Kwa ufupi
Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi zilisema Mbowe
alikamatwa saa moja asubuhi alipokuwa katika Hoteli ya A.M Country Side,
nje kidogo ya Mji wa Iringa alipokuwa amefikia.
Iringa. Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe na viongozi wengine wa chama hicho, jana walishikiliwa na
polisi kwa zaidi ya saa tano kwa tuhuma za kuzidisha muda katika mkutano
wa hadhara uliofanyika hapa juzi.
Baada ya kuhojiwa, waliachiwa kwa dhamana ya Sh2 milioni kila mmoja.
Wanatuhumiwa kuzidisha dakika 25 za mkutano huo
ambao ulikuwa maalumu kwa ajili ya kukusanya maoni ya Rasimu ya Katiba
Mpya uliofanyika juzi katika Viwanja vya Mwembetogwa, Iringa na
kuhudhuriwa na mamia ya wananchi.
Viongozi wengine wa chama hicho waliokamatwa ni
Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni ambaye ni Mbunge wa Singida
Mashariki, Tundu Lissu, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa
na Diwani wa Kata ya Mivinjeni, Iringa, Frank Nyalusi.
Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi zilisema Mbowe
alikamatwa saa moja asubuhi alipokuwa katika Hoteli ya A.M Country Side,
nje kidogo ya Mji wa Iringa alipokuwa amefikia.
Kamanda Mungi alisema Mbowe na wenzake walizidisha
muda walipokuwa wakihutubia mkutano huo kitendo ambacho alisema ni
kinyume cha sheria. Alisema jeshi hilo linawahoji na wakibainika kuwa na
makosa watafikishwa mahakamani.
“Ratiba yao ilielekeza kuwa wangefika na kuanza
mkutano wa kwanza katika Wilaya ya Mufindi saa 4.00 asubuhi lakini wao
waliwasili saa 9.00 alasiri,” alisema.
Alisema muda wote huo polisi walikuwa eneo la
mkutano kwa ajili ya ulinzi lakini hapakuwa na taarifa yoyote ya
mabadiliko ya muda hadi walipowasili saa 9.00 alasiri.
Alisema kwa mujibu wa ratiba yao walipaswa kuanzia
saa 6:00 mchana hadi saa 8:00 wafanye mkutano wao katika Tarafa ya
Ilula wilayani Kilolo lakini walifika saa 10:51 jioni.
Alisema walivumilia hayo lakini viongozi hao
wakazidisha muda walipofika katika Viwanja vya Iringa Mjini ambako
walianza mikutano saa 9.00 alasiri na kumaliza saa 12.25 jioni.
“Licha ya kuwakumbusha mara kwa mara hususan Mbowe
aliyekuwa akihutubia mkutano huo, alikaidi agizo la Polisi na kama
polisi wangeamua kupanda jukwaani na kuwashusha wangeweza kusababisha
vurugu.
Juzi, akifunga mkutano wa hadhara uliolenga
kukusanya maoni ya Rasimu ya Katiba, Mbowe aliwapongeza polisi wa Iringa
kwa uvumilivu, akidai wametumia busara wakati wa kusimamia mkutano huo.
“Naomba mniongeze dakika 10, ninawapongeza polisi wa Iringa kwa kuwa wavumilivu na kutumia busara wakati wote wa mkutano huu licha ya kuwa nimezidisha muda kwani wangekuwa askari wa maeneo mengine wangeanza kupiga mabomu,” alisema Mbowe.
source: Mwananchi news paper