Kwa ufupi.
Ni kama kuna kulindana, wahoji kama kweli dola haijui
Biashara ya dawa za kulevya inaonekana kushamiri
nchini, huku kukiwa na maswali mengi juu ya akina nani hasa wahusika wa
shughuli hii, hata inashindwa kukomeshwa.
Waliopewa mamlaka kuzuia dawa hizo nao wanahusika au hawana ujuzi, wafukuzwe?
Baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi wa
makala hii, wana mashaka kwamba huenda baadhi ya vigogo au wafanyakazi
waliopewa mamlaka kupambana na dawa nchini, wanahusika kufanya biashara
hii au kuwasaidia wanaoifanya kwa manufaa yao, madai ambayo wamekuwa
wakiyakanusha vikali.
Hata hivyo baadhi ya watu ambao wamewahi kuwa
majambazi na kujihusisha na biashara haramu, akiwamo mchungaji mmoja
kutoka Arusha ambaye amewahi kuwa jambazi kabla ya kuamua kuokoka na
kumtumikia Mungu, anasema ni vigumu mno na huenda ni jambo
lisilowezekana kufanikiwa kufanya mambo mabaya nchini kama ya ujambazi
au dawa za kulevya na ukadumu katika kazi hiyo kama hauna mtandao na
wale ambao wanahusika katika kuzuia vitendo hivyo.
“Kama una mawasiliano na wenye mamlaka utafanya
biashara yoyote chafu, kama huna ni ngumu kutokamatwa, mimi nimewahi
kuwa jambazi, ninaongea haya kwa uzoefu, sio kweli kwamba ulinzi nchini
ni mbaya, bali kuna watumishi si waaminifu” anasema Mchungaji huyo.
Kwa uzoefu wake ni kuwa iko haja kwa viongozi
walioko Serikalini kama kweli wana lengo la kupambana na dawa za
kulevya, kwanza kuwachukulia hatua wote ambao waliwakagua na kuwaruhusu
wahusika wa dawa wanaokamatwa kupita.
Ni kama hakuna lengo la kupambana na dawa za kulevya
“Kama mtu amepita uwanja wa ndege, inapaswa
kujulikana alikaguliwa na nani? Wote waliohusika wakamatwe mara moja,
waunganishwe kwenye kesi ya hizo dawa za kulevya, hii itaonyesha kweli
Tanzania tuna lengo la kupambana na dawa za kulevya, lakini
kinachofanyika sasa ni usanii wa mchana kweupe,” anasema Mchungaji huyo
ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.
Hatua kali kwa wauza dawa
Baadhi ya wananchi akiwamo Ameria Haule, mkazi wa Ubungo anashauri kutungwe sheria kali za kupambana na dawa za kulevya.
Aidha, Juma Hamisi wa Mtongaji, na Tuma Msongwa wa
Manzese, Dar es Salaam wanasema pale ambapo mtu amekamatwa na aina
yoyote ile ya dawa za kulevya, na kukawa na uthibitisho, kusiwe na haja
ya kufanya upelelezi juu yake zaidi, badala yake hukumu itolewe mara
moja. Hali kadhalika wakashauri dhamana iondolewe, wakisemabiashara hii
ni sawa na mauaji.
Kituo cha daladala kwa Manyanya
Mojawapo ya vituo vya daladala ambavyo vinadaiwa kutumiwa kwa
dawa za kulevya ni cha daladala cha Kinondoni kwa Manyanya, kama
unaelekea Posta ukitokea Kinondoni.
“Ni kawaida kuwaona vijana wakisinzia hapa kuanzia
asubuhi hadi asubuhi, kama kweli wenye mamlaka wana lengo la kupambana
na dawa, wangekuja hapa ikawasomba hawa wote wanaosinzia, kisha
ikawapime ili kuona walicholewa kimetokana na nini…kuna madai kuwa hao
ndio wauzaji wazuri wa rejareja hapa Kinondoni, hali kama hiyo iko pia
vituo vingine vingi vya daladala, huenda ndio sababu kwanini inakuwa
vigumu kupiga marufuku wapiga debe kuwepo, maana wauza dawa
wanajichanganya na wapiga debe,” anasema mkazi mmoja wa eneo hilo ambaye
aliomba jina lake lisiandikwe gazetini.
