Friday 14 June 2013

Kenya yaongoza bajeti EAC, Rwanda na Uganda nao wamo

 
Bajeti : Ushuru wapiga hodi kwa watumiaji fedha kwa simu,ahueni kwa wamiliki wa bodaboda, Kenya yaongoza ukanda EAC


Dar es Salaam. Bajeti za nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zilitangazwa jana zikitoa vipaumbele katika masuala ya usalama, afya, kilimo, elimu, nishati na kuboresha miundombinu.
Bajeti hizo zilizotangazwa na mawaziri wa fedha wa nchi hizo sambamba na ile ya Tanzania, ni za Uganda, Rwanda na Kenya ambayo iliongoza kwa ukubwa wa bajeti.
Bajeti hizo zilitofautiana kwa kiasi kikubwa kutokana na mahitaji na vyanzo vya mapato kwa kila nchi.
Mwelekeo wa bajeti hizo pia umelenga kuongeza mapato kupitia vyanzo vya ndani kwa kuongeza ushuru na kodi kwenye vileo, vyombo vya usafiri na bidhaa za anasa.
Kenya Sh28.5 trilioni
Waziri wa Fedha wa Kenya, Henry Rotich alisema kwamba Bajeti ya nchi hiyo kwa mwaka wa Fedha 2013/14 itafikia Sh1.5 trilioni za Kenya (sawa na Sh28.5 trilioni za Tanzania).
Bajeti hiyo ilisomwa jana bungeni jijini Nairobi, ndiyo ya kwanza kwa Rais Uhuru Kenyatta aliyechukua madaraka hivi karibuni.
Moja ya ameneo muhimu yaliyopewa kipaumbele katika bajeti hiyo ni elimu, ambapo Sh17.4 bilioni (Sh330.6 bilioni za Tanzania) zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha mkakati wa Serikali ya Jubilee wa kununua kompyuta ndogo 1,300,000 kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi.
Uganda Sh7.2 trilioni
Waziri wa Fedha wa Uganda, Maria Kiwanuka ametangaza Bajeti ya Serikali ya nchi hiyo kwa mwaka wa Fedha 2013/14 ambapo ambapo Sh 12 trilioni (sawa na Sh7.2 trilioni za Tanzania) zitatumika.
Bajeti hiyo inategemea vyanzo vya ndani vya mapato baada ya misaada ya wafadhili kushuka kwa zaidi ya asilimia 93, kutoka Sh749 bilioni (za Uganda) mwaka 2012/13 hadi Sh50 bilioni za Uganda mwaka 2013/14.
Kiwanuka alisema katika mwaka huu wa fedha, wafadhili wamesaidia asilimia 25 ya bajeti ya nchi hiyo lakini katika mfumo wa mikopo na kufadhili miradi, ambapo matumizi ya Serikali yatafikia Sh8.4 trilioni za Uganda.

Alisema kwamba ili kukabaliana na pengo lililopo la Sh3.6 trilioni, ni lazima kuwepo ongezeko kubwa la mapato kupitia kodi za maji, niashati, mawasiliano ya simu, bodaboda na magari.
Alitaja vipaumbele ambavyo vimezingatiwa kuwa ni pamoja na miundombinu, kukuza uchumi, uwezekaji katika miundombinu na maendeleo..
Rwanda yatenga Sh4.2 trilioni
Waziri wa wa Fedha nchini Rwanda, balozi Claver Gatete ametangaza Bajeti ya Faranga 1.6 trillioni (Sh4.2 trilioni) kwa ajili ya matumizi ya mwaka 2013/14.
Bajeti hiyo imeongezeka ukilinganisha na ile iliyopita ambapo iliyokuwa Faranga 1.4 trillioni. Alisema katika bajeti hiyo kipaumbele kitakuwa kuleta maendeleo ya uchumi na kupunguza umasikini , jambo ambalo ni muhimu kwa Rwanda. Mchango wa wawafadhili katika bejeti hiyo ni Faranga 223.4 bilioni kati ya fedha za maendeleo
Kenya
Pengo la Sh 223 bilioni litazibwa na misada ya nje, na Sh 106.7 bilioni zitapatikana kutoka soko la ndani.