namna moja au nyingine imewajeruhi na
hivyo wanaona kuwa huo ndiyo mwisho wa mafanikio katika ulimwengu huu.
Baada ya miaka miwili ya ndoa yake, Jennifer
Tress kutoka Washington DC, Marekani alibaini kuwa mume wake ana
uhusiano wa kimapenzi na mfanyakazi mwenzake.
Huo ulikuwa mwanzo wa filamu yenyewe, kwani alipomhoji kwa nini anamsaliti, alijibiwa ni kwa sababu yeye (Tress) si mrembo.
Tress aliumizwa na uzinzi wa mume wake, lakini zaidi hasa kwa kauli ya mume wake ya kumwambia ni mbaya kwa sura.
Hata hivyo, baada ya ndoa kuvunjika aliandika
kitabu na kuzindua mtandao unaoitwa, ‘youre not pretty enough’ (wewe si
mrembo kamili)ambao unawakutanisha wanawake wenye changamoto katika
ndoa.
Mtandao huu na kitabu kwa sasa vinamwezesha kupata
fedha kwa sababu ya kuwa na wanachama wengi, lakini si hivyo tu, bali
Tress amekuwa maarufu na huitwa katika mabaraza mbalimbali ya wanawake
kutoa ushuhuda.
Yawezekana hata wewe umeshawahi kupitia mtihani wa
maisha kama wa Tress, nikuombe wewe usikate tamaa na kuona kuwa huo ni
mwisho wa maisha, bali itumie changamoto hiyo kukuimarisha zaidi na
kukupa mwanga wa mafanikio.
Wapo vijana wengi nchini ambao wamekumbana na
mitihani ya maisha ambayo kwa namna moja au nyingine imewajeruhi na
hivyo wanaona kuwa huo ndiyo mwisho wa mafanikio katika ulimwengu huu.
Hilo si kusudio la Mungu kwa mwanadamu. Maisha
yanapokupa sababu 100 za kulia, yaonyeshe maisha kuwa una sababu 1,000
za kucheka.
Wapo wale waliowahi kupata ujauzito wakiwa shule,
hivyo wakadhani kuwa huo ndiyo mwisho wa elimu au mwisho wa kuwa
msichana mrembo.
Wapo wengine ambao wamepata ajali na kupoteza
viungo vya miili yao jambo lililowafanya wakate tamaa ya maisha na
kudhani kuwa hawataweza kuthaminika au kujipatia riziki katika dunia hii
na wapo wenye historia mbaya ambazo wanashindwa kuzisahau na
zinawafanya washindwe kusonga mbele.
Mwanasayansi, mgunduzi na mkandarasi, Alexander
Graham Bell aliwahi kuandika katika moja ya vitabu vyake kuwa, mlango
mmoja unapofungwa, mwingine hufunguliwa, lakini tatizo la mwanadamu ni
kuwa huuangalia kwa muda mrefu na kwa kujutia, mlango uliofungwa kiasi
cha kushindwa kuuona mlango ulio wazi.
Wengi wetu huongozwa zaidi katika mitazamo ya kibinadamu na kuona kuwa hakuna nafasi ya kufanya vyema tena duniani.
Kwa mfano, wapo wanaoamua kujitoa uhai kwa sababu tu, amefeli
mtihani wa kidato cha nne au ameachwa na rafiki wa kiume au wa kike.
Hapana shaka huku ni kukata tamaa kulikopita kiasi ambako humfanya
mwanadamu hushindwa kukabiliana na tatizo lililopo mbele yake.
Hivyo, sivyo inavyotakiwa kutendwa na mtu yeyote
katika maisha, siri ni moja kuyakanyaga, kuyatupa jalalani na kuyasahau
matatizo kisha safisha njia mpya ya kuingia katika mafanikio. Kwa mfano,
wapo ambao wamewahi kuishi katika mienendo mibaya mno wakati wa ujana
wao, pengine walikuwa walevi, watumiaji wa dawa za kulevya, wazinzi au
hata majambazi.
Historia zao zisiwe chanzo cha kushindwa kusonga
mbele na kuyarudia waliyoyatenda bali ziwe elimu kwa wengine na elimu
katika maisha binafsi.
Kama wewe ni mmoja wa watu wenye historia mbaya,
usihofu, kwani wanazuoni wanatueleza kuwa, tofauti ya pekee iliyopo kati
ya mwenye dhambi na ajiitaye mtakatifu duniani, ni kuwa kila mtakatifu
ana historia na kila mwenye dhambi ana mustakabali.
Lucius Seneca, mwanafalsafa wa Kirumi anatoa
mwongozo wake wa maisha na kusema kuwa changamoto katika maisha
zinaimarisha ufahamu, kama ambavyo uchungu wa kuzaa unaleta maisha ya
kiumbe duniani.
Mfano mzuri ni wa mwanahabari wa Mlimani Radio,
Tuma Dandi ambaye licha ya kupata ajali iliyomfanya apooze sehemu kubwa
ya mwili wake, hakukata tamaa, alisoma kwa bidii na kufanya kazi kwa
kujituma na sasa ni mhariri na mwanahabari aliyepata tuzo kadhaa za
umahiri.
Changamoto zisikukatishe tamaa, kama unakimbia na
kukutana na ukuta, usigeuke nyuma na kurudi ulikotoka. Tafuta njia ya
kuupanda, zunguka ukuta na utafute njia yeyote kuhakikisha unaukwea na
kufanikiwa kufika upande wa pili.
Ewe Mtanzania mwenzangu, kumbuka kuwa
unapolalamika kuwa huna viatu, basi kumbuka wapo wenzio ambao hawana
miguu. Kimbia peku peku, tengeneza picha ya mafanikio katika ufahamu,
igonge mhuri na hakikisha haifutiki…hakika utayafikia mafanikio hayo.
Ni vyema ukaugeuza udhaifu wowote, changamoto au
historia mbaya katika maisha yako kuwa nguvu mbadala ya mafanikio yako.
Kama wewe ni yatima, soma sana, jitume kwa bidii kwa sababu huna wa
kumtegemea, hivyo elimu na bidii ya kazi, ndiyo nguzo yako.
Vilevile, kama wewe ni mlemavu, huo usiwe mwanzo
wa kukata tamaa, bali tumia nafasi yeyote katika ufahamu na mwili wako
kutengeneza njia ya kutokea.
0754-438084
source: Mwananchi
source: Mwananchi