Kwa ufupi
- Alisema mmoja wa majambazi hao alikuwa ni mtu mwenye asili ya Asia na kwamba walikuwa wakizungumza Kiingereza kuwasiliana.
Dar es Salaam. Watu wanane wanaodhaniwa kuwa
majambazi, jana walipora zaidi ya Sh900 milioni katika Tawi la Benki ya
Habib, Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Wizi huo ulitokea saa tatu asubuhi kwenye benki hiyo iliyoko makutano ya Mitaa ya Livingstone na Uhuru.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Kamishna Suleiman Kova alisema fedha zilizoibwa ni Sh700 milioni na Dola
za Marekani 181,885 (Sh285,444,000).
Kamanda Kova alisema wameanza kuwasaka majambazi hao waliohusika katika tukio hilo.
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Kova alisema
majambazi hao walifika kwenye benki hiyo na kuingia ndani moja kwa moja
na kujifanya ni wateja ambao walikuwa wamesindikizwa na mtu mmoja
aliyekuwa amevaa sare za polisi.
Baada ya kuingia ndani, alisema waliwaweka chini
ya ulinzi wafanyakazi wa benki hiyo pamoja na wateja wanne waliokuwepo
ndani wakipata huduma.
“Wananchi waliokuwa nje ya benki hawakujua
chochote kinachoendelea huku dereva wa teksi aliyeambatana nao akipewa
jukumu la kuangalia ulinzi nje huku akiwa na ‘radio call’,” alisema
Kova.
Alisema mmoja wa majambazi hao alikuwa ni mtu mwenye asili ya Asia na kwamba walikuwa wakizungumza Kiingereza kuwasiliana.
Kamanda Kova alisema majambazi hao walikuwa
yanafahamu majina ya watumishi wa benki hiyo akiwamo Meneja wake, Daniel
Matemba jambo ambalo lilirahisisha kutekeleza uhalifu wao.
“Cha ajabu walianza kuwaita majina watumishi
wawili pamoja na meneja na kuwaamuru watoe funguo za chumba cha
kuhifadhia fedha baada ya kuchukua fedha zilizokuwa karibu,” alisema
Kamanda Kova na kuongeza kuwa licha ya meneja huyo kuambiwa na
wafanyakazi wake atoe taarifa kwenye Kampuni ya Ulinzi ya Security Group
inayohusika na kulinda benki hiyo kwa kubonyeza kitufe maalumu
alishindwa na badala yake kutii amri ya majamabazi hao.
Kamanda Kova alisema licha ya baadhi ya milango ya
vyumba kufunguliwa kwa siri, ilikuwa ni kazi nyepesi kwa majambazi
kuingia na kuchukua walichohitaji pasipo wananchi waliokuwa nje kujua
kinachoendelea.
“Baada ya kuchukua fedha hizo majambazi hao
walitoka nje kama vile wanatoka bafuni kuoga, yaani bila wasiwasi wowote
na waliingia kwenye gari lao na kutokomea kiulaini,” alisema Kamanda
Kova.
Alisema polisi imetangaza dau la Sh100 milioni kwa mtu atakayefanikisha kupatikana kwa taarifa za kukamatwa kwa majambazi hao.
source -: Mwananchi
Alisema polisi imetangaza dau la Sh100 milioni kwa mtu atakayefanikisha kupatikana kwa taarifa za kukamatwa kwa majambazi hao.
source -: Mwananchi