Kwa ufupi
Arusha. Wakati vumbi la matukio ya kigaidi ya
milipuko ya bomu kanisani na kwenye mkutano wa kampeni za Chadema
halijatulia, tukio lingine linalohusishwa na ugaidi limetokea wilayani
Arumeru kwa Sheikh wa wilaya hiyo, Said Juma Makamba aliyejeruhiwa kwa
kumwagiwa usoni kimiminika kinachoaminika kuwa tindikali.
Sheikh Makamba anayekaimu nafasi hiyo alikutwa na
hayo kati ya Saa 4:00 hadi 5:00 usiku wa kuamkia juzi akitoka kusali
Tarawei na alilazwa wodi namba nne katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya
Mount Meru kwa matibabu.
Jicho la kushoto la Sheikh huyo limeathirika, huku akiwa amebabuka na kuvimba usoni, kifuani, mkono wa kushoto na mgongoni.
Akizungumza kwa taabu kitandani kwake alikolazwa, Sheikh Makamba ambaye pia
ni Imamu wa Msikiti wa Sekei wilayani Arumeru alisema alimwagiwa
tindikali muda mfupi baada ya kurejea nyumbani kwake akitoka kuswali.
“Nilipotoka Msikitini, nilisindikizwa hadi
nyumbani na vijana wawili nilioongozana nao kutoka msikitini ambao
walihakikisha nimeingia ndani salama. Lakini kabla ya kulala nilitoka
nje kwa ajili ya kujisaidia kwenye choo cha nje ndipo nilimwona mtu
amesimama pembeni ya nyumba nikiwa najitahidi kumwangalia ili nimtambue,
ghafla alinimwagia kitu cha majimaji usoni,” alisema Sheikh Makamba.
Ingawa hataki kuingia kwa undani kuhusu
anaowatuhumu na sababu za kumwagiwa tindikali, Sheikh Makamba alisema
anadhani jambo hilo linatoakana na ugomvi wa madaraka msikitini hapo.
Katibu wa Bakwata Wilaya ya Arumeru, Sheikh Yahaya
Husein Mwangela aliwaomba polisi kuchunguza tukio hilo ili kuondoa hofu
miongoni mwa viongozi wa Bakwata.
Hili ni tukio la pili kwa viongozi wa Bakwata
Arusha kumwagiwa tindikali baada ya Oktoba mwaka jana, Katibu wa Baraza
hilo Mkoa wa Arusha, Abdukarim Njonjo kulipuliwa na kitu kinachosadikiwa
kuwa ni bomu. Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa hadi juzi kulikuwa
hakuna mtu aliyekamatwa.
ri imeanza upelelezi na uchunguzi wa kina wa tukio hilo kubaini wahusika.
Hadi jana jioni, hakuna mtu aliyekuwa akishikiliwa polisi kwa mahojiano kuhusu tukio hilo.