Kwa ufupi
Ingawa Kikwete hakuitaja Chadema kwa jina, lakini
chama hicho ndicho pekee kilichosusia kongamano la kutafakari amani
kikidai kwamba Serikali haitendi haki.
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete (pichani)
amekiponda Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kuanzisha
kikundi cha mgambo akisema hatua hiyo imejidhihirisha kwamba chama hicho
hakipendi amani.
Ingawa Kikwete hakuitaja Chadema kwa jina, lakini
chama hicho ndicho pekee kilichosusia kongamano la kutafakari amani
kikidai kwamba Serikali haitendi haki.
Kikwete alisema hayo jana wakati akifunga kongamano hilo lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
Chadema ilisusia kongamano hilo ikisema kuwa amani haitafutwi kwa kufanya makongamano kama ilivyofanya TCD.
“Chama cha siasa kuanzisha kikundi cha wanamgambo
kwa ajili ya kupiga watu ni kiashiria kwamba chama hicho hakitaki amani
bali kinaridhishwa na vurugu,” alisema Kikwete na kuongeza kuwa
wanaopenda amani humaliza tofauti zao kwa kuzungumza.
“Tusiiache nchi yetu ije kulindwa na majeshi ya
Umoja wa Mataifa, tusije kufikia huko, tujitahidi kuondoa tofauti zetu
kwa njia ya mazungumzo,” alisema Kikwete.
Juzi Chadema walitangaza kwamba wataanzisha
mafunzo kwa vijana wao kwa ajili ya kuwalinda ikidai kuwa dola imekuwa
haisikilizi madai yao.
Alisema wanaosusa kongamano hilo wangeweza kufika
wangeweza kutoa madukuduku yao kwa sababu viongozi wa Serikali na polisi
walikuwapo lakini bado hawataki.
“Sasa hawa kweli wanapenda amani yetu wakati
hawapendi kuja tuzungumze, wanataka watu wauane ama wapigane,” alisema
kwa mshangao Kikwete.
Alisema Serikali na viongozi wake hawapendi vurugu
na kwamba chama hicho kinafanya vurugu hizo ili kuwatoa katika ajenda
za kuwaletea maendeleo Watanzania.
Hata hivyo aliwapongeza Chadema kwa kushiriki katika maandalizi ya kongamano hilo licha ya kususia kushiriki.