Monday 8 July 2013

Hatima makada wa Chadema walioko Tabora kujulikana leo

             

Kilewo aliwekwa chini ya ulinzi wa polisi, Juni 21, mwaka huu, baada ya kuitwa makao makuu ya jeshi hilo na kuhojiwa kuhusiana na tuhuma hizo, kisha alisafirishwa hadi Igunga ambako aliunganishwa na wenzake waliokuwa wakikabiliwa na kesi hiyo.  

Na James Magai, Mwananchi   (email the author)

Posted  Jumatatu,Julai8  2013  saa 9:23 AM
Kwa ufupi
 
Ni wale wanaodaiwa  kumteka kwa nia ya ugaidi Musa Tesha huko Igunga Tabora.


Dar es Salaam. Hatima ya makada watano wa Chadema, wanaokabiliwa na kesi ya ugaidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora, inatarajiwa kujulikana leo, wakati mahakama hiyo itakapotoa uamuzi kuhusiana na kesi hiyopamoja na mambo mengine, uhalali wa mashtaka yanayowakabili.
Makada hao wa Chadema, Henry John Kilewo, ambaye ni Katibu wa Chadema Wilaya ya Kinondoni,  Evodius Justinian, Oscar Kaijage,  Rajabu Daniel, Seif Magesa Kabuta, walipandishwa kizimbani mahakamani hapo na kusomewa mashtaka mawili, moja la ugaidi na lingine la jinai.
Katika shtaka la kwanza wanashtakiwa chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi, wakidaiwa kumteka kwa nia ya ugaidi Mussa Tesha huko Igunga, Tabora,  na la pili wanashtakiwa chini ya Sheria ya Kanuni za Adhabu wakidaiwa kumdhuru Tesha kwa kumwagia tindikali.
Walidaiwa kutenda makosa hayo mwaka 2011, wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga.Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mawakili wao, Peter Kibatala na Profesa Abdallah Safari walipambana kuwanusuru na mashtaka hayo.
Mawakili hao walihoji uhalali wa mashtaka hayo,wakidai kuwa hakuna vigezo vya kutosha kuonyesha kuwa kuna ugaidi, huku pia wakihoji utaratibu wa kuwafungulia mashtaka katika mahakama hiyo badala ya kule walikokamatiwa.
Hivyo waliiomba Mahakama hiyo ama iwafutie mashtaka hayo au iamuru kila mshtakiwa arudishwe na kushtakiwa katika mahakama za mahali walikokamatiwa.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Juma Masanja akisaidiana na Wakili wa Serikali, Idelfonce Mukandara, walidai mashtaka hayo ni halali.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Joctan Rushwera aliahirisha kesi hiyo na kupanga kutoa uamuzi leo.
Hakimu Rushwera aliamuru washtakiwa wote wapelekwe mahabusu wakisubiri uamuzi wa kesi yao leo, kwa kuwa mashtaka yanayowakabili hayana dhamana.