Sunday 29 September 2013

Njia panda ya JK: Maslahi ya Chama au wananchi?

 

Rais Jakaya Kikwete 
Na Kelvin Matandiko, Mwananchi

Posted  Jumatano,Septemba25  2013  saa 13:53 PM
Kwa ufupi

Oktoba 10 mwaka huu umoja wa vyama vya siasa vya CUF, Chadema, NCCR Mageuzi, na vingine kadhaa visivyokuwa na wabunge wameitisha maandamano nchi nzima kuendelea kushinikiza rais asikubali kusaini muswada huo.


Kila upande miongoni mwa wanasiasa unaonzungumzia Katiba Mpya unajificha kwenye kivuli cha masilahi ya wananchi. Chama tawala, CCM, kinasema kinatetea maslahi ya wananchi na wapinzani nao wanadai kutetea maslahi hayo hayo.
Swali kuu, ni nani kati yao hasa anatetea wananchi? Mwenye majibu ni Rais Jakaya Kikwete anayetupiwa mpira wa ama kusaini au kutosaini sheria ya marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo inaaminika kuwa ama inaweza kuipatia Tanzania Katiba bora au bora Katiba.
Wakati upande wa CCM wamekwishatumia nguvu ya wingi wao kwa kupitisha sheria hiyo ndani ya Bunge, wapinzani wameanza kuunganisha makundi mbalimbali ya jamii kuikataa, huku wakisema “Katiba Mpya lazima ipatikane kwa gharama yoyote.”
Miongoni mwa makundi yaliyokutana na viongozi upinzani, ni wanahabari, viongozi wa dini, wasomi, wanaharakati na sasa wameanza kufanya mikutano ya wananchi wa kawaida.
Pamoja na kauli “katiba kupatikana kwa gharama yoyote”, viongozi hao wa upinzani waliokutana na wananchi jijini Dar es Salaam, wameweka bayana kuwa iwapo Rais Kikwete hatasikiliza hoja za umoja wao na kuachana na sheria hiyo, mapambano yataendelea kufanyika ndani na nje ya Bunge, lakini hawataingia katika Bunge Maalumu la Katiba.
Vilevile Oktoba 10, mwaka huu, umoja wa vyama vya siasa vya CUF, Chadema, NCCR Mageuzi, na vingine kadhaa visivyokuwa na wabunge wameitisha maandamano nchi nzima kuendelea kushinikiza rais asikubali kusaini muswada huo.
Viongozi hao Freeman Mbowe (Chadema), James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Profesa Lipumba(CUF), na akina Fahmi Dovutwa (UPDP), Emmanuel Makaidi (NLD) na Said Miraji (ADC) wanasema hawatarudi nyuma katika suala hili kwa kuwa lina maslahi ya wananchi.
Mbowe anaweka msisitizo: “Kosa kubwa katika kudai haki ni woga. Hatutapata Katiba Mpya kama tutaendelea kuwa taifa la watu wenye hofu. Hatutakubali kurudi nyuma katika mchakato huu na endapo rais atasaini muswada huu, tutajitoa kabisa katika harakati za kuandaa Katiba na badala yake tutaendelea kupiga kelele mpaka dunia yote itambue tunataka Katiba Mpya yenye tija kwa Watanzania.
Kwa vyovyote vile, mtu pekee wa kutegua kitendawili hiki ni Rais Kikwete, ambaye tayari viongozi wa CCM na Serikali yake wamekuwa wakimwomba asaini sheria hiyo na pengine kumtisha kuwa iwapo atasaini sheria hiyo machafuko yatazuka bungeni.
Marekebisho ya sheria hiyo yanaelezwa kuwa yamepitishwa bila kuwashirikisha Wazanzibari, wakati kwa ushirika wao wana haki sawa na Tanganyika ndani ya Muungano.
Inaelezwa pia kuwa marekebisho hayo yameweka wajumbe wa Zanzibar katika Bunge Maalumu la Katiba kuwa asilimia 36 ya wahumbe wote wakati nchi hiyo licha ya odogo wake kijiografia, ina haki sawa na Tanganyika. Usawa huo unaonyeshwa tu kwenye idadi ya wajumbe wa Tume ya Marekebisho ya Katiba ambayo inaundwa na wajumbe 15 kutoka kila nchi.
Pamoja na hoja ya kupinga Rais kuteua wajumbe 166 wasiokuwa wabunge, muswada huo unadaiwa kuwa, kinyume na katiba ya sasa, umeruhusu iwapo theluthi mbili za kila upande hazikupatikana kwa mara mbili katika Bunge Maalumu la Katiba, kwa mara ya tatu itakuwa kwa uwingi wa kawaida (‘simple majority’)  ya kila upande.

