Kwa ufupi
Akizungumza wakati wa hafla ya futari kwa wateja
iliyoandaliwa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) jijini Dar es Salaam
mwishoni mwa wiki, Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alisema
bidhaa hiyo imeletwa katika muda mwafaka.
Dar es Salaam. Serikali imewatoa hofu Watanzania
ikiwataka kutosita kujiunga na kutumia huduma za kifedha zinazofuata
kanuni za Kiislamu kwa kuwa huduma hiyo ni mkombozi kwa wananchi wengi.
Akizungumza wakati wa hafla ya futari kwa wateja
iliyoandaliwa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) jijini Dar es Salaam
mwishoni mwa wiki, Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alisema
bidhaa hiyo imeletwa katika muda mwafaka.
“Huduma hii hufuata sheria na kanuni za Kiislamu.
Ni huduma inayojali na kufuata maadili na ni furaha kwa Serikali kuona
kwamba hatimaye maadili sasa yanaingia hadi kwenye huduma za kifedha.
“Maadili yakiwa imara katika jamii, tunatarajia
pia kupata uchumi imara wenye kukua na viwanda vyenye kuzalisha bidhaa
na huduma zenye kukidhi mahitaji ya wote,” alisema.
Saada aliiomba NBC kuendelea kubuni na kuwaletea
Watanzania huduma nyingine zenye kukidhi mahitaji mbalimbali ya wateja,
wakubwa kwa wadogo, hususan mikopo kupitia Huduma ya Kibenki ya
Kiislamu.
Aliitaka pia benki hiyo kutoa elimu kwa Watanzania
ili waweze kufahamu kwa undani faida ya huduma hiyo ambayo iko wazi kwa
yeyote bila kujali itikadi au imani yake ya kidini.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi
Mtendaji wa NBC, Mizinga Melu alimuahidi Naibu Waziri kwamba benki hiyo
haitaacha mipango yake ya kuisaidia Serikali kutekeleza kauli mbiu yake
ya ‘maisha bora kwa kila Mtanzania’.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Huduma ya Kibenki ya
Kiislamu, Yassir Masoud alisema kuwa muda si mrefu NBC itaanzisha huduma
za mikopo kupitia bidhaa hiyo, akisisitiza kwamba wanaelewa kuwa watu
wengi wanaisubiri kwa hamu kubwa.
Huduma ya Islamic Banking ya Benki ya NBC ilizinduliwa Mei 2010.
chanzo: mwananchi news paper
cha
chanzo: mwananchi news paper
cha