Kwa ufupi
Upanga huo wenye uzito wa takriban kilo tatu na
wenye thamani ya zaidi ya fedha za Tanzania Sh600 milioni, ni kielelezo
kwa nchi inayokabidhiwa uongozi wa SARPCCO.
Jeshi la Polisi limeingia katika kashfa nzito
baada ya mkuu wake, Inspekta Jenerali Said Mwema, kuibiwa upanga wa
dhahabu ambao ni mali ya Shirikisho la Wakuu wa Majeshi ya Polisi wa
nchi za Kusini mwa Afrika (SARPCCO).
Upanga huo wenye uzito wa takriban kilo tatu na
wenye thamani ya zaidi ya fedha za Tanzania Sh600 milioni, ni kielelezo
kwa nchi inayokabidhiwa uongozi wa SARPCCO.
Mwaka jana Tanzania ilikuwa mwenyekiti wa SARPCCO,
ambapo upanga huo ulikabidhiwa kwa IGP Mwema na Jenerali Magwashi
Victoria ‘Riah’ Phiyega, ambaye ni Kamishna wa Taifa wa Polisi wa Afrika
Kusini aliyekuwa amemaliza muda wake kwa wakati huo.
Hilo ni tukio la pili la wizi la mali zinazohusu
ofisi ya IGP, ambapo mwaka jana ndani ya ofisi hiyo kuliibwa kompyuta
ndogo (laptop), ikiwa na taarifa muhimu za kipolisi. Hadi sasa hakuna
taarifa za kupatikana kwa kompyuta hiyo.
IGP Mwema alikabidhiwa upanga huo Septemba 5,
2012, katika mkutano saba wa SARPCCO uliofanyika Zanzibar na kuhudhuriwa
na wakuu wa majeshi ya Polisi kutoka nchi 13, pamoja na mashirika ya
kimataifa.
Upanga huo ambao unakwenda sambamba na bendera ya
SARPCCO, ni moja ya vielelezo vya nchi iliyochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa
shirikisho hilo, ambaye moja kwa moja anakuwa ni Mkuu wa Jeshi la
Polisi katika nchi husika.
Kwa mujibu wa taratibu za SARPCCO, vielelezo hivyo
hutakiwa kuwekwa ofisini kwa kiongozi husika, ikiwa ni alama ya kila
mgeni atakayeingia ofisini hapo kutambua uwepo wa wadhifa huo wa
kimataifa.
Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa IGP
aligundua kutoweka kwa upanga huo wiki iliyopita, wakati akijiandaa
kwenda kuukabidhi kwa mwenyekiti mpya wa SARPCCO, ambaye ni IGP wa
Namibia.
Taarifa za ndani ya jeshi hilo zilibaini kuwa, IGP
alilazimika kuondoka bila upanga huo alipokwenda Namibia wiki iliyopita
kuhudhuria mkutano wa nane wa SARPCCO, uliofanyika Jumapili iliyopita
mjini Windhoek.
Kwa mujibu wa uchunguzi, IGP Mwema alikabidhi
upanga unaofanana na huo ambao siyo wa dhahabu, alioazimwa kutoka kwa
Mkuu wa Jeshi la Polisi la Namibia, Inspekta Jenerali, Luteni Jenerali
Sebastian Ndeitunga, na kukabidhiwa kama ishara ya kukabidhiwa uenyekiti
wa SARPCCO kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Uchunguzi ulibaini kuwa IGP Mwema alitoa ahadi ya
kurejesha upanga halisi ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, au Serikali ya
Tanzania italazimika kutengeneza mwingine kulipa uliopotea.
Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa kashfa
hiyo ametupiwa Mkuu wa Polisi Zanzibar, Kamishna Mussa Ali Mussa pamoja
na dereva wake, ikidaiwa kuwa upanga huo baada ya kupokewa na IGP Mwema,
Septemba mwaka jana uliwekwa kwenye gari la kamishna huyo.
Kamishna Mussa ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi
ya Mkutano wa Saba, na pia ofisa mwenyeji kwa wajumbe wa mkutano huo
uliofanyika Zanzibar.
Hata hivyo, taarifa zingine zilidai kuwa IGP Mwema
naye analaumiwa kwa kutofuatilia kwa karibu zana za kazi, kwani baada
ya kuupokea alitakiwa kuhakikisha unakuwepo ofisini kwake kama alama ya
uenyekiti wake.
Gazeti hili lilipowasiliana kwa njia ya simu na
Mkuu wa Polisi Zanzibar, Kamishna Mussa Ali Mussa kuhusu madai hayo
alisema, kitara (upanga) hicho ni kweli kimepotea, lakini yeye hahusiki
kwa kuwa kila kitu kina utaratibu wake.
“Ni kweli kitara kilikabidhiwa kwa afande IGP na
mimi nilishuhudia kikikabidhiwa, na ni kweli kitara hakijulikani kiliko,
lakini mimi sihusiki na kupotea kwake. Ni kweli mimi nilikuwa ofisa
mwenyeji wa mkutano huo, lakini siku hiyo zilitolewa zawadi nyingi, watu
walipewa mikoba, kwa hiyo mtu akipoteza mkoba wake niulizwe mimi?”
alihoji Kamishna Mussa.
Alisema kila kitu kina utaratibu wake na kwamba
taarifa kwamba yeye amehojiwa kutokana na upotevu wa kitara hicho au
kuna kamati imeundwa, hazina ukweli.
“Sijawahi kuona kamati hiyo. Kamati hiyo kwanza
imeundwa na nani na inatoka wapi? Hayo maneno yanatengenezwa na watu wa
nje,” alisema Kamishna Mussa.
Alisema kinachofanyika hivi sasa ni kukitafuta ili kiweze kurejeshwa kunakohusika.
Taarifa zingine zilidai hata bendera ya mezani ya
mwenyekiti wa SARPCCO, aliyokabidhiwa sambamba na upanga huo nayo kuna
hatihati ilipotea.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso alipotakiwa kuzungumzia suala hilo alisema aulizwe kamishina wa polisi Zanzibar.
“Suala hilo muulize Kamishina wa Zanzibar ndiye anayejua,” alisema Senso.
Uchunguzi unaonyesha kuwa maofisa katika ofisi ya
IGP na ile ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, wamehojiwa akiwamo Kamishna
Mussa, na kwamba upelelezi mkubwa umekuwa ukiendelea ndani ya jeshi
hilo.
Hata hivyo, juhudi za gazeti hili za kutaka
kufahamu uamuzi wa SARPCCO katika ofisi yake ya uratibu iliyopo kwenye
ofisi za Makao Makuu ya Kanda ya Polisi wa Kimataifa (INTERPOL), Harare,
Zimbabwe, hazikuzaa matunda baada ya baruapepe iliyotumwa kwa ofisa
mratibu wa SARPCCO ambaye pia ni mkuu wa ofisi ya Kanda ya INTERPOL, C.
Simfukwe kutopata majibu.
SARPCCO ilianzishwa mwaka 1995, Victoria Falls, Zimbabwe, lakini
kisheria ilitambulika rasmi mwaka 2006 na lengo lake kuu ni kupambana
na uhalifu wa kuvuka mipaka.
Uenyekiti wake ni mwaka mmoja, ambapo kwa sasa
mwenyekiti ni Mkuu wa Jeshi la Polisi la Namibia Inspekta Jenerali,
Luteni Jenerali Sebastian Ndeitunga, aliyepokea wadhifa huo kutoka kwa
IGP Mwema.
source: Mwananchi
source: Mwananchi