Kwa ufupi
Siku ya Mandela huadhimishwa kuenzi kazi za kiongozi
huyo alizozifanya kwa miaka 67 akiutumikia umma wa wananchi wa Afrika
Kusini, zikiwamo vita dhidi ya ubaguzi wa rangi na hatimaye kuwa Rais wa
kwanza mzalendo kwa miaka mitano, kisha kustaafu.
Johannesburg: “Happy birthday Mzee Madiba.” Rais
wa kwanza na mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, leo anatimiza
umri wa miaka 95, pia anatimiza siku ya 40 tangu alipolazwa katika
Hospitali ya Medclinic, Pretoria kwa ajili ya matibabu.
Nelson Rolihlahla Mandela, alizaliwa Julai 18,
1918 katika Kijiji cha Mvezo, eneo la Mthatha, Transkei Mkoa wa Eastern
Cape na ametumia zaidi ya asilimia 70 ya maisha yake akipigania haki na
usawa wa wananchi wa Afrika Kusini.
Maadhimisho ya miaka 95 tangu kuzaliwa kwa Mandela
yanabeba uzito mkubwa kuliko maadhimisho mengine yaliyotangulia kwani
kwa siku 40, wananchi wa Afrika Kusini wamekuwa katika wasiwasi mkubwa
hasa kutokana na kuzorota kwa afya ya kiongozi huyo.
Mandela alilazwa katika hospitali hiyo Juni 8, mwaka huu akiugua magonjwa ya figo na afya yake imeelezwa kuwa ni mbaya.
Leo, Rais Jacob Zuma atawaongoza mamilioni ya
wananchi wa Afrika Kusini katika maadhimisho ya nne ya kimataifa ya
‘Siku ya Mandela’ ambayo yanakwenda sambamba na siku yake hiyo ya
kuzaliwa.
Tangu kulazwa kwa Mandela huko Pretoria, Rais Zuma
amekuwa akiwahimiza wananchi wake wajiandae kusherehekea miaka 95 ya
Mandela akiwatia moyo wale waliokuwa na wasiwasi kwamba Madiba
asingeweza kuifikia leo kutokana na matatizo ya kiafya.
Siku ya Mandela huadhimishwa kuenzi kazi za
kiongozi huyo alizozifanya kwa miaka 67 akiutumikia umma wa wananchi wa
Afrika Kusini, zikiwamo vita dhidi ya ubaguzi wa rangi na hatimaye kuwa Rais wa kwanza mzalendo kwa miaka mitano, kisha kustaafu.
Pia ‘Mandela Day’ hutumika kukumbuka kampeni yake
dhidi ya ubaguzi wa rangi na utetezi wa haki za binadamu maarufu kwa
jina la “46664”, ambayo ni namba ya utambulisho aliyoitumia alipokuwa
mfungwa katika Gereza la Visiwa vya Robben.
Dakika 67 za Mandela
Kwa maana ya Siku ya Mandela ambayo pia
imeidhinishwa na kutambuliwa na Umoja wa Mataifa, wananchi wa Afrika
Kusini wanatumia dakika 67 kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa
ni hatua ya kuenzi kile wanachokiita ‘kazi za mtu aliyejitoa maisha yake
kwa ajili ya kupigania haki na utu’.
Dakika hizo 67 zinawakilisha idadi kama hiyo ya
miaka ambayo Mandela alitumika, hivyo Waafrika Kusini watakuwa wakitoa
msaada na huduma kwa jamii iwe ni kwa watoto yatima au watu wengine
ambao ni wahitaji katika jamii.
Kituo cha Kumbukumbu ya Mandela kimewataka
wananchi kuungana na kuonyesha ushirikiano wao kwa Mandela kwa kutumia
dakika 67 za muda wao kuzisaidia jamii zao ili kumuenzi kiongozi huyo
ambaye ni alama ya dunia.
Kumbukumbu za kihistoria zinaonyesha kuwa alianza kampeni na
harakati za kutetea haki za binadamu mwaka 1942 na baadaye mwaka 1964
alikamatwa na kuwekwa gerezani alikokaa miaka 27 lakini alipotoka
aliwatumikia Waafrika Kusini akiwa rais wao wa kwanza mzalendo.
Mkurugenzi Mkuu wa Kituo hicho, Sello Hatang aliwataka Waafrika Kusini kufanya shughuli yeyote ile au msaada ambao utakuwa ni mchango kwa jamii yao.
“Watu wafanye kile wanachoona kinawapendeza,
watumie dakika 67 za kumuenzi Mandela. Ni vyema wakafanya kitu ambacho
kinawafurahisha ili waendelee kukifanya kila mwaka katika maisha yao”,
alisema Hatang.
