Na Minael Msuya na Benjamin Mwangoka, Mwananchi
(email the author)
Posted Ijumaa,Julai12 2013 saa 10:41 AM
Posted Ijumaa,Julai12 2013 saa 10:41 AM
Kwa ufupi
Alisema, biashara ya dawa za kulevya
inayoendelea inatokana na tatizo la utoaji na upokeaji wa rushwa ambao
unaongozwa na watu wakubwa, walioko katika mfumo halisi wa rushwa.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa
Makampuni ya IPP, Reginald Mengi amesema, biashara ya dawa za kulevya
inashamiri kutokana na tatizo la rushwa nchini.
Mengi alibainisha hayo jana katika uzinduzi wa
ripoti ya mazingira ya ufanyaji wa biashara nchini 2013, iliyoandaliwa
na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).
Alisema, biashara ya dawa za kulevya
inayoendelea inatokana na tatizo la utoaji na upokeaji wa rushwa ambao
unaongozwa na watu wakubwa, walioko katika mfumo halisi wa rushwa.
“Huwezi kutenganisha rushwa kubwa na dawa za
kulevya, hawa wasichana wasanii wetu, waliokamatwa Afrika Kusini na dawa
za kulevya na kile kiasi, lazima kuna mtu mkubwa aliye nyuma yao,siyo
wao,” alisema Mengi.
Mengi alisema,utashi wa Serikali katika
kupambana na rushwa uko kisiasa ndiyo sababu hakuna utekelezaji na
ikiendelea kuwakumbatia na kuwashikilia mkono watu hao nchi itadondoka.
Alisema, taifa linatakiwa kuwatenga watoa
rushwa na rushwa zao ili kuweza kuwa na taifa lenye nguvu kwa kuwa
Serikali imeshindwa kupambana dhidi ya rushwa. kwa kuwa inahofia
kukumbwa katika mfumo huo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo nchini,
Godfrey Simbeye alisema mazingira ya kufanyia biashara nchini ni magumu
kutokana na kodi nyingi na sheria ngumu zilizowekwa.
Simbeye alisema, utafiti unaonyesha kuwa suala la
utozaji wa kodi limekuwa changamoto kubwa katika biashara kutokana na
kuwa na kodi nyingi zisizoeleweka.
“Vikwazo vikubwa vinavyoyakabili mazingira ya
ufanyaji wa biashara nchini ni kodi, kumekuwa na kodi nyingi
zinazotozwa na zisizoeleweka na sheria zilizowekwa zinaifanya biashara
kuwa ngumu,” alisema.