 
  
            
Alex Massawe 
            
Kwa ufupi
Mkuu wa la Shirika la Polisi la Kimataifa 
(Interpol), Tawi la Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav 
Babile aliliambia gazeti hili jana kwamba Massawe alikamatwa kati ya 
Juni 20 na 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai 
akitokea Afrika Kusini.
Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu nchini, 
Alex Massawe ambaye alikuwa anatafutwa na Polisi wa Tanzania kwa muda 
mrefu, amekatwa Dubai, Falme za Kiarabu (UAE).
Mkuu wa la Shirika la Polisi la Kimataifa 
(Interpol), Tawi la Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav 
Babile aliliambia gazeti hili jana kwamba Massawe alikamatwa kati ya 
Juni 20 na 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai 
akitokea Afrika Kusini.
Babile alisema hivi sasa walikuwa wanaandaa taratibu za kumrudisha nchini ambako amekuwa akisakwa kwa muda mrefu.
“Ombi la kuleta mhalifu nchini kutoka nje ya nchi (extradition request),
 lina hatua ndefu. Unajua kuna mlolongo wa taratibu za kutekeleza ili 
Massawe aletwe. Kwanza lazima Polisi wa Tanzania watoe tangazo kwa 
Interpol kuhusu kumsaka mtu huyo ili aletwe,” alisema Babile.
Alisema Massawe alikamatwa wakati akifanya taratibu za ukaguzi baada ya kuwasili UAE.
Habari zilizofikia gazeti hili mapema kutoka Dubai
 zilieleza kuwa Massawe alikamatwa na maofisa wa usalama wa UAE kutokana
 na alama zake za vidole na kuonyesha kuwa alikuwamo kwenye orodha ya 
watu waliokuwa wanasakwa na Interpol.
Massawe ambaye anamiliki majumba na biashara ya 
utalii katika Miji ya Arusha, Dar es Salaam na Moshi, inadaiwa kwamba 
alikutwa na pasi tatu bandia za kusafiria zilizokuwa na majina tofauti 
wakati alama zake za vidole zilionyesha anaitwa Alex Massawe.
“Maofisa wa Usalama wa uwanja wa ndege walimuuliza
 kuwa wewe ndiye Alex Massawe? Alikana lakini alielezwa kuwa alama za 
vidole vinaonyesha anaitwa hivyo,” kilidokeza chanzo cha habari hizi kwa
 simu kutoka Dubai. Hata hivyo, Babile alisema hakuwa na taarifa za 
Massawe kukutwa na pasi bandia za kusafiria.
Uvumi wa Aprili
Mapema Aprili 27, mwaka huu kulikuwa na habari 
kwamba Massawe amekamatwa katika mji mmojawapo ulioko katika Pwani ya 
Afrika Kusini.
Habari hizo za kukamatwa kwa Massawe, ambaye pia 
hufadhili masuala ya kisiasa na michezo, zilisambaa kupitia mitandao 
mbalimbali ya kijamii ya Facebook, Twitter na Jamii Forum. Kulikuwa kuna
 mkanganyiko wa taarifa huku wengine wakidai alinaswa akiwa ndani ya 
boti huko Afrika Kusini, wengine wakidai alikamatwa wakati akijaribu 
kuingia Msumbiji akitokea Malawi.
Akizungumzia hilo Babile alisema huo ulikuwa ni 
uzushi na baada ya kuzisikia taarifa hizo walifuatilia katika maeneo 
aliyohusishwa kukamatwa na kubaini kwamba hapakuwa na ukweli wowote.
Kwa nini Massawe anatafutwa
Aprili 4 mwaka huu, mfanyabiashara huyo alitajwa 
mahakamani katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Onesphory Kituly 
ambaye aliuawa katika mazingira ya kutatanisha Novemba 6, 2011 akiwa 
nyumbani kwake Magomeni, Dar es Salaam.
Katika kesi hiyo ambayo mshtakiwa wa kwanza ni 
mfanyabiashara maarufu, Abubakar Marijani ‘Papaa Msofe’ na mshtakiwa 
mwingine, Makongoro Joseph Nyerere alitoa malalamiko mbele ya Hakimu 
Mkazi, Agnes Mchome baada ya Wakili wa Serikali, Mwanaisha Kombo kudai 
upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe mpya ya 
kuitaja. Mshtakiwa huyo, aliomba jalada la kesi yao lipelekwe mahakamani
 hapo kwa ajili ya kulifanyia kazi na kutuhumu kuwa ndugu wa marehemu 
Kituly hawataki maendeleo ya kesi yao hadi Massawe akamatwe.
chanzo : Mwananchi.co.tz
chanzo : Mwananchi.co.tz
