Friday 21 June 2013

Nassari: Lowassa anahusika kunipiga

Mbunge wa Arumeru Mashariki(Chadema) Joshua Nassari akiwa amelazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), jana, baada ya kuhamishwa kutoka Arusha kwa ajili ya kupata matibabu zaidi baada ya kuumizwa kwenye vurugu za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Makuyuni mkoani Arusha.Picha na Silvan Kiwale 
Na Beatrice Moses  (email the author)

Posted  Alhamisi,Juni20  2013  saa 21:28 PM
Kwa ufupi
  • Amemtuhumu pia Spika wa Bunge, Anne Makinda kuwa miongoni mwa watu wanaomchukia .


Dar es Salaam. Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari amemtuhumu Mbunge wa Monduli Edward Lowassa kwamba anahusika na kipigo alichokipata kutokana na chuki aliyonayo kwake.
Aidha amemtuhumu Spika wa Bunge, Anne Makinda kwamba naye ni miongoni mwa watu wanaomchukia pamoja na viongozi wengine wa Bunge, kwa kuwa hakuna kati yao aliyempigia simu au kumtumia ujumbe wa kumjulia hali kutokana na kipigo alichopata ambacho kimemsababishia maumivu makali.
Akizungumza jana akiwa kwenye chumba alicholazwa katika Taasisi ya Tiba ya Magonjwa ya Mifupa na Ufahamu Muhimbili (Moi), Nassari alidai Lowassa ambaye amewahi kuwa waziri mkuu kabla ya kujiuzulu, amemchukia tangu alipomshinda mkwewe Sioi Sumari, kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge uliofanyika Aprili mwaka jana.
Nassari aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Selian ya jijini Arusha kabla ya kuhamishiwa MOI, alidai kupigwa na kuchaniwa nguo na Green Guard wakati alipokuwa katika jitihada zake za kuhesabu kura kwenye uchaguzi wa udiwani wa Kata ya Makuyuni-Monduli.
“Kipigo nilichopata Lowassa anahusika ananichukia, anataka urais lakini hawezi kuupata kwa kuuumiza watu kama hivi, alifikiri kwamba nitakufa sitakufa hadi kwa mapenzi ya Mungu,” alisema.
Alisema kuna jambo ambalo wananchi wanapaswa kulifikiria ni jinsi ambavyo kumekuwa na matukio ya kutekwa na kuvamiwa, lakini hakuna yanayohusisha kiongozi wa CCM, badala yake ni raia wa kawaida na viongozi wa dini na siasa. Nassari alidai akiwa kama wakala mkuu wa Chadema katika kata hiyo, alikumbana na mambo kadhaa yaliyomshangaza, ikiwa ni pamoja na kufanyiwa jaribio la kutekwa mara mbili, kabla ya kushambuliwa kwa kipigo.
Alisema pia anashukuru kwamba askari wawili waliokuwepo katika eneo hilo walijitahidi kutaka kumnusuru, lakini walizidiwa nguvu na vijana hao, hasa kutokana na kutokuwa na bunduki, ambapo yeye alipofanikiwa kuchoropoka alikimbilia bastola yake na kuwanyoshea vijana hao bila kufyatua.
Akizungumzia kuhusu hali yake, Nassari alisema amepimwa kipimo cha X-ray ambapo imeonyesha kuwa pingili za mgongo wake zipo sawa, lakini daktari ameshauri afanyiwe kipimo kingine kiitwacho MRI ili kuangalia hali ya mishipa kutokana na maumivu makali anayoendelea kuyapata.
Aidha alitumia fursa hiyo kumshukuru Mbunge wa Kuteuliwa, Joseph Mbatia kuwa ndiye aliyemsaidia kufanya mipango kuwasiliana na uongozi wa Bunge na kumwezesha kuhamishiwa Moi, baada ya wabunge wote wa Chadema kwenda Arusha kushughulikia waliofariki kwa bomu.
Hata hivyo, Lowassa alipotafutwa kuhusiana na tuhuma hizo alikataa kuzungumzia suala hilo na kusema hilo aulizwe Msimamizi wa Uchaguzi, Paulo Kitaleki.
Mwananchi ilimtafuta Kitaleki ambaye pia ni katibu tarafa, alikanusha kuhusika kwa Lowassa akielezea kuwa siku ya tukio hilo alikuwa Geita.
“Huyu Nassari ni mwigizaji na anafaa kuwa msanii kwa kuwa anaigiza tu hata hakupigwa, bali yeye ndiyo aliyempiga Wakala wa CCM, Hussein Osama ambaye ni mlemavu, kisha akatimua mbio baada ya vijana kutaka kumkamata, nashangaa kumwona yupo hospitali akidai kupigwa, siyo kweli,” alisema Kitaleki.