Kwa ufupi
Sidhani kama ule usemi wa Zanzibar ni njema
atakaye na aje kama kuna mtu atauamini tena. Iweje vyombo vya dola, hasa
polisi wanashindwa
Zanzibar. Niliwahi kusema huko
nyuma kwamba Zanzibar haimalizi mwezi bila kuzuka jambo, siku hizi mambo
yazukayo ni ya ajabu na yenye kusikitisha sana katika jamii yetu.
Mambo hayo kama hayatashughulikiwa kwa nguvu zote
na hasa kama vyombo vya dola havitojirekebisha katika utendaji wa kazi,
inawezekana wananchi wakapungukiwa imani navyo.
Vitendo vya watu wasiokuwa na hatia kumwagiwa
tindikali ni vitendo ambavyo vinaweza kutafsiriwa kama ni ishara ya
vyombo hivyo kushindwa kutimiza wajibu wao wa kuwalinda raia.
Hii ni kwa sababu tukio la kumwagiwa tindikali kwa
Padri wa Parokia ya Machui, Anselmo Mwang’amba limepangwa na
kutekelezwa ikiwa ni mwezi mmoja tangu raia wawili wa Uingereza, Kate
Gee na Kirstie Trup walipomwagiwa tindikali, maeneo ya Mji Mkongwe
wakati wa Magharibi.
Shambulizi hilo lilifanyika katika eneo la
Shangani katika Mji Mkongwe wa Zanzibar. Tukio hili ni mfululizo wa
matukio kadhaa ya watu kushambuliwa kwa kumwagiwa tindikali hapa
Zanzibar.
Baadhi ya matukio, kwa mfano kumwagiwa tindikali
kwa Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga,
kumwagiwa tindikali kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa
hatujapata kusikia kama kuna watu waliokamatwa na kufikishwa mahakani!
Ni jambo la kusikitisha na linalovunja moyo kuona kwamba Zanzibar
iliyokuwa ikisifika kwa hali ya amani, utulivu na ukarimu wa watu wake
leo imekuwa tishio kwa tindikali.
Sidhani kama ule msemo wa Zanzibar njema atakaye
aje sijui kama kuna mtu anayeweza kuja katika hali kama hii, hivi
ninajiuliza inakuwaje vyombo vya dola hasa polisi wanashindwa kubaini
mtandao wa wanaopanga na kutekeleza mashambulizi ya tindikali?
Haiwezekani sehemu kama hii ya Zanzibar dola
ishindwe kubaini watu wanaojihusisha na matukio ya kihalifu kama hayo ya
kuwamwagia tindikali, mpaka lini matukio haya yataendelea Zanzibar?
Ukimya umegubika matukio ya tindikali, hadi leo
licha ya kutoa matamko makali, lakini vyombo hivi havijatuambia sisi
wananchi vimefikia wapi katika kuwasaka wahalifu.
Sasa, suala la kujiuliza kwa nini matukio haya
yanafanyika katika maeneo ya Mkoa wa Mjini Magharibi na si katika mikoa
mingine ya Zanzibar?
Pengine, vyombo hivi vingekuwa na hatua zaidi ya
kutafiti kwanini matukio haya yamejikita kieneo? tatizo la kijamii,
tatizo la kisiasa, tatizo la uchumi au ni jambo gani hili?
Juhudi za makusudi zichukuliwe katika kukomesha
vitendo hivyo na wala suala la siasa lisipewe nafasi katika
kuwashughulikia wahalifu hao wanaotaka kuchafua jina zuri la Zanzibar,
wanaotaka kuharibu uchumi wa nchi, maana hali hiyo inaweza kuwatisha
watalii kutotembelea hapa Zanziba.
Tukiwa raia wema tuungane kwa nguvu moja na Serikali yetu katika
kuwatafuta na kuwafichua wale wote wanaohusika na kuwashambuliwa watu
kwa tindikali.
Tayari, SMZ kupitia kwa Rais wake na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein imetoa msimamo wake katika
kuchukua hatua sahihi kukomesha.
Katika maelezo yake, Dk Shein ameliagiza Jeshi la
Polisi kufanya uchunguzi wa kina na kukabiliana na matukio yakumwagia
watu tindikali.
“Hatuwezi kuviacha vitendo hivi viendelee,ni
lazima Polisi wajitahidi kuwasaka na kuwafikisha katika vyombo vya
sheria wale wote wanaohusika na vitendo hivyo, lazima sheria ichukue
mkondo wake,” aliagiza Dk. Shein.
Je, ni kwa kiasi gani polisi wanaweza kuyafanyia
kazi maagizo haya ya SMZ maana huko nyuma yameshatolewa maagizo ya aina
hiyo na viongozi mbalimbali kwa nyakati tofauti.
Agizo la hivi karibuni ni la Waziri wa Habari,
Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar, Said Ali Mbarouk ameshatoa kauli
ya kuwaomba wananchi washirikiane na vyombo vya dola kuwafichua wahalifu
waliotenda tukio la kumwagiwa tindikali raia wa wawili wa Uingereza.
“Katika kuhakikisha jambo hilo halipewi nafasi
kuendelea tena, Serikali imekusudia kuchukua hatua kadhaa ikiwemo
kuendesha uchunguzi mkali wa kuwasaka wahusika ili kuweza kuwafikisha
kwenye vyombo vya sheria,”alisema Waziri Mbarouk.
Tunafarijika kuona kwamba serikali imeahidi sio tu
kukomesha vitendo hivyo, lakini pia kuanza kuratibu na kusimamia kwa
makini zaidi biashara ya tindikali kwa kutunga sheria itakayoweka
masharti maalum.
“Kwa vile bidhaa ya tindikali katika siku za hivi
karibuni imeanza kutumika vibaya, SMZ inachukua kila hatua kudhibiti
matumizi ya bidhaa hiyo kwa kudhibiti uingizaji, usambazaji, upatikanaji
na utumiaji wa tindikali na inazitaka taasisi zote zinazohusika
zitimize wajibu wake katika matumizi ya tindikali kwa kutumia sheria
iliyopo na kwa haraka kutunga kanuni za kuthibiti uuzaji na matumizi ya
tindikali,” alisema Waziri Mbarouk.
Matukio haya yanaacha maswali mengi vichwani mwa
watu, lakini ni muhimu kutoingiza hisia zozote zaidi ya uhalifu maana
siyo dini wala siasa inayoeleza mtu au kikundi cha watu kufanya vitendo
vya kuvunja sheria kama kilichofanywa. Zanzibar ni moja kati ya nchi
zenye historia kongwe ya uvumilivu wa kidini ambapo pia ina historia
ndefu ya dini Uislamu na Ukristo. Hivyo, ni suala lililo wazi kuwa
vitendo vya watu kumwagiwa tindikali ni vya kihalifu na hakuna budi
tuvikatae.
SOURCE: MWANANHI
SOURCE: MWANANHI