Wednesday 12 June 2013

Hali ya Mzee Mandela ni tete, wasiwasi watanda, familia yake yaanza kurejea Afrika kusini


Posted  Jumanne,Juni11  2013  saa 21:32 PM
Kwa ufupi
  • Mwanaye wa kwanza, Zenani Mandela-Dlamini ambaye ni Balozi wa Afrika Kusini nchini Argentina amewasili Pretoria kufuatilia hali ya baba yake aliyelazwa hospitali Jumamosi iliyopita.

Johannesburg. Wasiwasi umezidi kutanda miongoni mwa familia na raia wa Afrika Kusini kuhusu afya ya Rais wa zamani wa nchi hiyo, Nelson Mandela ambaye amekuwa akipatiwa matibabu kwenye Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) kwenye Hospitali ya Mediclinic, Pretoria, Afrika Kusini.
Tayari wanafamilia wake wameanza kurejea Afrika Kusini kutoka maeneo mbalimbali duniani na ndani ya Afrika Kusini na kuelekea Pretoria kufuatilia kwa karibu hali yake. Kwa mujibu wa taarifa za kitabibu, Mzee Mandela (94) ambaye ni maarufu kwa jina la Madiba, hajitambui. Amelazwa hospitalini kwa siku ya tano sasa ambako anaendelea kupatiwa matibabu kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu.
Mwanaye wa kwanza, Zenani Mandela-Dlamini ambaye ni Balozi wa Afrika Kusini nchini Argentina amewasili Pretoria kufuatilia hali ya baba yake aliyelazwa hospitali Jumamosi iliyopita.
Mkewe, Graca Machel alilazimika kuahirisha safari yake ya kikazi tangu Jumamosi ili kuwa karibu naye na mke wake wa zamani ambaye walitalikiana, Winnie Mandela pia ni miongoni mwa jamaa waliojumuika kumjulia hali Rais huyo wa Kwanza mweusi wa Afrika Kusini.
Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), lilisema kwamba Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma jana alikutana na madaktari wanaomtibu Mzee Mandela na baadaye kutoa taarifa fupi akisema ameridhishwa na jitihada wanazofanya katika kumpatia matibabu.
Kijijini kwake
Huko kijijini kwake Qunu, wakazi wameendelea kukumbwa na shaka na wamekuwa wakifanya maombi ili afya ya Mandela iimarike.
Tayari baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa vimeshaweka kambi katika eneo hilo la Qunu kwa ajili ya kuchukua matukio mbalimbali yanayoendelea katika kipindi hiki cha shaka na wasiwasi kuhusu kiongozi huyo.
Jana, Msemaji wa Ikulu ya Afrika Kusini, Mac Maharanji alisema hali yake haijabadilika.