Sunday 29 September 2013

Ugaidi Kenya: Kibao chawageukia mawaziri

Wananchi wakiondolewa katika jengo la Westgate nchini Kenya mara baada ya watu wanaosadikiwa kuwa ni magaidi kuliteka jumba hilo maarufu kwa biashara. PICHA | FAILI 
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi

Posted  Jumapili,Septemba29  2013  saa 1:0 AM
Kwa ufupi
Taarifa hizo mpya zimekuja wakati ripoti nyingine za uchunguzi zikibainisha kuwa huenda magaidi walioshambulia jengo la Westgate walitoroka kupitia njia ya ardhini inayoanzia kwenye maegesho ya magari chini ya jengo hilo.


Nairobi. Shambulizi la kigaidi lililoua watu 67 nchini Kenya wiki iliyopita, limeanza kuchukua sura mpya baada ya kubainika kuwa mawaziri wanne na mkuu wa majeshi walipewa tahadhari kabla kuhusu kutokea kwa tukio hilo.
Taarifa hizo mpya zimekuja wakati ripoti nyingine za uchunguzi zikibainisha kuwa huenda magaidi walioshambulia jengo la Westgate walitoroka kupitia njia ya ardhini inayoanzia kwenye maegesho ya magari chini ya jengo hilo.
Kuhusu mawaziri
Tahadhari hiyo iliyoanza kutolewa Januari mwaka huu, iliwaonya viongozi hao ambao pia ni wanachama wa Baraza la Usalama la Taifa, kuwa Kundi la Al-Shabaab lilikuwa likipanga shambulizi jijini Nairobi.
Kwa mujibu wa ripoti ya kuzuia ugaidi iliyonukuliwa na Gazeti la The Saturday Nation, imewataja Waziri wa Fedha, Julius Rotich, Waziri wa Mambo ya Ndani, Joseph ole Lenku, Waziri wa Ulinzi, Raychelle Omamo, Waziri wa Mambo ya Nje, Amina Mohammed na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Julius Karangi kuwa walikuwa na taarifa za shambulizi hilo.
“Taarifa ilitolewa kwao ikiwatahadharisha kuongezeka kwa vitisho vya ugaidi na mipango ya kuanzishwa kwa mashambulizi mfululizo katika miji ya Nairobi na Mombasa kati ya Septemba 13 na 20, 2013,” inasema ripoti hiyo.
Ripoti hiyo inasema kuwa magaidi walikuwa wakipanga shambulizi linalofanana na lile lililotokea Mumbai, India ambapo walishambulia jengo na kuteka raia.
Pia, taarifa hiyo ilitolewa kwa Kamati ya Ushauri ya Usalama wa Taifa katikati ya Septemba, mwaka huu ambapo taarifa za kiintelijensia zilionyesha kuwa Al-Shabaab wameongeza harakati zao Kenya na kwamba walikuwa wanapanga shambulizi.
Kamati hiyo ambayo ndiyo ngazi ya juu ya usalama nchini Kenya, inajumuisha Rais, Naibu Rais, Waziri wa Ulinzi, Mambo ya Nje, Mambo ya Ndani, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Majeshi, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa na Mkuu wa Jeshi la Polisi.
Viongozi wote waliotajwa kupewa taarifa hawakupatikana, hata ujumbe mfupi wa maandishi waliotumiwa na gazeti hilo kwenye simu zao haukujibiwa.
Shambulizi la wiki iliyopita kwenye jengo la kibiashara la Westgate jijini Nairobi, linalomilikiwa wa raia wa Israel, liliua watu 67 na zaidi ya watu 170 kujeruhiwa.
Israel iliionya Serikali ya Kenya dhidi ya kuwapo kwa shambulizi la kigaidi kwenye majengo yanayomilikiwa na raia wa Israel wakati wa msimu wa sherehe za Kiyahudi kati ya Septemba 4 na 28.

