Kwa ufupi
- Alisema Chadema wamekuwa wawazi kwa kufanya mikutano yao nchi nzima, lakini hawakuwahi kusikia CCM wamekusanya maoni jambo ambalo alidai ni la ajabu kwa chama hicho kutaja idadi hiyo.
Katibu mkuu huyo wa Chadema pia alieleza
kusikitishwa kwake na mapendekezo yanayotolewa na CCM kuhusu Katiba
Mpya na kupingana na maoni ya Tume ya Katiba.
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willibrod Slaa ameelezea kusikitishwa kwake na kauli ya
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwamba chama hicho tawala
kimekusanya maoni ya Katiba kwa Watanzania milioni mbili.
Akizungumza jana kwenye mkutano wa hadhara wa
kukusanya maoni ya Katiba, uliofanyika kwenye Viwanja vya Shule ya
Sekondari Turiani, Magomeni, Dar es Salaam Dk Slaa alisema:
“Nimesikitishwa sana na kauli ya Kinana kwamba wamekusanya maoni ya
Katiba yanayofikia milioni mbili jambo ambalo si kweli.”
Alisema Chadema wamekuwa wawazi kwa kufanya
mikutano yao nchi nzima, lakini hawakuwahi kusikia CCM wamekusanya
maoni jambo ambalo alidai ni la ajabu kwa chama hicho kutaja idadi
hiyo.
Akifungua Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec),
Dodoma juzi, Kinana alisema CCM kimekusanya maoni milioni mbili ya
wanachama kuhusu Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba, mchakato unaoendelea
kupitia mabaraza.
Alidai kuwa Kinana alisema uongo kwa sababu
hakuwahi kusikia maoni hayo yakikusanywa kama Chadema kinavyofanya kwa
kuzunguka nchi nzima.
“Sisi tunafanya mikutano yetu ya kukusanya maoni
ya Katiba kwa uwazi, lakini CCM wanatangaza kwa wanachama wao kwamba
wamekusanya maoni milioni mbili bila kueleza njia wanazotumia...
“Chadema imefanya mikutano ya kukusanya maoni nchi nzima na kufanya
mikutano 48.”
Katibu mkuu huyo wa Chadema pia alieleza
kusikitishwa kwake na mapendekezo yanayotolewa na CCM kuhusu Katiba Mpya
na kupingana na maoni ya Tume ya Katiba akisema kinapinga mambo mengi
ya msingi.
“Kuna mambo ya msingi ambayo yana masilahi kwa
taifa na wananchi kwa jumla, lakini wao (CCM), wanataka yasiwepo kwenye
Katiba na wanapingana na Tume,” alisema.
Baadhi ya mambo ambayo Dk Slaa aliyataja ni pamoja
na ubaguzi, rushwa, dhuluma, vitisho na unyanyasaji ambayo alisema
Rasimu ya Katiba imeyapa umuhimu kwa kuyatambua na kueleza kwamba
hayapaswi kufanyika ili kulinda haki za wananchi.
“Ninasikitishwa na CCM kwamba kila jambo ambalo
Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba ameona lina
umuhimu kuwepo kwenye Katiba wao wanapingana nalo kitu ambacho ninaona
hawana nia njema na maisha ya Watanzania na taifa kwa jumla,” alisema.
Aidha, Dk Slaa alizungumzia tukio la kukamatwa kwa
Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe huko Iringa kwa madai ya kuvunja sheria
kwa kuzidisha muda wa kufanya mikutano.
“Polisi ni watu wa kushangaza sana wamemkamata Mbowe kwa madai ya kuvunja sheria, ni kifungu gani kinachoeleza kwamba mtu anaweza kukamatwa kwa jambo hilo? Mimi naona kuna kitu wanachokitafuta kwa Chadema,” alisema Dk Slaa.
source: Mwananchi
“Polisi ni watu wa kushangaza sana wamemkamata Mbowe kwa madai ya kuvunja sheria, ni kifungu gani kinachoeleza kwamba mtu anaweza kukamatwa kwa jambo hilo? Mimi naona kuna kitu wanachokitafuta kwa Chadema,” alisema Dk Slaa.
source: Mwananchi