Alisema Waafrika Kusini wanaweza kumuenzi Mandela
kwa kuwasaidia wazee na watoto yatima katika vituo mbalimbali, kufanya
usafi au kuwatazama na kuwapa chochote wagonjwa.
Miaka 15 ya ndoa
Siku hii pia inakwenda sambamba na kumbukumbu ya
miaka 15 ya ndoa yake na mke wake wa tatu; Graca Machel ambaye walifunga
naye ndoa Julai 18, 1998 wakati wa kumbukumbu ya miaka 80 ya kuzaliwa
kwake.
Pia siku hii inaadhimishwa siku tatu baada ya
kutimia miaka 69 tangu Mandela alipofunga ndoa na mkewe wa kwanza Evelyn
Mase Julai 15, 1944. Evelyn ambaye sasa ni marehemu alikuwa muuguzi,
pia binamu wa aliyekuwa mpigania uhuru wa Afrika Kusini, Walter Sisulu.
Graca ndiye mtu wa karibu zaidi na Mandela kwa
sasa na kwa siku 40 amekuwa akiishi hospitalini Medclinic akimuuguza
mumewe na mchana kutwa amekuwa akikaa pembezoni mwa kitanda cha Mandela
na pale anapochoka hasa usiku, hulala kwenye chumba kinachopakana na
kile alicholazwa mumewe.
Ndugu wengine kutoka familia ya Mandela wamekuwa
wakifika hospitalini mara kwa mara kumjulia hali kisha kuondoka.
Miongoni mwao ni pamoja na mtalaka wake, Winnie Madikizela-Mandela
pamoja na binti yake mkubwa, Makaziwe ambaye ni binti pekee wa Mandela
aliye hai aliyemzaa kwa Evelyn miaka 60 iliyopita.
Nje ya Medclinic, kuta za uzio unaozunguka
hospitali hiyo zimeendelea kupambwa kwa kadi, michoro, picha, maua na
ujumbe ambao unamtakia heri ya kupona haraka Mzee Mandela. Hata hivyo,
leo pengine na siku chache zijazo kuta hizi zitageuzwa kuwa mahali pa
salamu za pongezi kwa Mandela kufikisha umri wa miaka 95.
Mbali na hayo, kwenye kuta za Medclinic, katika
lango la kuingilia hospitalini hapo, nyimbo na sala vimeendelea kusikika
kutoka makundi mbalimbali kumwomba Mungu ampe maisha marefu zaidi.
Miongoni mwa vikundi vilivyokuwapo hapo vikipaza
sauti zao ni kwaya ya Shule ya Sekondari ya Juu ya Wasichana ya Oranje
ambao ni siku chache tu ilirejea kutoka katika tamasha la muziki la
vijana huko Slovakia na kupata ushindi dhidi ya vikundi vingine 22.
Mandela ni nani?
Kwa jumla, Mandela unaweza kumwita utakavyo kwa
maana ya ukombozi na Afrika Kusini ya sasa. Kwa maana hiyo ni
mwanasiasa, mpigania uhuru, mwanasheria, mfungwa wa uhaini, Baba wa
Taifa la Afrika Kusini, Chifu wa Wathembu na zaidi ya yote, Rais wa
Kwanza Mzalendo wa Afrika Kusini.
Nelson Rolihlahla Mandela ni mtoto wa Mama
Nonqaphi Nosekeni na Mzee Henry Mgadla Mandela ambaye alikuwa Kiongozi
wa Kimila (Chifu) katika jamii ya Wathembu.
Awali, kabla ya kuitwa Nelson, alijulikana kwa
jina lake la kati, Rolihlahla ambalo maana yake ni ‘kungo’a tawi kutoka
kwenye mti’ au kwa maana isiyo rasmi ‘mtu mkorofi’. Jina la Nelson
alipewa na mwalimu wake alipojiunga na shule ya wamisionari.
Mandela aliishi na baba yake kwa miaka 12 tu kwani
mzazi wake huyo alifariki dunia mwaka 1930 na kuanzia hapo alilelewa na
mpwa wa baba yake, David Dalindyebo ambaye pia alikaimu uongozi wa
katika jamii ya Wathembu.
Mwaka 1944, Mandela alioana na Evelyn ambaye
alijaliwa kupata mtoto wa kiume mwaka 1945 na kumwita Madiba Thembekile
(Thembi kwa kifupi). Hata hivyo, mtoto huyo alifariki katika ajali ya
gari mwaka 1969 wakati Mandela akiwa jela.
