Rais Uhuru Kenyatta (kulia) akiwa na Naibu Rais William Ruto baada ya kuwasili kutoka London, Uingereza Mei 9, 2013. Picha/PPS
Na BENSON MATHEKA Na JUMA NAMLOLA
Imepakiwa - Monday, July 15
2013 at
09:24
Kwa Mukhtasari
Uhusiano
wa Kenya na mataifa ya kigeni umewekwa katika darubini baada ya siku
100 za utawala wa Muungano wa Jubilee. Kipindi hicho, kumekuwepo mzozo
kuhusu raia wa Nigeria Anthony Chinedu, Rais wa Amerika Barack Obama
alikosa kuzuru na kesi za ICC bado zipo.
UHUSIANO wa Serikali na mataifa ya
kigeni umewekwa katika darubini baada ya siku 100 za utawala wa Muungano
wa Jubilee, hasa kufuatia kesi zinazowakabili Rais Uhuru Kenyatta na
Naibu wake William Ruto katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu,
ICC.
Hivi majuzi,
serikali ilipuuza hatua ya Rais Barack Obama wa Amerika ya kutozuru
Kenya kwa sababu viongozi wake wanakabiliwa na kesi katika ICC
alipotembelea mataifa matatu barani Afrika.
Naibu Rais William Ruto alisema kwamba hatua ya Rais Obama haikukosesha serikali usingizi kwa sababu Kenya ina marafiki wengi.
Kwenya hotuba
yake ya kwanza kwa taifa baada ya kuapishwa, Rais Kenyatta alisema
Kenya inathamini na kutegemea uhusiano wake na mataifa jirani ya Afrika
Mashariki na bara la Afrika kwa jumla.
“Serikali yangu imejitolea kufanikisha biashara na ushirikiano na mataifa ya eneo hili,” alisema Rais Kenyatta.
Alikiri
kwamba Kenya itaendelea kushirikiana na mataifa ya Afrika chini ya
Muungano wa Afrika kwa kuungana ili kupata suluhu la matatizo
yanayoikuba bara hili.
Siku chache
baada ya kuapishwa, alimtuma Naibu wake William Ruto kutembelea mataifa
kadha barani katika kile kilichotajwa kama njia ya kutafuta kuungwa
mkono dhidi ya kesi za ICC.
Kwenye hotuba
yake alisema anaamini kwamba mataifa yote ya ulimwengu yanategemeana na
kuahidi kukuza uhusiano na washirika wa kibiashara wa Kenya.
Alisema Kenya itaheshimu mikataba ya kimataifa mradi tu iliwekwa kwa misingi ya heshima.
Majuzi
uhusiano wa Kenya na ya mataifa kigeni uliwekwa kwenye mizani baada ya
kuwatimua raia wa kigeni walioshukiwa kuhusika na ulanguzi wa dawa za
kulevya maafisa pale ndege ya Kenya na maafisa walipozuiwa Nigeria kwa
majuma mawili.
Serikali
ilikanusha kwamba uhusiano wake na serikali ya Nigeria haukuathiriwa na
tukio hilo huku ikilaumiwa kwa kukiuka kanuni za kimataifa ilipomtimua
mfanyabiashara Antony Chinedu.
Baadhi ya Wakenya wanahisi kwamba Kenya inapasa kuimarisha sera za uhusiano wake na mataifa ya kigeni ili kuvutia wawekezaji.
Wanasema
huenda uchumi wa Kenya ukaathirika kwa sababu nchi za ulaya na Amerika
zinajivuta kushirikiana na Kenya kutokana na kesi zinazowakabili
viongozi katika ICC.
Kesi dhidi ya Bw Ruto imepangiwa kuanza Septemba 10 huku inayomkabili Rais Kenya ikitarajiwa kuanza Novemba mwaka huu.
Akihutubia
wahariri na wanahabari katika ikulu ya Nairobi Ijumaa, Rais Kenyatta
alisema Kenya iko tayari kushirikiana na taifa lolote linaloheshimu
serikali kote ulimwenguni. Alisema kwa sasa uhusiano wa Kenya na mataifa
yote ulimwenguni ni mzuri.
“Sijasikia
ubalozi wa Kenya uliofungwa au nchi iliyofunga ubalozi wake nchini. Kwa
hivyo ninaamini uhusiano wetu na mataifa ya kigeni ni mzuri,” akasema.
Lakini inasubiriwa kuona hatua atakazochukua siku zijazo baada ya
kuteua mabalozi.
Mashirika ya
jamii kupitia Jukwa la Katiba, sasa yanaitaka serikali ikomeshe mtindo
wa kutochukua hatua nchi inapotishwa na mataifa mengine ya Afrika.
Dharau
Rais wa
mashirika hayo Bw Morris Odhiambo, alisema sera hii ya kunyamaza wakati
raia wa kenya wanapohangaishwa unaifanya Kenya itazamwe kwa jicho la
dharau nje ya mipaka yake.
“Katika kisa
kama cha Chinedu, rais alipaswa kuchukua hatua kali na kuhakikisha
anaikemea Nigeria. Lakini badala yake, serikali ilinyamaza na kuacha
Wakenya kuwa mateka mikononi mwa mshukiwa huyo wa dawa za kulenya kwa
wiki kadha. Huo ni uoga,” akasema.
Bw Odhiambo
alisema ingawa Kenya inajifanya kuendeleza ushirikiano na mataifa
mengine ya Afrika, haipaswi kuvumulia uchokozi wa aina yoyote. Alitoa
mfano wa serikali ya Uganda kuendelea kukalia kisiwa cha Migingo na hata
maafisa wake kuwapiga maafisa wa usalama wa Kenya waliotumwa kulinda
mpaka wa kisiwa hicho.
“Hata wananchi wetu wanaposhambuliwa, hatusemi kitu. Lazima tuache uoga huu kama tunataka kuendelea mbele,” akasema.
Majuzi
maafisa wa polisi wa Utawala wa Kenya walipigwa na kuumizwa na wenzao wa
Uganda katika kisiwa cha Migingo baada ya ugomvi kuzuka kati yao.
“Huko nje
tunadharauliwa sana. Rais na naibu wake wanapaswa kuwa na sera
zitakazotupatia heshima. Wasidhani kuwa wanaangaliwa kwa njia nzuri eti
kwa vile wao ni vijana,” akasema Bw Odhiambo.
Rais Kenyatta amesisitiza kuwa Kenya itashirikiana na mataifa ya Afrika zaidi kuliko mengine.
Source : Swahili hub