Kwa ufupi
Mfanyabiashara maarufu jijini Dar es Salaam ameshambuliwa kwa kumwagiwa tindikali
Dar es Salaam. Mtu asiyejulikana juzi usiku alimvamia mmiliki wa maduka ya Home Shopping Centre, Said Mohammed Saad (pichani) na kumwagia maji usoni yanayodhaniwa kuwa ni tindikali.
Tukio hilo lililotokea juzi saa 1 usiku karibu na
kituo cha Polisi cha Oysterbay, lilithibitishwa na Kaimu Kamanda wa
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ally Mlege kwa kusema kuwa bado
polisi wanaendelea na uchunguzi wao ili kuwabaini waliohusika.
“Ni kweli tukio hili limetokea ila polisi
wanaendelea na uchunguzi. Tukikamilisha uchunguzi tunatarajia kutoa
taarifa kamili za tukio zima,” alisema na kuongeza;
“Hatuna haja ya kuficha ukweli wa tukio hili, uchunguzi wetu ukikamilika na watuhumiwa wakikamatwa kila mtu atajua.”
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi
zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa mtu huyo, alimkuta Saad akiwa
anazungumza na mmoja wa wafanyakazi wake katika duka lake jipya lililopo
karibu na Kituo cha Polisi cha Oysterbay.
“Wakati akizungumza na mfanyakazi wake, huyo mtu
alikuwa kama anapita na alichomoa kitu fulani na kummwagia Saad usoni na
kisha kukimbia,” zilieleza taarifa hizo na kuongeza;
“Baada ya tukio hilo alipelekwa katika Hospitali
ya AMI, sasa hatujui kama bado yupo hapo au ameondoka, ila sisi
tulizungumza naye na alitueleza mwonekano wa mtu aliyemwagia tindikali.”
Taarifa hizo zilifafanua kwamba polisi wanazitumia taarifa hizo walizopewa na Saad, ili kuweza kumkamata mhusika.
Taarifa hizo zilifafanua kuwa polisi wanapanga
tena siku ya kumhoji kwa mara ya pili Saad, kwamba watataka kufahamu
kama mfanyabiashara huyo alikuwa akipewa vitisho au ujumbe wowote, kabla
ya kukutwa na tukio hilo.
Hata hivyo, habari nyingine zilizolifikia
Mwananchi Jumapili zilieleza kuwa mtu huyo baada ya kummwagia Saad
tindikali, alipanda pikipiki na kutokomea eneo hilo.
“Walikuwa wawili, mmoja alikwenda kufanya unyama
na mwingine alibakia katika pikipiki, baada tu ya kumwagia tindikali mtu
yule alikimbia mpaka pale alipokuwa imesimama pikipiki, alipanda na
kuondoka kwa kasi,” zilieleza habari hizo.
Taarifa zilizopatikana jana asubuhi zilieleza kuwa
ndugu na marafiki wa mfanyabiashara huyo, walikuwa katika mipango ya
kumpeleka nje ya nchi kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
Source. Mwananchi news paper
Source. Mwananchi news paper