Kwa ufupi.
Julai 20, mwaka huu: “Uwepo wa Serikali tatu
utafumua mfumo mzima wa utendaji ndani ya Serikali. Hatuwezi tena
kufanya uchaguzi wa Rais na wabunge 2015, hatuwezi kufanya chochote nje
ya Katiba ya Serikali Tatu kwa kuwa kinachofuata ni kuunda Katiba
nyingine inayohusiana na Serikali tatu.”
HUKU Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikiwa kimeweka
bayana kwamba hakiungi mkono Serikali tatu kama Rasimu ya Katiba
inavyoonyesha, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe ameibuka na
kusema endapo Mabaraza ya Katiba yatawasilisha hoja za kuikubali, kuna
uwezekano mkubwa wa Uchaguzi Mkuu wa 2015 kukwama.
“Uwepo wa Serikali tatu utafumua mfumo mzima wa
utendaji ndani ya Serikali. Hatuwezi tena kufanya uchaguzi wa Rais na
wabunge 2015, hatuwezi kufanya chochote nje ya Katiba ya Serikali Tatu
kwa kuwa kinachofuata ni kuunda Katiba nyingine inayohusiana na Serikali
tatu.
“Kama tutafanya uchaguzi, utafanyika kwa taratibu
zipi, ipi itakuwa mipaka ya marais wa Serikali tatu, makamu na mawaziri
wakuu, mfumo wa Mahakama, Tume ya Uchaguzi, utendaji wa Bunge na
wabunge, yako mengi, sasa mpaka hayo yaingie kwenye Katiba,” alisema
Chikawe juzi Dar es Salaam.
Alisema lazima CCM isimamie suala hilo kwa kuwa
kukubali Serikali tatu kutaua Muungano ambao sehemu kubwa unalindwa na
chama hicho tawala.
“CCM wamejipanga kama baraza na kusimamia hili la
Serikali mbili ambalo lengo ni kuulinda Muungano. Litakapokuja hili la
Serikali tatu, lazima Muungano uparaganyike,” alisema.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Waziri Chikawe
inakinzana na ile aliyoitoa Juni 4, siku moja baada ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kutangaza hadharani Rasimu hiyo.
Waziri huyo alikaririwa na gazeti hili akisema upo
uwezekazo wa Katiba Mpya ya Tanzania Bara ikapatikana kabla ya Uchaguzi
Mkuu wa 2015 ikiwa mchakato wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano
utakamilika kama inavyokusudiwa na rasimu hiyo kupitishwa na wananchi
katika ngazi zote bila mabadiliko.
“Watu wasiwe na hofu. Sioni tatizo endapo rasimu
itapita bila mabadiliko na kupata Katiba Mpya. Aprili mwakani mpaka
Desemba inatosha kabisa kuandaa Katiba ya Tanzania Bara na tukaenda
katika Uchaguzi Mkuu tukiwa na Katiba Mpya,”alikaririwa akisema na
kuongeza:
“Tunaweza kuwatumia wajumbe walewale wa Tume ya
Katiba lakini safari hii tukawachukua wale wa Tanzania Bara pekee
wakashiriki katika kuandaa Katiba hiyo.”
Alisema kutokana na muda kuwa mfupi, Tume hiyo
inaweza isifanye kazi ya kukusanya maoni kutoka kwa wananchi kama
ilivyofanya sasa na badala yake ikaandaa rasimu na kujadiliwa na wadau
kisha kupelekwa katika mabaraza ya Katiba kabla ya kupata Katiba Mpya.
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajiwa
kukamilika Aprili mwakani.
Alisema kuanzia hapo, Serikali inaweza kuitumia
tume ya sasa kutangaza rasimu ya kwanza ya Katiba ya Tanzania Bara kwa
kurejea maoni iliyokusanya hivyo hatua ya kwanza ikawa ni kujadiliwa kwa
rasimu hiyo kwenye mabaraza ya Katiba kwa miezi miwili na baadaye
kupelekwa katika Bunge la Katiba jambo litakaloifanya ipatikane mapema.
Alisema kinachotakiwa sasa ni kujiandaa kwa Tanzania Bara kuwa
na Katiba yake ambayo itatumika kwa ajili ya mambo mbalimbali, ukiwamo
Uchaguzi Mkuu wa 2015 na kuwatoa hofu Watanzania kwamba hakuna mpango wa
kumwongezea muda wa uongozi, Rais Jakaya Kikwete kama ambavyo imekuwa
ikielezwa kwani Serikali ina uhakika kwamba kila kitu kitafanyika katika
muda uliopangwa.
Kauli hiyo ilikuwa ikirejea shaka ya Mwenyekiti wa
CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba kuwa Serikali ina mpango wa kumwongezea
Rais Kikwete muda wa kuongoza.
Juzi, Waziri Chikawe aliwaonya Wazanzibari akisema
endapo mapendekezo ya Serikali Tatu yatapita, ni wazi kuwa wataumizwa
na muundo wake kwa kuwa bado ni tegemezi kwa Tanzania Bara.
“Ukiangalia Wazanzibar wako milioni moja hivi na
ukija Tanzania Bara wako milioni 44, halafu tuseme uwepo na mgawanyiko
sawa wa mapato na matumizi kwa ajili ya Serikali ya Shirikisho, ni wazi
hali itakuwa mbaya kwa Zanzibar.
Alisema Wazanzibari wanaoshabikia suala la
Serikali tatu bila kufahamu madhara ama muundo wake watafikia hatua
watataka Serikali mbili ziendelee.
Alisema kukubali kuwapa nafasi wanaotaka Serikali
tatu ni kama demokrasia na ni wazi kuwa watatoa hoja zao hadi mwisho na
watakapokuja kufanya upembuzi yakinifu, wataona kumbe wamepotoka.
Akizungumzia hoja hiyo, Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema: Tuachieni muda… hayo
mengine ni hisia tu. Ni kweli tunayajua lakini acheni tumalize hili
kwanza (Mabaraza ya Katiba). Hii ndiyo hatua tuliyopo sasa.”
Amsifu Warioba kwa Serikali tatu
Lakini kwa upande mwingine, Chikawe alimsifu Jaji
Warioba akisema kukubali kwake na kuisimamia hoja ya Serikali tatu
ijadiliwe, kumeliepusha taifa kuingia kwenye machafuko ya kisiasa.
“Nampongeza sana Jaji Warioba kwa msimamo wake...
Amesimamia Serikali tatu, ana maana yake. Juni 3, wakati akitangaza
mapendekezo ya Rasimu ya Katiba, Jaji Warioba amekuwa akisimamia suala
la Serikali tatu na amekuwa akiipigania mara zote anapokuwa majukwaani,
huku akisisitiza kuwa Muungano utaimarika.”
“Unajua watu hawakumwelewa Jaji Warioba, kama
angekuja na suala la Serikali mbili, ni wazi ingekuwa mzozo mkubwa wa
kisiasa, kungekuwa na kutokuelewana kuwa katumwa... Anasimamia chama
chake na watu wangetumia nafasi kufanya vurugu kwa kisingizio cha kudai
Serikali yao, lakini sasa hilo halipo,” alisema.
Source: Mwananchi news paper
Source: Mwananchi news paper