Posted Jumatano,Julai24 2013 saa 7:55 AM
Kwa ufupi
Mnyika asema mjadala wa Katiba ya Tanganyika unapaswa kuanza sasa sambamba na huu wa Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Butiku asema hakuna cha kuogopa kwani Zanzibar imeshaonyesha njia
Dar es Salaam/Moshi. Chadema
kimepinga kauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba kuhusu hatima ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kikisema mchakato
wa sasa wa Mabaraza ya Katiba, usiwe kikwazo cha mjadala wa muundo wa
Serikali Tatu.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, John
Mnyika alisema Dar es Salaam jana kuwa hatima ya Uchaguzi Mkuu wa 2015
utakaotokana na mchakato wa mabadiliko ya Katiba unaoendelea, siyo suala
la kusubiri.
Akizungumza na mwandishi wetu juzi kuhusu kauli ya
Waziri wa Katiba na Sheria Mathias Chikawe kwamba endapo mapendekezo ya
Serikali Tatu yatapitishwa, kuna hatihati ya Uchaguzi Mkuu wa 2015
kufanyika, Jaji Warioba alisema: “Tuachieni muda… hayo mengine ni hisia
tu. Ni kweli tunayajua lakini acheni tumalize hili kwanza ( la Mabaraza
ya Katiba). Hii ndiyo hatua tuliyopo sasa.”
Lakini jana Mnyika alisema: “Hatuwezi kusubiri
hadi Mabaraza ya Katiba yakamilishe mchakato kama alivyoeleza Jaji
Warioba katika gazeti lenu la Mwananchi toleo la leo, (jana),” alisema
Mnyika kwa simu.
Jaji Warioba alitaka suala la muundo wa Serikali
Tatu utakavyokuwa lisiwe hoja kwa sasa kwa kuwa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba inachokifanya ni kukusanya maoni kupitia Mabaraza ya Katiba na
kisha kuandaa rasimu itakayopelekwa bungeni kwa ajili ya majadiliano na
kwamba mjadala huo utawachanganya wananchi endapo utaingizwa katika
hatua hii ya ukusanyaji maoni.
Lakini Mnyika alisema: “Mijadala hii haiwezi
kusubiri mpaka hatua ya Mabaraza ya Katiba, inapaswa kuanza wakati huu
kupitia mabaraza yanayosimamiwa na Tume na Mabaraza yanayoendeshwa na
makundi ya kijamii. “Pia, masuala hayo ya mpito pamoja na marekebisho ya
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ni mambo ambayo yanapaswa kutolewa
ufafanuzi wa ziada na Serikali zaidi ya kauli ambayo Waziri wa Sheria na
Katiba Mathias Chikawe ameitoa kupitia gazeti la lenu la leo (jana).”
Alisema kimsingi bado kunahitajika mjadala wa
masuala ya mpito kwa sababu kuna uwezekano kwamba Katiba Mpya, ya
Muungano au ya Zanzibar na ya Tanganyika, isiwe tayari kabla ya Uchaguzi
Mkuu wa 2015, endapo suala la Serikali tatu litapita.
Alisema kwa upande mwingine, rasimu ya Katiba
iliyotolewa imeibua mjadala juu ya mkwamo wa kikatiba (constitutional
stalemate), ambao ni muhimu upatiwe suluhisho akisema chama chake
kinapendekeza mchakato wa Katiba Mpya ya Tanganyika uanze mara moja ili
uende sambamba na huu wa Katiba Mpya ya Muungano. Alisema ilikuwa vyema
yote yakajadiliwa katika Bunge la Agosti 27, mwaka huu.
Waziri Chikawe alikaririwa na gazeti hili juzi
akisema: “Uwepo wa Serikali tatu utafumua mfumo mzima wa utendaji ndani
ya Serikali. Hatuwezi tena kufanya uchaguzi wa Rais na wabunge 2015,
hatuwezi kufanya chochote nje ya Katiba ya Serikali Tatu kwa kuwa
kinachofuata ni kuunda Katiba nyingine inayohusiana na Serikali tatu.
