Friday 21 June 2013

Lwakatare sasa awaponda polisi

Na Phinias Bashaya, Mwananchi  (email the author)

Posted  Alhamisi,Juni20  2013  saa 21:55 PM
Kwa ufupi

Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare, amesema mfumo wa kuwatafuta wahalifu ndani ya Jeshi la Polisi ni dhaifu kwani pamoja na kutuhumiwa kwa  ugaidi matukio hayo yameendelea kuitikisa nchi katika maeneo mbalimbali.

Akiwahutubia wananchi  wa mjini Bukoba juzi katika Uwanja wa Mashujaa, Lwakatare alidai kuwa aliwaeleza maofisa wa polisi kuwa amegundua udhaifu wa kuhoji  ili kubaini watuhumiwa na kutaka salamu hizo zimfikie Mkuu wa Jeshi hilo Saidi Mwema.
Kwa mujibu wa Lwakatare jeshi hilo bado lina safari ndefu ya kuwapata watuhumiwa sahihi wa makosa ya ugaidi.
Alisema udhaifu uliopo ndiyo unaosababisha matukio hayo yaendelee kutokea na watu kupoteza maisha.
 Alisema siku 92 alizoishi gerezani zimemfundisha mambo mengi na kuwa atatumia siku zote atakazokuwa huru kutoa ushuhuda wa mambo mbalimbali aliyoshuhudia.
Pia Lwakatare alimsifu kiongozi wa Jumuiya za Kiisalamu, Shekhe Issa Ponda kuwa ni kiongozi shupavu aliyemfundisha kuwa jasiri na mtu wa kumwomba Mungu baada ya kuishi naye gerezani kwa siku kadhaa.
Akizungumzia hatima yake kisiasa, kiongozi huyo alisema hana uhakika kama atagombea nafasi ya ubunge lakini alisema hayuko tayari kung’oka  Chadema badala yake ataendelea kupambana na maadui waliomzunguka.
Lwakatare aliwasili mjini Bukoba kwa staili mpya baada ya wananchi waliokuwa wamesubiri uwanja wa ndege tangu asubuhi kutangaziwa kuwa kiongozi huyo angewasili kwa gari akitokea Mwanza.
Alipoulizwa kama mabadiliko hayo ya ghafla ilikuwa ni kukwepa hujuma ambayo ingeweza kutokea wakati wa mapokezi yake, Mwenyekiti wa Chadema Bukoba Mjini, Victor Sherejei alisema kuwa Lwakatare alikosa ndege baada ya kufika Mwanza na hivyo kutumia gari ili kuwahi mkutano.