Ubungo darajani
Katika maeneo ya Ubungo kuna watu kadhaa
wanahusika na dawa hizi; Kwa mfano yuko jamaa ambaye huzunguka usiku
akisambaza dawa za kulevya kwa gari lake dogo. Hali ni mbaya zaidi eneo
la Ubungo Maziwa, wapo hadi akina mama kadhaa kwenye vijiwe vya vijana
wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Maeneo mengine ya Tanzania
Karibu nchi nzima, kuna kashfa hii ya kuwapo kwa
dawa za kulevya, huku maswali makuu yakielekezwa kwa wana usalama nchini
kama ni kweli hawaoni yanayoendelea.
Iundwe tume ya siri
Baadhi ya wananchi wanashauri kuundwe kikosi cha
siri kuchunguza utendaji wa askari ili kutoa mashaka ambayo yanaonekana
kuongezeka miongoni kwa jamii kuwa baadhi yao huenda wanashiriki katika
biashara hii ya dawa mbalimbali za kulevya yakiwemo cocaine, mirungi na
bangi.
Wanahoji ni kwanini Serikali ni kama inaonekana
kushikwa na kigugumizi katika kupambana na tatizo hili la dawa za
kulevya, licha ya idadi ya watumiaji ikionekana kuongezeka kadri siku
zinavyokwenda mbele.
Wengine wakashauri Rais Kikwete kumaanisha katika
kuchukua hatua na kuwachukulia hatua viongozi ambao wanaonekana wazi
kutochukua hatua
Ahadi nyingi vitendo haba
Licha ya kuwapo madai mengi miezi ya hivi karibuni
ikiwemo kwamba kuna viongozi wa dini wanahusika na dawa za kulevya,
wapo wabunge waliosema wanawajua wenye kufanya biashara hiyo, baadhi ya
viongozi wakielezwa kuhusika.
Mbunge aja na yake
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), amewahi kuahidi kuwa ataanika majina ya vigogo wanaofanya biashara hiyo haramu.
Mbunge huyo pia aliwatuhumu viongozi wakiwamo mawaziri, kwa kuhusika na vitendo vya rushwa ama mihadarati.
Lugola alitoa kauli hiyo wakati akichangia Hotuba
ya Makadirio ya Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, inayoshughulikia
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
“Ninawaomba wabunge wenzangu, kabla ya kumaliza
mkutano huu wa Bunge nitakuja na orodha ya viongozi wa taasisi za
Serikali, wanaojihusisha na dawa za kulevya naomba mniunge mkono,”
alisema bila mafanikio. Jana mwandishi alimtafuta ili kujua sababu za
kutotaja, hakupatikana.
Tume dhaifu iwajibishwe
Hata hivyo, Lugola alisema Kamishina wa Tume ya
Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya, Christopher Shekiondo, anapaswa
kuwajibishwa kwani ameshindwa kazi, kwani kuna wakati aliwahi kunukuliwa
akisema anawajua wanaohusika na dawa hizo nchini, lakini kuna ugumu wa
namna ya kuwakamata.
“Hakuna cha kushindwa hapa kama sio rushwa nini,
Shekiondo awajibishwe kama anashindwa kuwakamata, kwanini kama
kuwakamata ni tatizo wasiombe msaada hata kwa FBI kama walivyoletwa juzi
baada ya mauaji ya Padri,” alisema.
Orodha ya viongozi wa dini wanaohusika na dawa za kulevya
Wakati fulani mwaka juzi kulielezwa kuwa kuna orodha ya viongozi wa dini ambao wanahusika na biashara ya dawa za kulevya.
