Kwa ufupi
Kalambo. Imependekezwa kuwa katiba ijayo itamke
bayana kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano anaweza kushitakiwa baada ya
kumaliza kipindi chake cha uongozi, iwapo atakuwa na tuhuma za kufanya
makosa ya kikatiba katika utawala wake.
Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Katiba Wilaya ya
Kalambo mkoani Rukwa, wamesema wakati wakichangia maoni yao kwenye
Rasimu ya Katiba hiyo iliyowasilishwa kwao na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba.
Mmoja wa wajumbe wa baraza hilo, Leonard
Shalamwana alisema kuwa iwapo katiba itaeleza kwamba rais anaweza
kushitakiwa baada ya kumaliza kipindi chake, itasaidia kuongoza taifa
kwa kufuata misingi ya haki na uwajibikaji.
“Katiba ikiweka bayana kwamba rais anaweza
kushitakiwa, itasaidia kudhibiti vitendo vya kifisadi, kujilimbikizia
mali.......italeta uwajibikaji na kutakuwa na utawala wa haki
unaozingatia sheria bila......tabia ya baadhi ya watu kujifanya wapo juu
ya sheria itakoma” alisema William Kisabi mkazi wa Mtai.
Kisabi aliongeza kuwa viongozi wetu wamekuwa
wakifanya ufisadi mkubwa ambapo hakuna hatua zozote zinazochukuliwa kwa
kuwa katiba inawapa nguvu ya kutoshitakiwa mara baada ya kumaliza muda
wake wa utawala kitu ambacho kinachangia kudumaza maendeleo ya taifa
hili.
Faustine Mkula alipendekeza ibara ya 76 kifungu
cha tatu kiondolewe ili kutoa fursa ya watu wengine wenye uwezo kugombea
urais katika ya Serikali ya muungano na kuepesha tamaa ya watu kutaka
kukaa madarakani kwa kipindi kirefu zaidi.
Ibara hiyo kifungu hicho inaeleza kwamba mtu
aliyewahi kuwa Rais wa Tanzania bara au Zanzibar hatapoteza sifa ya
kugombea nafasi za kugombea na kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano kwa sababu aliwahi kushika nafasi ya madaraka ya Rais wa
Tanzania bara au Rais wa Zanzibar.
Pia wajumbe wa baraza hilo walipendekeza Rais
kutoa taarifa ya hali ya hatari kwa bunge ndani wiki moja badala ya wiki
mbili kama ilivyopendekezwa kwenye rasimu ya katiba ibara ya 80 kifungu
cha kwanza hadi cha tatu.
CHANZO CHA HABARI HII: Mwananchi news paper
CHANZO CHA HABARI HII: Mwananchi news paper