Waziri Chikawe afafanua
Juzi, Waziri Chikawe alitoa ufafanuzi juu ya utata
wa hoja zake kwa kuipongeza Tume ya Jaji Warioba kwa kazi inayofanya
huku akisema anaunga mkono msimamo wa CCM wa kutaka kuendelea na muundo
wa Muungano wa Serikali mbili.
Alisema mchakato wa kuandika Katiba Mpya unapaswa kuangaliwa kwa jicho pana zaidi ya lile la Uchaguzi Mkuu wa 2015.
“Kuna mambo mawili hapa. Mosi ni msimamo wa chama changu cha
Mapinduzi (CCM) kuhusu Rasimu ya Katiba na pili msimamo wa Serikali
ambayo mimi ni Waziri tena mwenye dhamana ya Katiba,” alisema na
kuongeza:
“Msimamo wa CCM ni Serikali mbili na wanachama
wote nikiwamo mimi tunajua hivyo. Lakini kuna suala la Serikali ambayo
ndiyo iliyoamua kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa kadri ya uelewa
wangu, Serikali haijatoa msimamo na inaunga mkono kazi inayofanywa na
Tume.”
Alisema mambo hayo mawili hayapaswi kuchanganywa
na kuwa kila chombo (CCM na Serikali) kinaweza kutoa kauli au msimamo
kadri kinavyoona inafaa.
Licha ya kusema kwamba jukumu la kisheria la
kuandaa Uchaguzi Mkuu ni la Tume ya Taifa ya Uchaguzi, alisisitiza kuwa
ili ufanyike mwaka 2015 chini ya muundo wa Serikali Tatu unaopendekezwa
na Tume ya Warioba, basi itabidi yafanyike mabadiliko makubwa ya sheria
mbalimbali kazi ambayo haiwezi kufanywa kwa kukurupuka.
Hata hivyo, alisema maoni yake hayana maana kuwa
Uchaguzi Mkuu hauwezi kufanyika mwaka 2015, bali yanalenga kuonyesha
kazi kubwa iliyopo mbele.
Butiku
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph
Butiku amesema baadhi ya viongozi wakuu serikalini hawataki tume itoe
ufafanuzi kuhusu mapendekezo ya muundo wa Serikali tatu kwa kuwa unagusa
vyeo vyao.
Aidha, amesema hakuna haja ya kuwa na hofu kwani
tayari Zanzibar imekwishaanza kujitegemea ikiwa na bendera yake, wimbo
wake wa taifa na sasa inaidai Serikali yake kamili.
Butiku alitoa kauli hiyo juzi wakati wa kikao cha
Baraza la Katiba la Wilaya ya Moshi Vijijini, ambacho kilitawaliwa na
mvutano mkubwa miongoni mwa wajumbe kuhusu suala la kuwapo kwa Serikali
tatu, huku wajumbe ambao ni madiwani, viongozi na wafuasi wa CCM
wakitaka Serikali mbili.
Alisema kwa hali ilivyo sasa, tayari Zanzibar ina
Serikali yake yenye mihimili yote ya dola na tume ilichokipendekeza ni
kuiondoa Serikali ya Tanzania Bara kwenye ‘tumbo’ la Muungano.
Butiku alisema sababu hasa ya Zanzibar kutaka kuwa
na nchi yao ni hofu ya kumezwa na Tanzania Bara katika Muungano wa
Serikali mbili na hofu hiyo bado haijakwisha na inazidi kukua.
Butiku aliyataja mambo ambayo Zanzibar iliyafanya
kwa baraka za marais wa wakati huo licha ya kwenda kinyume cha Katiba
kuwa ni pamoja na kuwa na bendera yao pamoja na wimbo wa taifa.
Alisema Baba wa Taifa, hayati Julius Nyerere alifariki akiwa na
imani kuwa Serikali tatu zitavunja Muungano na alifanya hivyo kwa sababu
alitaka kuwapo kwa nchi moja.
Butiku alisema hata Mwalimu Nyerere katika kitabu
chake alichoandika baada ya Kundi la Wabunge la G55 kutaka Serikali ya
Tanganyika, alizungumzia kuwa na Serikali moja au Shirikisho.
Nyongeza na Daniel Mjema, Mos
Source: Mwananchi news paper