Sunday 8 September 2013

CHADEMA: Tunatafakari kwa kina ni hatua gani tutamchukulia naibu spika wa bunge Mh Job Ndugai


                       
 Uongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) umesema unatafakari kwa kina ni hatua gani watamchukulia naibu spika wa bunge Mh Job Ndugai kwa kitendo cha kuamrisha askari wa bunge kumtoa nje ya ukumbi wa bunge kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni Mh Freeman Mbowe kwamba hatua hiyo ni ukiukwaji wa kanuni za bunge zilizo wazi.
Mkurugenzi wa habari na mawasiliano wa chama hicho Mh John Mnyika ameyasama hayo alipokutana wa vyombo vya habari katika ofisi za makao makuu ya chama hicho jijini Dar es salaam na kusema bado wahajajua ni hatua gani watachukua mara baada ya kukamilika kwa mfululizo wa mikutano ya sekretarieti ya chama inayoanza kesho chini ya katibu wa chama hicho Dk. Wilbroad Slaa.
Kuhusu uamuzi wa wabunge wa upinzani kutoka nje ya ukumbi wa bunge kwa lengo la kutoshiriki kuchangia hoja muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba mpya Mh Mnyika amesema hakubaliani na vipengele ambavyo vinakataka kutoa fursa ya kuongeza idadi ya wawakilishi kuongezwa katika muswaada huo ili kutoa haki ya ushiriki kwa makundi mengi zaidi katika jamii na kupata katiba bora tofauti na ilivyo sasa, hivyo chama hicho kimesema kitachukua hatua ya kurudi kwa wananchi ili kuwaeleza upungufu uliopo katika muswaada huo ambao tayari wabunge wamekwisha upitisha na kusubiriwa kuwa sheria baada ya rais kuusaini.
Wakati huo huo Chama cha wananchi (CUF) kimelaani  kitendo cha naibu spika Mh Job Ndugai  kuamuru  askari wamtoe  nje  kiongozi wa kambi ya upinzani  bungeni   Mh Freeman Mbowe kitendo walichokiita kuwa ni  cha aibu  na hakikupaswa  kufanya na kiongozi mkubwa  kama huyo.
Hayo  yamesemwa na mwenyekiti wa taifa wa  chama hicho Mh Profesa  Ibrahim  Lipumba  wakati akizungumza  makao makuu ya chama hicho jijini Dar es salaam na kusema kuwa  ni  wazi kuwa kumekuwepo  na upendeleo  mkubwa  bungeni baina wabunge wa upinzani na wale wa chama tawala.
Aidha kuhusu mchakato wa katiba mpya  Profesa  Lipumba amesema  kuna njama za wazi wazi ambazo  zimekuwa zikifanywa  ili katiba  mpya iwe ya manufaa kwa kundio moja na siyo kwa taifa  zima.

source: ITV-Daima