Na Sharon Sauwa, 15th July 2013
Chama cha Mapinduzi (CCM)
Harakati hizo zinatokana na kusambaza waraka unaojulikana kama ufafanuzi kuhusu rasmu ya kwanza ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wanachama na viongozi wa CCM.
Ufafanuzi huu licha ya kutumika kama kitini katika semina za wanachama wa CCM waliochaguliwa kuwa wajumbe wa mabaraza ya Katiba ya Wilaya, pia umesambazwa katika baadhi ya makundi mengine ya jamii.
Akitoa mahubiri katika ibada ya misa ya kwanza katika Kanisa Katoliki Parokia ya Uwanja wa Ndege, Paroko wa kanisa hilo, Sostenesy Luyembe, alisema ufafanuzi huo unalenga katika kukidhi matakwa ya CCM na si ya Taifa.
“Mimi nimeletewa hapa na CCM na nimesoma. sehemu kubwa inalenga katika kukidhi interest (matakwa) yao na si ya Taifa kwa ujumla hali ambayo inaonyesha kutakuwa na mvutano wa kimakundi bila kujali maslahi ya Taifa zaidi,”alisema.
Ufafanuzi huo ambao NIPASHE unao, umeanza na kueleza kipengele katika rasimu hiyo na kisha maoni ya chama, sababu za kukataa na baadaye kusisitiza kuhusiana wana CCM kuwa makini na kutoa maoni yao.
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, CCM inasema sera ya chama hicho ni muundo wa serikali mbili kama ilivyo sasa.
Chama hicho kimependekeza kuondolewa kwa shughuli za utendaji zinazohusu Tanzania Bara katika kipengele cha 57(1)(C), na Ibara ya 57(3), zisimamiwe na Serikali ya Muungano na zile za Zanzibar zisimamiwe na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ).
Sababu ya kukataa muundo wa serikali tatu zipo katika maeneo manne ya kisheria, kisiasa, kiuchumi na kijamii.
KISHERIA
Misingi mikuu ya muungano kati ya iliyokuwa Jamuhuri ya Tanganyika na Jamuhuri ya Watu wa Zanzibar ni wa serikali mbili kwa mujibu wa makubaliano ya mwaka 1964
Mfumo wa serikali tatu utaleta urasimu na utata wa kisheria katika umiliki na uendeshaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii.
Kusababisha mgogoro wa kisheria kuhusu uwakilishi katika Bunge la jamuhuri ya Muungano kwasababu majimbo yatakuwa mikoa kwa bara na wilaya kwa Zanzibar wakati uundwaji wa mikoa na wilaya si ya muungano.
KISIASA
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano itaelea kimadaraka na kimamlaka kwa kuwa haitakuwa na uwezo wa kushughulikia moja kwa moja masuala yanayowahusu wananchi ingawaje rasimu hiyo yanazungumziwa kama mambo ya muungano.
KIUCHUMI
Serikali ya Muungano itakuwa tegemezi kwa serikali zinazounda muungano hasa ya Bara ambayo uchumi wake ni mkubwa.
Urasimu wa kibiashara na umilikaji wa ardhi utaongezeka kwasababu ardhi na umilikaji mali wa aina nyingine si mambo ya Muungano.
Gharama za uendeshaji wa serikali zilizopo hivi sasa ni kubwa na kuwepo kwa serikali ya tatu kutakuwa ni gharama za ziada na hivyo kuwa mzigo mkubwa kwa wananchi.
KIJAMII
Muundo unaopendekezwa utahatarisha amani, utulivu na utangamano wa kitaifa kwani watu wa pande mbili za Muungano wamekuwa na uhusiano na mwingiliano kwa miaka mingi.
Aidha, CCM wanataka kufutwa kwa ibara ya 117(1)(e) inayomuondolea mbunge aliyewahi kuwa mbunge kwa vipindi vitatu kwasababu nafasi ya ubunge ni ya uwakilishi na wapiga kura ndio watakaoamua ukomo wa uwakilishi wa mtu waliyemchagua.
sOURCE:IPPMEDIA