Posted Julai20 2013 saa 22:30 PM
Kwa ufupi
Ni zile za laini ya simu zilizopitishwa na Bunge kama moja ya vyanzo vya kodi nchini na kupingwa na wengi.
Dar es Salaam. Serikali imekubali kupitia mawazo
na maoni yaliyotolewa na Umoja wa Wamiliki wa Kampuni za Simu Nchini
(MOAT), kuhusu kufutwa kwa tozo ya kodi ya laini za simu ‘Simcard tax’
ya Sh1000 kutokana na kulalamikiwa na wadau wa sekta ya mawasiliano.
Hali hiyo inatokana na kauli za viongozi wa
Serikali, wabunge na wananchi wanaopinga tozo hiyo kwa kile
wanachokieleza kitaongeza mzigo wa ugumu wa maisha kwa mtumiaji hususan
wa kipato cha chini.
Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa akizungumza na
wandishi wa habari jana alisema, wamekutana na MOAT na kupokea
mapendekezo yao na sasa wanayafanyika kazi.
“Tumeendelea kusikia malalamiko kutoka pande
mbalimbali na juzi, tulikutana na MOAT na tumejadiliana na wametoa
mapendekezo mazuri tu kipi kifanyike ili tupunguze makali ya kodi hii
hususan kwa wananchi wa hali ya chini,” alisema Dk Mgimwa na kuongeza:
“Katika suala hili, jazba zisiwepo kwani ni suala
la kisheria kutokana na kupitishwa bungeni hivyo ili kuondolewa ni
lazima kufuata mkondo na tunatizama mapendekezo ya jinsi ya
kulishughulikia.”
Dk Mgimwa aliendelea kusema “Hakuna mtu anayelenga
kumkamua mwananchi,lakini hili lilitokana na mapendekezo 67
yaliyotolewa na Kamati ya Bajeti kuwa chanzo cha mapato
kinachotekelezeka lakini kama inaonekana kuwa kikwazo tutangalia jinsi
ya kukabiliana nalo.”
Waziri huyo alisema lengo la tozo hiyo ilikuwa
kupata fedha zitakazoelekezwa katika miradi ya maji, barabara na umeme
hususani vijijini kunakokabiliwa na changamoto mbalimbali muhimu za
maendeleo.
Alisema mpaka sasa hakuna mtumiaji wa huduma hiyo
ambaye ameanza kukatwa tozo hiyo kutokana na mchakato huo kuwa bado
unaendelea katika utekelezaji wake.
Naye Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,
Profesa Makame Mbarawa alisema, Serikali itahakikisha mwananchi hapati
mzigo usiokuwa na sababu.
“Serikali ni sikivu na inawasikiliza wananchi wake
hivyo kupitia mawazo na mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa yanafanyiwa
kazi ili kutokuathiri pande zozote,” alisema Profesa Mbarawa.
Profesa Mbarawa alisema, uwekezaji hususani vijini
umekuwa ukikabiliwa na changamoto za miundombinu ya barabara, umeme na
maji vitu ambavyo vikiboreshwa vitawavutia wawekezaji wengi.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, Januari Makamba Juzi alisema, wizara hiyo ilipinga tangu
awali mpango huo kabla ya kupitishwa na kuwa sheria na kwamba anaamini
itaondolewa.
Nacho chama tawala, CCM,Chadema walikaririwa na vyombo vya habari wakiitaka Serikali kuangalia vyanzo vingine vya mapato badala ya tozo hiyo
source: Mwananchi news paper
Nacho chama tawala, CCM,Chadema walikaririwa na vyombo vya habari wakiitaka Serikali kuangalia vyanzo vingine vya mapato badala ya tozo hiyo
source: Mwananchi news paper