Kauli ya Rais kuhusu viongozi wa dini kuhusika na
biashara ya dawa za kulevya alitamkwa Juni 5, 2011 wakati akiwa
akiwahutubia waumini wa Kanisa Katoliki la Jimbo la Mbinga wakati wa
ibada maalumu ya kuwekwa wakfu na kupewa daraja la uaskofu na hatimaye
kusimikwa kuwa Askofu wa jimbo la Mbinga, Mhashamu John Ndimbo.
Maaskofu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania waongea
Katika taarifa yao kujibu hilo la Rais Kikwete, Maaskofu wa
Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), walimpa Rais Kikwete saa 48 za
kuwataja kwa majina viongozi wote wa Dini anaowatuhumu kuhusuka na
biashara haramu ya dawa za kulenya “unga”.
Agizo la CCT lilitolewa na Mwenyekiti wake taifa,
Askofu Peter Kitula jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa
habari linasema, “Tunampa saa 48 Rais awataje kwa majina viongozi hao
ambao yeye anadai wanajihusisha na kuuza dawa na kama atashindwa kufanya
hivyo tunamtafsiri ni mwongo na mzushi”. Hata hivyo Kikwete hajawahi
kuwataja viongozi wa dini wanaohusika na biashara hiyo.
Agnes na Melisa wakamatwa na kilo 150 Afrika Kusini
Tukio la hivi karibuni kabisa ni la wanawake
wawili toka Tanzania, waliokamatwa Uwanja wa Ndege wa OR Tambo, Afrika
Kusini wakitokea Tanzania Julai 6, mwaka huu wakidaiwa kuwa na dawa za
kulevya takribani kilo 150.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Tume ya Kuratibu
Udhibiti wa Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa, wanawake hao ni Agnes Jerald
(25) maarufu kwa jina la Masogange na Melisa Edward (24).
WASANII NA DAWA ZA KULEVYA
Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi
‘Sugu’ anasema baadhi ya wasanii na watu maarufu wamekuwa wakitumiwa
kubeba dawa za kulevya kwa vile wanasafiri mara nyingi na huwa
wanaonekana kutotiliwa shaka. Kwamba hata yeye kabla ya Ubunge aliwahi
kuombwa afanye kazi hiyo alikataa.
Binti Kiziwi
Mrembo Sandra Khan, aliyepata jina la Binti Kiziwi
baada ya kushiriki video ya wimbo wa Binti Kiziwi ambao ni mali ya
mwanamuziki Ally Mohamed Ahmad ‘Z-Anto’, alikamatwa Februari, mwaka huu
China na kudaiwa kukutwa na madawa ya kulevya tumboni.
Sisitizo la Nzowa
Kamishna Nzowa, anasisitiza kuwa suala la vita ya
kupambanana na dawa za kulevya linahitaji mikakati endelevu na kwamba
wanaendelea kujipanga kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika vita hii.
Akizungumzia kuhusu waliohusika kupitisha kilo 150
za dawa za kulevya kumsaidia Masogange uwanja wa ndege, Nzowa anaamini
wote watakamatwa.
Hali ya dawa za kulevya nchini
Kwa mujibu wa ripoti ya ofisi ya Waziri mkuu, Tume
ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya, tatizo la dawa za kulevya
nchini limeendelea kukua licha ya jitihada mbalimbali zinazofanyika
katika kupambana nalo.
Hali hii inadhihirishwa na kiasi kikubwa cha dawa
za kulevya kilichokamatwa hususan heroin na cocaine katika mwaka 2011
ikilinganishwa na mwaka 2012.
Takwimu zinaonyesha kuwa kilo 264.3 za heroin
zilikamatwa mwaka 2011 ikilinganishwa na kilo 185.8 zilizokamatwa mwaka
2010. Takwimu hizi zinaonyesha.
Ongezeko la asilimia 42 la kiasi cha heroin
kilichokamatwa katika kipindi cha mwaka mmoja tu. Aidha, mwaka 2011 kilo
126 za cocaine zilikamatwa ikilinganishwa na kilo 63 zilizokamatwa
mwaka 2010 ambalo ni ongezeko la asilimia 100.
Source: Mwananchi news paper
Source: Mwananchi news paper