Saturday 15 June 2013

Mangula: CCM haitakiwi kutoa maoni

 
Na Florence Majani, Mwananchi  (email the author)

Posted  Ijumaa,Juni14  2013  saa 13:4 PM
Kwa ufupi
Akichambua baadhi ya vipengele vya rasimu hiyo, Chikawe  alisema haoni kama ni vyema katiba kuruhusu wananchi kumvua ubunge, mbunge ambaye hajatimiza wajibu wake kwani hali hiyo itazua vurugu na fitina.


Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Philip Mangula amesema viongozi wa chama hicho hawatakiwi kuichambua rasimu ya katiba mpya na kutoa maoni binafsi na badala yake wataitembeza rasimu hiyo kwa wanachama ili waikosoe.

“Unajua sisi ni viongozi na hatutakiwi kutoa maoni binafsi, sisi tunawawakilisha wananchi ambao ni wanachama wa CCM, tutawaplekea hao ili watoe maoni yao” alisema Mangula.
Alisema ni vigumu kwa kikao kimoja cha Kamati Kuu  ya CCM kutoa maoni kwa sababu hao ni wawakilishi tu wa chama, hivyo wanachama wote wa chama hicho watapelekewa rasimu wakaichambue ndipo chama kitatoa msimamo wake.
“Sisi viongozi hatutoi maoni tutaipeleka rasimu kwa wanachama wetu  zaidi ya 6,000 tuyasikie wanayosema, kwa sababu hao ndiyo wananchi” alisema Mangula Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe alizungumza na gazeti hili na kusema kuwa  ni vyema kama  wananchi ambao CCM inawawakilisha wakatoa  maoni kuhusu rasimu hiyo, ingawa nao viongozi wanaweza kuchangia maoni yao kama wananchi wa kawaida.
Akichambua baadhi ya vipengele vya rasimu hiyo, Chikawe  alisema haoni kama ni vyema katiba kuruhusu wananchi kumvua ubunge, mbunge ambaye hajatimiza wajibu wake kwani hali hiyo itazua vurugu na fitina.  Alisema kwa kuwa siasa  unafananishwa na mchezo mchafu, wapinzani wa ndani ya chama wanaweza kufanya fitina na mbunge aliye madarakani kung’olewa pengine bila hata makosa.