Posted Alhamisi,Julai11 2013 saa 15:7 PM
Kwa ufupi
Arusha. Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua
Nasari, amewasili Arusha na kupokelewa na ulinzi mkali wa polisi,
kuanzia uwanja wa ndege wa Arusha hadi ofisi yake ya ubunge Arumeru
Mashariki.
Nassari ambaye jana alitarajiwa kupokewa na mamia
ya wanachama wa chama hicho, baadaye angefanya mkutano wa hadhara
jimboni kwake, aliwasili saa 6:00 Uwanja wa Ndege Arusha.
Hata hivyo, polisi ilitangaza kufuta mapokezi na
mkutano wake, kwa maelezo kuwa ni kutekeleza uamuzi ya Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (Nec kuzuia shughuli zozote za kisiasa Arusha hadi kukamilika
uchaguzi wa madiwani Julai 14, mwaka huu.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas,
alisema wamelazimika kuongeza ulinzi na kuzuia mapokezi hayo na mkutano,
kwani vingekiuka maagizo ya Nec.
Akizungumza ofisi za Chadema Mkoa wa Arusha jana, Nassari alieleza kushangazwa na ulinzi mkali wa polisi.
“Ulinzi huu umeanzia Dar es Salaam Airport (uwanja
wa ndege), nimeshuka Arusha hadi sasa polisi wanarandaranda nje ya
ofisi hizi,” alisema Nassari.
Pia, mbunge huyo alieleza kushangazwa na polisi
kuweka ulinzi ofisi yake, huku wananchi wenye shida wakishindwa
kuzungumza naye kwa uhuru.
Alisema amerejea Arusha salama na sasa amepona yupo tayari kushiriki kama wakala wa uchaguzi mdogo wa Jumapili.
Akizungumzia maandalizi ya uchaguzi mdogo, Katibu
wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa, alisema chama kimewapanga
wabunge wake kadhaa kuwa mawakala.
“Tumeunda vikosi na Godbless Lema (Mbunge Arusha Mjini) atakuwa anaongozwa kikosi cha QS1 hakuna matata,” alisema Golugwa.