Monday 30 September 2013

EAC ziunganishe nguvu kutokomeza ugaidi


29th September 2013
Maoni ya Katuni
Inaweza ikadhaniwa kuwa vitendo vya kigaidi vilivyofanyika maeneo ya kibiashara ya Westgate jijini Nairobi huko Kenya kuanzia wiki iliyopita, vinawahusu wananchi wa Nairobi na vitongoji vyake tu.
Ukweli ni kwamba mauaji yaliyotokea katika eneo la kituo cha biashara cha Westgate chenye mtandao wa biashara kimataifa, yaliwagusa hata raia wa nchi mbalimbali akiwamo mmoja aliyefahamika kwa jina la Vedasrus Nsanzungwanko wa kutoka Tanzania, ambaye taarifa zilisema alijeruhiwa kwa risasi mguuni.

Shambulizi la Westgate, pamoja na ukweli kwamba kikundi cha al Shabaab, chenye uhusiano wa karibu na al Qaeda kinadai kuhusika, bado mtandao wa maharamia hao haujajulikana kama umelenga kufanya nini baada ya shambulizi la Westgate.

Bado akilini mwa wengi hayajasahaulika mashambulizi yaliyowahi kufanywa kwa wakati mmoja na kikundi cha al Queda katika majengo ya balozi za Marekani jijini Dar es Salaam na Nairobi tarehe 17 Agosti 1998 ambapo yalisababisha hasara ya vitu pamoja na mauaji ya raia zaidi ya 200.

Waasi hao wa Kiislamu, walitamka wazi kuwa shambulizi hilo, lilikuwa ni la kulipiza kisasi kwa hatua ya Kenya ya kupeleka vikosi vyake nchini Somalia mwaka 2011 kwa ajili ya kupambana nao. Msemaji wao pia alisisitiza kupitia televisheni kuwa watu kutoka Magharibi hawatakuwa salama nchini Kenya hadi hapo nchi hiyo itakapoyatoa majeshi yake nchini Somalia.

Msemaji wa al Qaeda aliendelea kutishia kupitia mtandao wao mpya wa Twitter kuwa “Wakenya wana damu viganjani mwao. Yeyote aliye tayari kuja Kenya anapaswa kujiandaa kukabiliana na hali halisi".

Akasema tena 'Hatuogopi watu kutoka Ulaya na Marekani kwa sababu sisi si dhaifu, na tunawaambia hao wazungu kwamba yeyote ambaye amekuwa akisaidia waliokuwa wakitushambulia, waambieni Wakenya kuacha mashambulizi yao kama wanataka kubaki salama."

Tukio hilo la ugaidi, ambalo, limefanyika nyakati za mchana kukiwa kweupe katika viunga vya jumba la kibiashara la Westgate huko Nairobi, kwa mara nyingine ni kama limeziweka nchi za Afrika Mashariki kuwa tishio kubwa kwa mashambulizi zaidi.

Kutokana na uzoefu wa mashambulizi ya aina hiyo, Nairobi pamoja na miji mingine mikubwa ya Afrika Mashariki yanaweza kuwa yamelengwa kuhujumiwa kwa nyakati tofauti. Wao al Qaeda wanafahamu kuwa shambulio hili limezigusa nchi wanachama wa Afrika Mashariki na kwamba hawawezi kubakia kimya.

Inafahamika wazi kuwa karibia watu 70 walipoteza maisha wakati wengine zaidi ya 250 wakijeruhiwa katika shambulio hilo baya zaidi ambalo halijawahi kutokea miaka ya hivi karibuni.
Tunaamini kuwa hujuma za aina hizo, ambazo mara nyingi huwakuta makundi yasiyojihami kama watoto, akina mama na wengine wasiojiweza, zinaweza kuelekezwa kwa makundi ya aina hiyo ambako magaidi wanajua hawatapambana na upinzani mkubwa.

Vitendo vya ugaidi tayari vimeshazigusa nchi za Afrika Mashariki, ambapo mwaka 2010 wananchi zaidi ya 70 pia walipoteza maisha jijini Kampala kutokana na mauaji ya kujilipua mabomu yaliyotokea wakati wanaangalia mashindano ya dunia ya mpira wa miguu.

Hakuna anayeweza kujua kama magaidi hao sasa wanalenga kufanya mashambulizi eneo gani, na kwa vile al Shabaab tayari wametoa onyo la kuendelea na mauaji, ni wajibu wa nchi za Afrika Mashariki kuunda mtandao wa kudhibiti ugaidi usitokee tena.

Tunaamini kuwa nchi zote sasa zinachukua tahadhari za kuimarisha usalama, tunatoa wito kwa wananchi wote kutoa taarifa za mienendo ya watu wanaoweza kutiliwa mashaka kwa mamlaka husika, kila mwananchi na awe mwanausalama, tukishikamana pamoja tutatokomeza ugaidi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.


CHANZO: NIPASHE JUMAPILI