Mandela na Evelyn walijaliwa kupata watoto wengine
watatu; Makaziwe mkubwa ambaye hata hivyo, alifariki dunia akiwa
mchanga 1948, Makgatho Mandela aliyezaliwa 1950 na kufariki 2005 na
Makaziwe mdogo mwaka 1953 ambaye kwa jumla ndiye anayesimamia shughuli
na mali katika familia hivi sasa.
Desemba 1956 alikuwa mmoja wa washtakiwa wa kesi
ya uhaini na wakati kesi hiyo ikiendelea alioana na Nomzamo Winifred
Madikizela mwaka 1958. Alibahatika kupata naye watoto wawili wa kike.
Kijijini Qunu
Kumekuwa na harakati nyingi za maadhimisho ya Siku
ya Mandela na mojawapo ni tukio la Waafrika Kusini wawili waliopanda
Mlima Kilimanjaro kumuenzi.
Katika Kijiji cha Qunu, vijana wamejipanga
kusafisha mitaa, kupaka rangi shule, huku wanasiasa wakitumia kila mmoja
dakika 67 kuzindua au kukamilisha mradi wowote wa kitaifa.
Watoto wote katika shule za msingi na sekondari wametakiwa kuanza vipindi vyao vya masomo kwa kuimba ‘happy birthday’ Mandela.
Msemaji wa Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, huko Port
Elizabeth, Jean Makasiwe alisema kila mhadhiri, mwanafunzi na
mfanyakazi wa chuo hicho atashiriki kwa namna moja au nyigine kumuenzi
Mandela.
“Natumaini kuwa kila mmoja atashiriki, ingawa yeye
Mandela hataifurahia siku hiyo muhimu kwake, lakini tuna hakika
atafanya hivyo wakati akiadhimisha miaka 96 hapo mwakani,” alisema
Makasiwe.
Alisema chuo hicho kilijengwa kwa kumbukumbu ya Mandela, hivyo ni lazima kila mmoja ajitoe kumuenzi baba huyo wa taifa.
Rais Zuma leo atakabidhi nyumba 300 kwa wazungu wa eneo la Bethlehemu huko Pretoria ambao wanaishi katika makazi duni.
Umoja wa Mataifa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban ki Moon
amewataka watu wote duniani kuadhimisha siku hiyo kwa kufanya kazi nzuri
kwa watu na kwa dunia.
“Hii ndiyo namna pekee ambayo tunaweza kumlipa mtu
huyu wa kipekee ambaye alijitoa kwa namna ya pekee kuwasaidia watu wa
taifa lake,” alisema Ban na kuongeza:
“Mandela alitumia miaka 67 kupigania haki za
binadamu, usawa na umoja. Katika kuadhimisha siku hii, UN inashiriki kwa
kuwataka watu ulimwenguni kutoa dakika 67 za muda wao kwa ajili ya
kuadhimisha.”
Watu tisa kati ya 10 Afrika Kusini, wapo tayari kushiriki kikamilifu kusherehekea na kutoa muda wao kumuenzi Mandela.
Asilimia 89 ya watu 16,046 waliofanyiwa uchunguzi
wamekubali kutoa dakika 67 za muda wao kwa ajili ya kufuata njia ya
kujitoa kwa jamii kama Mandela alivyofanya.
Utafiti huo uliotolewa jana na Kampuni ya
Pondering Panda ulionyesha kuwa karibu Waafrika Kusini wote wapo tayari
kusherehekea Sikukuu ya Mandela kwa kujitoa kusaidia, kuchangisha fedha,
kufanya usafi, kuhudumia wagonjwa na yatima.
“Idadi hii inaonyesha kuwa tutafanya mambo makubwa
hapa nchini kupitia siku hii, hapo kesho (leo), tunataka kila mtu
aonyeshe kuijali siku hii kama Mandela alivyosema,” alisema Msemaji wa
Pondering Panda, Shirley Wakefield.
Alisema Siku ya Mandela iliundwa maalumu kwa ajili ya
kuwaunganisha Waafrika Kusini wote wenye mapenzi mema kwa nchi yao na
duniani kote.
Katika eneo la Upington, kundi la wazee linamuenzi
na kumshukuru Madiba kwa kuwapa eneo la makazi na wanasema pasipo
jitihada zake za 1998, wasingeweza kupata eneo hilo.
Huko Eastern Cape alikozaliwa Mandela, baadhi ya
shule za msingi zilinufaika na Wiki ya Mandela baada ya kupata ufadhili
wa seti zote muhimu za vifaa vya kompyuta ambavyo awali hawakuwa navyo.
chanzo: Mwananchi news paper