Sheria yenye vipengele hivyo ilipishwa na wabunge wa CCM baada ya wale wa upinzani kutoka nje ya Bunge kupinga kuwa sehemu ya uamuzi hayo na tangu kuanza kwa mvutano huo Rais Kikwete yuko kimya, bila shaka akitafakari ni njia ipi yenye unafuu aweze kupenya ili abaki na heshima yake na usalama ndani na nje ya chama chake.
Kwa upande wa CCM na Serikali yake, pia shinikizo si haba. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano, Uratibu wa Sera, Stephen Wasira yeye anakipinga hoja zote za kumshinikiza asisaini mswada huo. Anasema endapo Rais hatakubali kusaini mswada huo, taifa litaingia kwenye mgogoro wa kikatiba.
Naye Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe anaongeza kuwa mswada huo ulipitishwa kwa haki na demokrasia ya kuhesabu kura ya wabunge, hivyo Rais anapaswa kuusaini.
Mitego aliyovuka JK
Huu si mtego wa kwanza  kwa Rais Kikwete tangu kuanza kwa mchakato wa Katiba Mpya.
Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kukuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Azaveli Lwaitama anasema hatua ya Watanzania kutaka Katiba Mpya ilipingwa na viongozi wengi wa CCM,  lakini Rais Kikwete akafikia uamuzi wa kukubaliana na ombi hilo.
Mbali na hatua hiyo, Dk Lwaitama anasema Rais Kikwete aliamua pia kutofautiana na chama chake baada ya kuagiza mjadala wa sheria ya mabadiliko ya Katiba urudishwe bungeni kwa mara ya pili ili kuleta maridhiano.
“Ninaamini huu pia ni mtego mwingine anaokutana nao Rais kutoka ndani ya chama chake, ninaamini kama kiongozi anayepima hoja za Katiba kwa mustakabali wa kizazi kijacho, atafanya uamuzi wa kutokusaini muswada huo,” anasema Lwaitama.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zacharia Kakobe anasema kuwa Rais Kikwete akisaini muswada huo, Watanzania watajua kuwa hana nia njema na taifa kwa kuwa wengi wanaupinga.
Hofu ya Kakobe juu ya muswada huo, anasema inatokana na mamlaka ya Rais kuteua wajumbe nje ya majina yaliyopendekezwa. “Sina hakika kama CCM ina dini ya kutuwakilisha hata sisi, ni hatari sana kuiteka Katiba ya Watanzania, ninamwomba Rais usikubali mtego huo,” anasema Kakobe.
Naye kiongozi wa maimamu nchini, Sheikh Rajab Katimba anasema Katiba Mpya ni kwa ajili ya Watanzania na siyo chama, dini au kundi lolote.
 “CCM ilikataa Katiba isianzishwe, Jakaya Kikwete pekee alijipiga kifua akakubali, ingawa alishambuliwa na chama chake, kwa hiyo ninaomba kwa msimamo aliotumia awali, asisaini muswada huo,” anasema Shekh Katimba.

SOURCE: MWANANCHI