Thursday 6 June 2013

Spika ampandishia Mbatia kwa kutamka ‘ sumu’






Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia, jana aliingia matatani baada ya kutakiwa kutoa maelezo ya kauli yake kuwa vitabu vilivyopo nchini ni sumu kwa Taifa.

Agizo hilo lilitolewa na Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye alisema kuwa maneno yaliyotolewa na Mbatia ni mazito na kama hayatatolewa ufafanuzi yanaweza kuleta madhara makubwa.
Mbatia alitoa kauli hiyo wakati akiuliza swali la nyongeza kufuatia swali lake na msingi ambalo alitaka kujua vitabu vya hisabati kwa shule za sekondari, ambavyo havikuandikwa kwa ubora unaokubalika.
Mbunge huyo pia alihoji wataalamu ambao walipewa kazi ya kupitia vitabu hivyo hawakuweza kubaini udhaifu huo na kama waliuona licha ya kuwa walitumia zaidi ya Sh24.4 bilioni huku Wizara ikidanganya kuwa vitabu hivyo, vilipewa ithibati mwaka 2011 wakati ithibati ilitolewa Oktoba 2010.
“Huu ni uongo tena uongozi mbaya, na ninataka Waziri atuambie hawa waliotoa majibu ya uongo wanachukulia hatua gani pamoja na kutumia Sh24 bilioni, kwa nini wasifukuzwe kazi, hii ni sumu kali kwa Taifa,” alihoji Mbatia.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo alisema kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ilikubaliana na Chuo Kikuu Cha Jimbo la Carolina na Shirika la Usaid kutumia vitabu vilivyoandikwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar.
Alisema kuwa mpango huo ulifuatia ombi la Rais Jakaya Kikwete la mwaka 2009 ambapo aliomba vitabu vya sayansi na Hisabati kutoka Serikali ya Marekani.
Alikanusha kuwa hakuna sumu yoyote ambayo wataalamu waliiweka katika mitalaa hiyo kwani waliweza kupitia vizuri na kwamba makosa yaliyobainika hayakuwa makubwa.