Thursday 19 September 2013

‘Mnigeria wa dawa za kulevya hakupita Tanzania’


Raia wa Nageria anayetuhumiwa na kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, Emmanuel Peter Inobembe akiwa Mahakama ya Nairobi alipofikishwa ujibu tuhuma hizo. Picha na Paul Waweru 
Na Mussa Juma, Mwananchi

Posted  Alhamisi,Septemba19  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Ninachoweza kusema,sisi hatuna taarifa kama mtu huyu alipitia Namanga katika mpaka wetu.

Arusha.Idara ya Uhamiaji mkoani hapa,imeeleza kuwa raia wa Nigeria aliyefukuzwa Kenya kwa kuhusishwa na dawa za kulevya, Enobenhe Emanuel Peter hajaingia nchini kupitia mpaka wa Namanga uliopo wilayani Longido.
Akizungumza na mwananchi jana, Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Arusha, Daniel Namomba alisema, baada ya juzi na jana kupitia kumbukumbu za wageni wote waliopita katika mpaka huo,hakuna jina la Mnigeria huyo.
“Baada ya vyombo vya habari kuripoti juu ya Mnaigeria huyu kuwa alipitia Namanga tumefanya uchunguzi na hakuna kumbukumbu zozote kuwa alipita katika mpaka huo,”alisema Namomba.
Alisema Peter mwenye pasi ya kusafiria namba 02743350 kama angepita katika mpaka huo,kumbukumbu zake zingeonekana.
“Ninachoweza kusema,sisi hatuna taarifa kama mtu huyu alipitia Namanga katika mpaka wetu,”alisema Namomba.
Raia huyo wa Nigeria ambaye amekuwa akitumia majina mbali mbali,alifukuzwa Kenya miezi minne iliyopita kwa kuhusishwa na biashara ya dawa za kulevya lakini alikamatwa tena hivi karibuni,akiwa na pakti 425 za heroini na ilielezwa alirejea Kenya akitokea Tanzania.
Wakati huo huo,Idara ya Uhamiaji mkoani Arusha,imefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu,222 ambapo kati yao 80 wamefungwa.
Namomba alisema,kati ya wahamiaji hao, walowezi ni 68 na hadi sasa kesi mbili bado zinaendelea mahakamani na wengine wamerejeshwa makwao.

SOURCE: MWANANCHI