“Ubalozi wa Israel, Nairobi, umetoa angalizo kwa Wizara ya Mambo ya Nje kuwa Iran na Hezbollah kutoka Lebanon wamekuwa wakikusanya taarifa za kiintelijensia za kutaka kuwalenga Waisrael na Wayahudi duniani kote ikiwamo Kenya,” inaonya ripoti iliyotolewa Septemba 13, 2013.
Pia, raia wa Marekani, Uingereza pamoja na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ambayo haikufahamika iwapo ililengwa kushambuliwa. Ripoti hiyo inataja hata majina ya watu ambao wangehusika kwenye shambulio hilo.
Inaendelea kufichua kuwa, shambulizi la Westgate ambalo tayari limetekelezwa na jingine la Kanisa ya Holy Family Basilica, Nairobi yalikuwa yamepangwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu na walioyaandaa wanatajwa na ripoti hiyo.
Inasema kuwa shambulizi la Westgate lilitekelezwa na Al-Shabaab chini ya uongozi wa Abdi Godane, huku ikidaiwa kuwa baadhi ya wanamgambo waliratibu shambulizi hilo kutokea eneo la Bullo Marer, Somalia.
Godane ndiye kiongozi mpya wa Al-Shabaab baada ya kuuawa kwa Omar Shafik Hammami na kumtimua Sheikh Aweys, ambaye aliamua kujisalimisha kwa Serikali ya Somalia.
Rais Uhuru Kenyatta ameahidi kuwaadhibu magaidi waliotekeleza shambulizi kwenye jengo la Westgate na kuapa kuwa jeshi halitarudi nyuma katika kuilinda mipaka ya Kenya.
Ripoti hiyo, pia imetoa tahadhari kuhusu kuibuka kwa vikundi vya kidini vyenye misimamo mikali Kaskazini Mashariki na mikoa ya pwani ya nchi ya Kenya.
“Kule Lamu, idadi isiyofahamika ya Al-Shabaab imejificha karibu na kambi ya wafugaji kati ya Katsakakairu na Nyangoro karibu na Witu,” inasema ripoti hiyo.
Mbali na kuyalenga makanisa Kaskazini mwa Kenya, magaidi hao wanadaiwa kulilenga jengo refu la Time Tower na baadhi ya sehemu maarufu za burudani kwenye mitaa ya Koinange na Kimathi jijini Nairobi.
“Mbali na kumbi za starehe, wameshaliangalia jengo la Times Tower na Nyayo. Katika mipango yao, waliangalia muda ambao watu wanakuwa wengi, usalama, kamera za CCTV na sehemu watakayosimama wakati wa kutekeleza shambulizi,” inasema ripoti na kuongeza kuwa:
“Pia, waligundua kuwa majengo yataingilika kirahisi kwa kutumia kadi bandia zinazotengenezwa River Road, Nairobi.”
Magaidi walivyotoroka

Taarifa za kiuchunguzi zimeeleza kuwa baadhi ya wanamgambo wa kundi la Al-Shabaab waliotekeleza shambulizi kwenye jengo la Westgate, walitoroka kupitia mfereji mkubwa wa maji machafu chini ya jengo hilo.
Mfereji huo unaanzia sehemu inayotumika kuegesha magari kwenye jengo hilo na kutokea katikati ya Jiji la Nairobi.
Kwa mujibu wa gazeti la Sunday Mirror la Uingereza, sehemu ya kutokea kwenye mfereji huo imezungukwa na vichaka, vinavyoaminika kutumiwa na magaidi kujificha.
Baada ya kukimbia kutoka kwenye jengo walilolishambulia, walitoroka kupitia kwenye mfereji huo.
Akizungumza ndani ya handaki hilo, mwandishi wa Sunday Mirror, Russell Myers alisema: “mfereji unaanzia Westgate mahali ambapo shambulizi lilitokea Jumamosi wiki iliyopita.”
“Magaidi huenda waliweza kupitia hapa bila kuonekana na kukimbia kuelekea jumba la makumbusho la Nairobi, kisha wakabadilisha nguo na kuingia kwenye magari,” alisema Myers.
Mbali na taarifa hizo, pia imekwisharipotiwa kuwa baadhi ya magaidi waliteketea hadi majivu ndani ya jengo hilo, huku Serikali ya Kenya ikisema sita kati yao waliuawa katika mapambano na wengine kutoroka sambamba na mateka waliookolewa.

SOURCE: MWANANCHI