Meya wa Jiji la Arusha, Gaudance Lyimo (CCM) 
            
Kwa ufupi
Meya huyo aliwataka madiwani kutoka Chadema 
kuacha kupoteza muda na nguvu nyingi kuweka mikakati ya kumng’oa 
madarakani, badala yake watumie muda na nguvu hizo kuwatumikia wananchi 
waliowaamini na kuwapigia kura kwenye uchaguzi
Arusha.Meya wa Jiji la Arusha, 
Gaudance Lyimo (CCM), ametamba kuwa wanaofikiria kumng’oa kwenye kiti 
chake wanaota ndoto za alinacha kwa sababu lazima wazingatie kanuni za 
uendeshaji wa Mabaraza ya Madiwani.
Baada ya kushinda kata nne za Arusha kwenye 
uchaguzi mdogo juzi, Chadema ilitamba kuwa kazi inayofuata ni kumng’oa 
Meya kutokana na kuwa na viti vingi kwenye Baraza la Madiwani.
Lyimo aliliambia Mwananchi kuwa pamoja na Chadema kuwa wajumbe wengi kwenye Baraza la Madiwani, bado hawana ubavu wa kumtoa.
Alisema ili kumtoa katika nafasi hiyo wanahitaji 
kuwa na theluthi mbili ya wajumbe . Lyimo alisema maana yake ni kuwa ili
 ang’oke lazima Chadema waungane na madiwani wa CCM ndiyo watafanikisha 
azma hiyo.
“Sharti la kumng’oa madarakani Meya au Mwenyekiti 
wa halmashauri ni kupata theluthi mbili ya kura za wajumbe wote. 
Najiuliza wenzetu watafikiaje kiwango hicho hadi waanze kutamba 
kuning’oa madarakani,” alisema Lyimo.
Jiji la Arusha lina jumla ya wajumbe 32 kwenye 
Baraza la Madiwani ambapo ukimtoa Meya, wajumbe wanaostahili kupiga kura
 wanasalia 31 hivyo kufanya wenye nia ya kumng’oa kiongozi huyo kuhitaji
 zaidi ya kura 24 kutimiza lengo lao.
Baada ya kunyakua viti vyote vinne
 kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika Jumapili iliyopita, Chadema 
imefikisha wajumbe 15 kwenye baraza ikiwa ni madiwani 12 pamoja na 
wabunge watatu, wawili wa viti maalumu na mmoja wa jimbo.
Kwa upande wake, CCM kimebakia na wajumbe 14, 
ikiwa ni madiwani 11 na wabunge watatu wa viti maalumu, huku TLP ikiwa 
na wajumbe wawili ambao ni diwani mmoja wa kata na mwingine wa viti 
maalumu.
Kata ya Sombetini ambayo awali ilishikiliwa na CCM
 iko wazi baada ya aliyekuwa diwani wake, Alphonce Mawazo kujivua 
uanachama na kuhamia Chadema.
Kutokana na mchanganuo huo, Meya Lyimo alisema 
hana hofu ya kupoteza nafasi yake kwa sababu ili Chadema wafikie lengo 
hilo, ni lazima waungwe mkono na wajumbe kutoka CCM, jambo alilosema ni 
ndoto ya kutokea.
“Nakusisitizia ndugu yangu, mimi nipo na 
nitaendelea kuwepo hadi mwisho wa kipindi changu kwa uwezo na msaada wa 
Mwenyezi Mungu. Hakuna wa kuning’oa. Hata leo nilikuwa ofisini 
kutekeleza majukumu yangu ya kuongoza kikao cha kamati ya fedha,” 
alitamba Lyimo.
Meya huyo aliwataka madiwani kutoka Chadema kuacha
 kupoteza muda na nguvu nyingi kuweka mikakati ya kumng’oa madarakani, 
badala yake watumie muda na nguvu hizo kuwatumikia wananchi waliowaamini
 na kuwapigia kura kwenye uchaguzi.
Chanzo: Mwanachi
Alisema kwa nafasi yake ya Umeya, atashirikiana na madiwani wote
 kutatua kero na kutafutia ufumbuzi matatizo ya wananchi bila kujali 
tofauti zao kiitikadi kwa sababu suala la maendeleo halina itikadi, dini
 wala ukabila.
Akizungumzia kiti cha Umeya, Katibu wa Chadema 
Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alisema ajenda kuu ya Chadema ni 
kupata wingi wa kura na hivyo kuwa na uamuzi katika Baraza la Madiwani 
limefanikiwa baada ya kurejesha kata zake zote nne.
“Hata kama wenzetu wataendelea kubaki na Meya wao 
wa ‘kuchonga’, bado uamuzi wote unayohitaji kura kwenye baraza la 
halmashauri yatasimamiwa na kuongozwa na Chadema. Hilo ni faraja na 
ishara njema ya kunyakua uongozi wa halmashauri na nchi katika uchaguzi 
mkuu ujao,” alisema Golugwa.
Tangu achaguliwe kushika wadhifa huo mwaka 2010, 
Meya Lyimo amekuwa akipingwa na Chadema kwa madai kuwa hakuchaguliwa 
kihalali ambapo Januari 5, 2011, chama hicho kikuu cha upinzani 
kiliitisha maandamano makubwa kumpinga ambayo yaliishia kwa watu 
kujeruhiwa na kuuawa baada ya polisi kuyasambaratisha.
Chanzo: Mwanachi
 
  