Kwa ufupi
Dar es Salaam. Viongozi wa madhehebu ya dini 
wametakiwa kuhakikisha wanadumisha utulivu uliopo nchini kwa kuhubiri 
amani na upendo kwa watu wote.
Rai hiyo ilitolewa katika Parokia ya Mtakatifu 
Yohane Mbatizaji Luhanga, Dar es Salaam jana na Msaidizi wa Askofu Mkuu 
Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Askofu Eusebius Nzigilwa wakati 
alipokuwa akiendesha misa ya upadrisho kwa Siriack Malasi na Shadrack 
Lyimo.
Nzigilwa alisema viongozi wa dini wana mchango 
mkubwa katika jamii, hivyo wanapaswa kuilinda na kuidumisha amani 
iliyopo na kwamba jukumu walilonalo mapadri hao wapya ni kuhakikisha 
jamii wanayoizunguka inaishi katika mazingira ya utulivu na amani kama 
ndugu.
“Nendeni mkahubiri amani, furaha na upendo kwa watu wote hiyo ndiyo kazi yenu kubwa, tunahitaji kuwa na amani,” alisema Nzigela.
Akitoa neno la shukrani baada ya kupandishwa 
daraja la upadri, Padri Siriack Malasi alisema kuwa safari ya kufikia 
hatua hiyo haikuwa rahisi na kwamba wana kila sababu ya kuwashukuru watu
 wote waliowawezesha kufika katika daraja hilo.
“Neno tunaloweza kulisema ni asante sana, tumepita
 katika wakati mgumu na mara nyingine tulikuwa tunawasumbua kidogo. Hata
 kufika kwenu hapa ni mchango muhimu, kama wangefika mapadri na maaskofu
 bila nyinyi (waumini) ingekuwaje?” alihoji Malasi.
Misa hiyo ya upadrisho iliambatana na uzinduzi wa 
kitabu cha marehemu Jackson Mosha aliyekuwa Mjasuiti ambaye alifariki 
dunia mwaka 2009.
source: Mwananchi news paper
source: Mwananchi news paper
