 
  
            
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare akiwa 
amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam, jana, 
kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya Shingo. 
            
Kwa ufupi
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwenye wodi 
ya uchunguzi ya Sewahaji, Lwakatare alisema kuwa anakabiliwa na matatizo
 ya pingili za shingo na jopo la madaktari linakutana leo kuamua kama 
afanyiwe upasuaji ama la.
Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama 
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare 
amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na matatizo ya 
shingo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwenye 
wodi ya uchunguzi ya Sewahaji, Lwakatare alisema kuwa anakabiliwa na 
matatizo ya pingili za shingo na jopo la madaktari linakutana leo kuamua
 kama afanyiwe upasuaji ama la.
“Nilifanyiwa uchunguzi kwa x-ray na madaktari 
walisema hakuna jinsi zaidi ya upasuaji na kesho (leo) jopo la madaktari
 linasoma picha za x-ray kuamua aina ya upasuaji...nimegundulika 
kuharibika pingili ya sita na saba.
“Nilipata ajali mwaka 2008 na nilipona, lakini 
nilipatwa na kadhia hii baada ya kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi baada
 ya kukamatwa na zaidi ni kutokana na kulala chini,” alisema Lwakatare 
akiwa kitandani.
Alisema kuwa aliwahi kuumwa akiwa Gereza la Segerea alikokuwa anashikiliwa kabla ya kuachiwa kwa dhamana na kwamba alihudumiwa.
Alisema tatizo hilo lilijirudia jana asubuhi 
ambapo alifikishwa hospitali hiyo na kupatiwa kitanda kabla ya kufanyiwa
 vipimo vya X-ray na kukutwa tatizo hilo ambalo alisema gharama yake ni 
Sh3.5 milioni.
