Wednesday 19 June 2013

Mbowe:Walitaka kuniua , Mwema na Kikwete watoa Pole kwa Mbowe.








Jumatatu, Juni 17, 2013 05:52 Abraham Gwandu na Eliya Mbonea
*IGP Mwema aunda kikosi kazi
   *JK awatumia pole Chadema

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
MWENYEKITI Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Freeman Mbowe amesema tukio la mlipuko wa bomu lililoua watu wawili juzi mkoani Arusha, lilimlenga yeye na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Arusha jana, Mbowe alisema bomu hilo ambalo liliambatana na milio ya risasi lilikusudiwa wazi kuondoa uhai wake, jambo ambalo ni hatari kwa uhai wa taifa.


Alisema katika tukio hilo, kulikuwa silaha za aina tatu ambazo zilitumika, ukiondoa bomu, kulikuwa na bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG) na bastola.

“Waliopanga unyama ule walilenga kutuua sisi, waliokufa wamekufa kwa niaba yetu,

“Watu hawa, waliandaliwa na wengine walikuwa katikati ya umati wa watu, waliokuwa pembezoni mwa uwanja, tumebaini wanalindwa na polisi,

“Risasi za SMG zilitoboa tanki la mafuta la gari letu la matangazo, ambalo sisi tulikuwemo juu, lengo likiwa baada ya bomu kulipuliwa,tanki nalo lingelipuka,

“Hawa walitaka kufanya mauaji halaiki, ikiwemo sisi viongozi wa Chadema, Mungu bado anatusimamia,”alisema

Alisema majeruhi wote ambao wamelazwa, bado wana vyuma vingi milini mwao kutokana na kujeruhiwa vibaya.

“Tumepiga picha makasha ya risasi na kuyakabidhi polisi,bado tunaamini,kwa sababu tukio hili halihitaji mashine ya kiuchunguzi ya mwezini vyombo vya usalama, vitatoa taarifa mapema,”alisema Mbowe.

Kutokana na msiba huo, Mbowe alitangaza kuwa wabunge wa chama hicho, wote kuanzia leo hawatashiriki mkutano wa Bunge la Bajeti hadi marehemu watakapozikwa.

“Msiba huu, umekigusa chama,wanachama,wapenzi na wananchi wote wa Tanzania,wabunge wote watakuwa bega kwa bega na wananchi wa Arusha mpaka watakapopumzishwa marehemu,”alisema Mbowe

Alisema mazishi ya marehemu wote, yatafanyika kitaifa kwenye Viwanja vya Soweto, kabla ya marehemu wote kusafirishwa na ndugu zao.

“Chama kinauchukulia msiba huu kama msiba wa taifa,tumeamua kupiga mahema katika uwanja ule na marehemu wataagiwa hapo ambapo moja ni atazikwa Kilimanjaro na mwingine Tabora”

“Tukio hili ni la kisiasa na limepangwa, ninawataka wenzetu kama shughuli za siasa zimewashinda wafute mfumo wa vyama vingi ili wananchi wasio na hatia wasiendelee kufa”

Alisema chama kitafanya harambee kuchangia majeruhi kwa ajili ya matibabu yao.


IGP Mwema
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP),Said Mwema amesema jeshi hilo, limefanikiwa kunasa mchoro na wajihi wa mtu aliyehusika

Alisema kupatikana kwa michoro hiyo,kumesaidia kuendesha msako mkali nchi nzima ili kuwabaini watu wote waliohusika na mipango hiyo,ambayo inadaiwa kuwa ni ya kigaidi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Dar es Salaam jana, IGP Said Mwema alisema kupatikana kwa michoro hiyo, kutasaidia mno kubaini watu ambao wamekuwa na nia mbaya ya kuchafua sifa ya Tanzania.

“Tumefanikiwa kupata michoro iliyohusika katika tukio hili, nawashukuru wananchi walioanza kutupa taarifa za muonekano wa mtu aliyetupa bomu hilo.

“Natoa wito kwa wananchi kuwa watulivu na kuendelea kutoa ushirikiano, wakati uchunguzi ukiendelea na wenye taarifa wanaweza kunipatia kwa namba yangu ya simu ya kiganjani 0754 785 557,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, IGP Mwema alisema ameunda timu hiyo ya uchunguzi, inayoongozwa na makamishna wawili ambao ni Mkuu wa Oparesheni na Mafunzo, Kamishna Paul Chagonja na Kamishna wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Issaya Mngulu ambao watashirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

K ATUMA SALAMU
Naye Rais Jakaya Kikwete,amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo na kusema amepokea kwa mfadhaiko, mshituko na huzuni taarifa za shambulio la mlipuko lililotokea katika mkutano wa CHADEMA.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu mjini Dar es Salaam kwa vyombo vya habari jana,ilisema Rais Kikwete pia amewatumia salamu za pole viongozi wa CHADEMA kutokana na kutokea kwa tukio hilo, huku akivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua stahiki za kuchunguza kwa haraka, kubaini, kuwakamata na kuwafikisha mbele ya sheria wote waliohusika na tukio hilo.

“Nimepokea kwa mfadhaiko, mshituko na huzuni ubwa shambulio la mlipuko lililotokea katika mkutano wa CHADEMA mjini Arusha jioni ya juzi, tukio ambalo limesababisha vifo na majeruhi ya Watanzania wenzetu.

“Nakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo salamu zangu za rambirambi kutokana na vifo na pole nyingi kutokana na majeruhi katika tukio hilo na naomba kupitia kwako unifikishie salamu zangu za rambirambi kwa jamaa na ndugu wa wafiwa na pole nyingi sana kwa majeruhi,” alisema Rais Kikwete.



Askofu Lebulu
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu alisema mwelekeo wa nchi haueleweki na kwamba hatua kali zinapaswa kuchukuliwa na vyombo vya dola.

Akizungumza wakati wa ibada jana asubuhi katika Kanisa la Mtakatifu Theresa, Askofu Lebulu alionya viongozi na wananchi kuwa wanapaswa kujitizama na kuchukua hatua za haraka kuzuia uonevu.

“Nchi yetu inakwenda mrama, hata mwezi haujaisha vizuri baada ya wale watoto na mama kuuawa na bomu pale Olasiti, leo watoto wengine na mama wamekufa tena kwa bomu.”

 RC Mulongo
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo alisema watu kadhaa wanashikiliwa na vyombo vya dola kutokana na tukio hilo bila kutaja idadi wala majina yao.


chanzo: mtanzania news paper