Amina Juma 
            
Kwa ufupi
Habari zilizothibitishwa na baadhi ya 
waombolezaji waliokuwa nyumbani kwa marehemu Visiga, Kibaha zinasema 
baadhi ya wanandugu walimkana Amina siku chache baada ya kutangazwa vifo
 hivyo.
Kibaha/Tanga. Hata kabla ya 
maziko askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waliouawa Darfur,
 Sudan hayajafanyika, mchumba wa mmoja wa wapiganaji hao, Amina Juma 
ameonja chungu nyingine baada ya kutimuliwa kwenye nyumba aliyokuwa 
akiishi na marehemu mwenza wake.
Amina ambaye inadaiwa kuwa alikuwa akiishi na 
Fortunatus Msofe aliyekuwa askari katika Kambi ya Msangani, 36KJ Pwani 
alisema jana: “Kumekuwa na mzozo wa hali ya juu na ndiyo maana 
tumeshindwa hata kufika Uwanja wa Ndege kuupokea mwili na hata kesho 
(leo) sidhani kama nitakwenda... kuna mtafaruku mkubwa wa kifamilia.”
Baada ya kutimuliwa, Amina ambaye hawakuwahi 
kupata mtoto na marehemu Msofe, alilazimika kuondoka kwenye nyumba hiyo 
na kwenda Mlandizi kwa wazazi wake.
“Nimeishi na Msofe kwa miaka mitatu, akiwa kambini
 mimi niko hapa na wakati mwingine alikuwa analala huku... lakini leo 
wamenitimua,” alisema huku akilia.
Habari zilizothibitishwa na baadhi ya waombolezaji
 waliokuwa nyumbani kwa marehemu Visiga, Kibaha zinasema baadhi ya 
wanandugu walimkana Amina siku chache baada ya kutangazwa vifo hivyo.
Ilidaiwa kwamba Amina alitimuliwa katika nyumba 
hiyo Ijumaa iliyopita, saa saba mchana baada ya ndugu watatu wa marehemu
 kufika hapo wakitokea Tanga.
Walipofika inadaiwa kuwa walitangaza kusitishwa msiba huo katika nyumba hiyo na kutangaza kutomtambua mke huyo.
Watu hao waliwaeleza waombolezaji kuwa walitumwa 
na baba mzazi wa marehemu, Willbad Msofe kutoka Kange, Tanga kufika 
Kibaha kusitisha msiba uliokuwa ukiendelea nyumbani kwa mtoto wake huyo.
Inadaiwa pia kuwa katika msafara huo,  alikuwapo mdogo wa marehemu ambaye aliwahi kuishi kwa miaka miwili na Amina hapo Visiga.
Ilidaiwa kuwa walipofika nyumbani hapo walionana 
na mfiwa, Amina na wazazi wake ambao pamoja na majirani na watu wengine 
wengi, walikuwa wakimfariji binti yao huyo.
Mmoja wa waombolezaji alisema baada ya salamu 
wanandugu hao walianza kuulizia mali za marehemu na walikuwa wakimuuliza
 Amina ambaye aliwaleza kila kitu kilipo na baada ya hapo ndipo 
walipomweleza kuwa wametumwa na baba wa marehemu kuwa watu hawatakiwi 
kuomboleza kwenye eneo hilo kwani msiba upo Tanga tu ambako ndiko iliko 
familia yake.
Alipoulizwa baba wa marehemu, Mzee Msofe alisema: 
“Mimi ndiye niliyeagiza nyumba ifungwe na ukweli ninamfahamu Amina, 
lakini simtambui kama mkewe kwa kuwa hawajafunga ndoa... Hata wewe si 
unayafahamu haya? Uchumba si ndoa na ukifunga ndoa ndipo unatambulika 
rasmi,” alisema.
Akiwa kwa wazazi wake Mlandizi jana, Amina alisema:
“Namwachia Mungu maana hayo yote nashangaa 
yanatokea wakati huu mume wangu ‘Fortu’ amekufa, mbona kipindi chote cha
 miaka mitatu iliyopita familia ya Tanga dada zake na mdogo wake 
tuliishi nao vizuri kwangu nilipokuwa na marehemu? Nimeishi na ndugu 
wote lakini hawakuwahi kuhoji, hata nilipokwenda na mume wangu Kange 
baba na mama Msofe nilikaa nao zaidi ya wiki na hawakunikana, ila 
nashangaa,” alisema na kulia kwa uchungu.
Akizungumzia kitendo hicho, baba yake Amina, Juma 
Juma alisema: “Nimeshangaa hizi taarifa. Tulikuwa tunajiandaa kupokea 
msiba wa mwanetu, lakini leo yanakuja mengine kwa kweli imetushangaza 
sana.”
“Nasubiri baada ya kumzika marehemu, nitazungumza 
nao... Kinachonishangaza ni kwamba walituandikia barua ya kumposa binti 
yangu na tukawajibu na gharama zilikuwa Sh1.2 milioni... Tutazungumza, 
ngoja hili lipite kwanza,” alisema mzee Juma.
Maisha ya Amina na ‘Fortu’
Akisimulia maisha yao, Amina alisema: “Tulianza 
kuishi Mbezi Luis mwaka 2010 katika nyumba ya kupanga na nikamshawishi 
tununue kiwanja na kwa kuwa mimi ni mwenyeji wa Kibaha, niliwatumia 
marafiki wa familia yangu Mlandizi wakatafutia eneo na mwaka 2011 
tulipata na tukaanza ujenzi.
“Tukiwa Mbezi, tulianza kufyatua matofali kisha 
ujenzi ukaanza Visiga mwaka 2012 mwanzoni na  Septemba mwaka huo 
tulihamia kwenye nyumba yetu na hapo ndiyo ilikuwa makazi yetu hadi 
marehemu anaondoka kwenda Darfur.
“Wakati wote huo ‘Fortu’ alikuwa keshaniposa na 
hata barua zote za posa zipo na tulikuwa tukisubiri utaratibu wa kijeshi
 marehemu kukamilisha miaka sita ya kukaa kambini kisheria ndipo 
aruhusiwe kuoa.
“Fortu alikamilisha miaka hiyo mwaka 2012 mwishoni
 na wakati akijiandaa kwa kufunga ndoa ndipo ikatokea safari ya Darfur 
mwanzoni mwa mwaka huu na tukakubaliana tusitishe kwanza akirudi 
tukamilishe, lakini haikuwa.... Halafu wananifukuza wanasema hawanijui,”
 alieleza huku akiangua kilio.
Nyongeza na Burhani Yakubu
Update, tarehe 23.07.2013
Mwananchi inaripoti
 
