Kwa ufupi
Hivi karibuni Rais Kagame alinukuliwa na vyombo
vya habari akisema kuna siku atamwadabisha Rais Kikwete na Tanzania kwa
ujumla kutokana na ushauri alioutoa kwa Rais huyo wa kumtaka akae
kwenye meza ya mazungumzo na vikundi vya waasi wa nchi hiyo vinavyoishi
kwenye misitu ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Ni Frank Magoba aliyewahi kuwa mbunge Kigamboni kupitia CUF, adai Kagame ametamka kauli mbaya
Dar es Salaam. Aliyewahi kuwa
mbunge wa Jimbo la Kigamboni Dar es Salaam kupitia Chama cha Wananchi
(CUF), Frank Magoba amemfyatukia Rais wa Rwanda, Paul Kagame, akimtaka
aiombe radhi Tanzania, Rais Jakaya Kikwete kwa kumkebehi na
kumdhalilisha kupitia vyombo vya habari.
Hivi karibuni Rais Kagame alinukuliwa na vyombo
vya habari akisema kuna siku atamwadabisha Rais Kikwete na Tanzania kwa
ujumla kutokana na ushauri alioutoa kwa Rais huyo wa kumtaka akae kwenye
meza ya mazungumzo na vikundi vya waasi wa nchi hiyo vinavyoishi kwenye
misitu ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Magoba alisema kauli ya Kagame ni ya dharau na
kebehi mbaya kwa Rais wa Tanzania na kwamba inahatarisha kuwapo kwa
Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye umoja na mshikamano.
‘’Nikiwa mbunge mstaafu na mwanajeshi mstaafu
napenda kuungana na Watanzania wengine kulaani kejeli na dharau kwa nchi
yetu kwani tunatambua kuwa baadhi ya viongozi walishazoea kumwaga damu
katika nchi zao kwa masilahi binafsi’’ alisema.
Akizungumza na vyombo vya habari jana alisisitiza
kwamba kauli hiyo ni ya uchokozi wa hali ya juu na kwamba haina nia
nzuri kwa Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
“Watanzania tulitarajia Kagame atakanusha kwamba
hakutoa kauli hiyo mwenyewe, lakini kwa kukaa kimya inamaanisha wazi
kwamba aliitoa kwa nia maalumu’’ alisema na kusisitiza kwamba kama
hakuitoa yeye basi aombe radhi. Magoba ambaye kwa sasa ni mwanachama wa
CCM alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kukaa kimya na kutojibu lolote
na kwamba kauli ya Kagame siyo ya mtu mwenye hadhi ya watu wanaojua
demokrasia, ubinadamu na upendo kwa jamii.
source: Mwananchi news paper
source: Mwananchi news paper