Chadai polisi kuvamia nyumbani kwa Mbowe
Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa tuhuma nzito kwa Jeshi la
Polisi, baada ya kudai askari wake kuvamia nyumba ya Mwenyekiti wa
chama hicho, Freeman Mbowe kwa nia ya kumkamata.
Tuhuma hizo zimetolewa na Katibu Mkuu wa
Chama hicho, Dk. Wilbroad Slaa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika
uwanja wa Ukombozi eneo la Manzese jijini Dar es Salaam jana.
Mkutano huo uliitishwa kwa ajili ya kutoa tamko kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya kwa wanachama na wafuasi wa chama hicho.
Dk. Slaa alisema polisi wakiongozwa na
mkuu wa upelelezi mkoa wa Kinondoni, walivamia nyumba ya kiongozi huyo
juzi usiku majira ya saa 6.55 na kulazimisha kuingia ndani kwa ajili ya
kumkamata.
Alisema kitendo hicho alichokiita kuwa ni
kinyume na utaratibu, kilifanywa huku ikiwa imepita siku nne tangu Rais
Jakaya Kikwete kuliagiza jeshi hilo kuacha tabia ya kuwaandama
wapinzani.
"Tunataka maelezo kwanini polisi wavamie
nyumba ya Mbowe katika muda huo ambao kisheria hawaruhusiwi kumkamata
kutokana na hadhi yake," alisema Dk. Slaa.
Aidha, alilitaka jeshi hilo kuomba radhi
kutokana na kitendo hicho alichokiita cha udhalilishaji kwa Mwenyekiti
wao wa chama, Kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni na Mbunge wa Jimbo
la Hai.
Aliwaambia wafuasi wa chama hicho kuwa
vurugu zinazotokea sehemu mbalimbali nchini zinatokana na jeshi hilo
kufanyakazi kwa upendeleo na bila kufuata taratibu za kazi.
"Polisi hawakuleta barua ya kumkamata au
kutakiwa kwenda ofisini kwao, kibaya zaidi kutokana na wadhifa wake
hastaili kukamatwa baada ya saa 12:00 jioni, kinachofanyika sasa ni
ukandamizaji wa hali ya juu," alisema.
Akijibu tuhuma hizo, Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alimtaka Dk. Slaa akasome sheria ya
polisi vizuri kabla ya kutoa tuhuma hizo.
Alisema polisi wana mamlaka ya kukamata
mtu wakati wowote na kwamba kumkamata au kutomkamata liko ndani ya jeshi
la polisi, hivyo hawezi kutoa maelezo yoyote.
Awali, wakitoa tamko la chama hicho,
Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lisu na Mjumbe wa Kamati Kuu
ya Chadema, Mabere Marando walisema chama hicho kinaunga mkono Rasimu
ya Katiba Mpya iliyotolewa na Jaji Joseph Warioba.
Walisema wanashangaa kwanini CCM inapinga
baadhi ya mapendekezo yakiwamo ya kuundwa kwa serikali tatu na tunu ya
Taifa, ikiwa vifungu hivyo vinataka kuiweka Tanzania katika hali bora na
udhibiti wa maliasili.
Lisu alitahadharisha Watanzania wawe
tayari kupiga kura ya kudai Uhuru endapo Serikali ya CCM itaendelea
kutumia nguvu kuifanya nchi kuwa ya serikali mbili ambayo imeonekana
kuparaganyika.
chanzo: Ippmedia.