                    Update, tarehe 23.07.2013
Mwananchi inaripoti
Kibaha. Mchumba wa marehemu, Fortunatus Msofe, 
ambaye ni mmoja wa wapiganaji wa JWTZ, waliofia Darfur, ameondoka kwenda
 Tanga kumzika mwenza wake huyo.
Mwanamke huyo Amina Juma, amekataliwa na ndugui wa
 marehemu ambao wameifunga kwa kufuli nyumba inayodaiwa kuwa amejenga 
marehemu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Amina alisema 
ingawa awali alikata tamaa ya kumzika mwenzake, lakini jana aliamua 
kwenda Tanga kuhudhuria mazishi na kwamba hatua hiyo ilikuja baada ya 
kujishauri sana.
Baba wa marehemu, Wilbad Msofe aliiambia gazeti 
hili kutoka Kange, Tanga kuwa alishangazwa na hatua ya Amina 
kutowafahamisha kuhusu msiba huo.
Alisema hiyo ndiyo sababu za yeye kuamua kutaka mwanawe apelekwe Kange kwa mazishi.
Akizungumza na Mwananchi akiwa njiani kwenda 
Kange, Amina alisema: “Nilikuwa ninataka sana kumzika mwenzangu lakini 
ile hali ilikuwa imenichanganya pamoja na kwamba nilishauriwa, sasa 
nimekata shauri nakwenda Tanga.
“Najua kuna kitu hapa, lakini ‘Fortu’ kwa kuwa 
nilikuwa naye, na wana ndugu wa upande wa wake wameshanikana, mimi 
nitamzika tu mwenzangu na kurudi,” alisisitiza.
Miili ya wapiganaji hao iliagwa jana katika Makao 
Makuu ya Jeshi, yaliyoko Upanga na Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni 
Amiri Jeshi Mkuu, Mkuu wa Majeshi, Davis Mwamunyange, makamanda na 
wanajeshi walishiriki kuwaaga wanajeshi hao.
Akizungumza kwa masikitiko na huku sauti ikiwa 
imemkauka kutokana na kulia muda mrefu, Amina alisema: “Siwazii 
mtafaruku uliopo, moyo umenituma kwenda kumzika mume wangu, niliwaza 
usiku kucha na leo (jana) Jumatatu asubuhi nikaamua kwenda Tanga.”
“Msofe amekufa tulikuwa tuna mipango mingi, 
tulipanga harusi kubwa lakini haikuwahi kufanyika, niliongea naye 
alfajiri ya Jumamosi ya Julai 13, akaniambia tutaongea baadaye maana 
wanakwenda kwenye operesheni...
“Unajua tuliishi maisha ya kipekee sana 
tulipendana kiukweli hata majirani tuliokuwa tukiishi nao Mbezi na 
Visiga wanajua hilo na wengi walikuwa wakinisihi sana nisije kumuudhi 
huyu kijana.
Baadaye akiwa Tanga alisema: “Nafsi yangu inaniuma
 sana, yaani kila muda na saa zinavyozidi kwenda. Alisema hatua ya wakwe
 zangu kudai kutonitambua si ya kiungwana.
“Jana (juzi) usiku nikiwa nimejipumzisha nilihisi marehemu ananiambia niyashinde majaribu,” alisema Amina na kuangua kilio.
Akizungumzia kuhusu kufungwa kwa nyumba yao ya 
Visiga, alisema anamuachia Mungu, kwa sasa yeye haangalii mali na kwamba
 akili yake ikafikiria msiba uliopo.
Source: Mwananchi news paper
Source: Mwananchi news paper
 
  