Sunday 29 September 2013

PICHA: Dr. Slaa akutana na majeruhi wa Vita ya Afghanistani; Ajifunza kuhudumia maveterani wetu


Kiongozi Mkuu wa Upinzani nchini Dr. Wilbrod Slaa amesema kuwa Tanzania ina jukumu la kuhakikisha kuwa inatoa huduma muafaka kwa majeruhi wake wa kivita na wanajeshi ambao wanapata madhara wakiwa kazini. Dr. Slaa amesema hayo baada ya kukutana na wanajeshi wa Marekani ambao walijeruhiwa vibaya katika vita huko Afghanistani kwenye hospitali ya Kijeshi ya Walter Reed huko Bethesda Jimbo la Maryland.


Dr. Slaa ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo alikubali mwaliko wa kutembelea majeruhi hao ikiwa ni sehemu ya ziara yake ndefu ya Marekani ambayo inaitwa “Maono Tanzania” ambayo anatumia kujifunza mambo mbalimbali ambayo yanaweza kutumika nchini pia katika kuendeleza utawala wa uwajibikaji, demokrasia na kuharakisha maendeleo. Katika chakula cha mchana na majeruhi hao ambao wengi wao wamepoteza viungo mbalimbali kufuatia milipuko ya mabomu ya kutegwa (Improvised Explosive Devices-IEDs) Dr. Slaa alipata nafasi ya kujifunza jinsi ambavyo serikali ya Marekani inajitahidi kuwahudumia na kuwaonesha kuwajali wapiganaji wake ambao inawatuma katika majukumu mbalimbali ya kijeshi ndani na nje ya Marekani.


Akizungumzia Tanzania Dr. Slaa amesema kuwa serikali ya Tanzania chini ya Chama cha Mapinduzi haina sera iliyotengenezwa yenye kuelekeza utaratibu wa kuwahudumia wapiganaji walioumizwa vitani au wakiwa kazini. “Ni mapungufu makubwa kwani toka Vita ya Kagera na operesheni mbalimbali ukiondoa huduma za awali za matibabu hakuna mfumo mzuri wa kutoa huduma kwa maveterani ambao umewekwa kisheria ukiwahakikishia askari wetu huduma bora kabisa ya tiba endapo wanaumia au kujeruhiwa wakiwa kazini” amesema Dr. Slaa.


Dr. Slaa alipata wasaa wa kuangalia baadhi ya huduma ambazo zinatolewa hospitalini hapo ikiwa ile ya viungo bandia pamoja na sehemu ya mazoezi kwa wapiganaji ambao wanapatiwa huduma za viungo hivyo. Akizungumza na baadhi ya Watanzania na wageni wengine aliofuatana nao Dr. Slaa amesema kuwa CHADEMA inaandaa sera ambayo itatumika kuandaa sheria na miundo mbinu ya kiutendaji pindi CHADEMA itakapoingia madarakani 2015 ili kuwapatia askari huduma bora kabisa ya afya pamoja na uhakika mwendelezo wa huduma hiyo hata wanapotoka jeshini.


Chini ni picha za Dr. Slaa akiwa na baadhi ya majeruhi hao akiwa ameambatana na mke wake Bi. Josephine.




 





 SOURCE:
Habari na M. M. Mwanakijiji, Picha na CHADEMA DIASPORA