Kwa ufupi
Waziri Mkuu Mizengo Pinda ni kati ya viongozi
ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakitoa kauli juu ya hali elimu
nchini hususan kwenye nyanja ya sayansi na teknolojia.
Mwaka 2008 akiwa Bungeni Mjini Dodoma, alieleza
kwa undani kuhusu masomo ya Sayansi na Hisabati akitoa tahadhari ya
kukosa wanasayansi ambao ni watu muhimu katika maendeleo.
Katika maelezo yake, analinganisha ufaulu wa
masomo ya sayansi na sanaa katika shule za msingi na sekondari, ambako
ilithibitika kwamba ufaulu wa masomo ya sayansi kwa kipindi cha kuanzia
mwaka 2003 hadi 2007 ulikuwa umeshuka.
Akifafanua zaidi anasema, mwaka 2001, katika
mtihani wa kumaliza darasa la saba, asilimia 62 ya watahiniwa katika
Wilaya ya Morogoro Vijijini walipata sifuri katika mtihani wa Hisabati.
Anaeleza kuwa katika mtihani wa kidato cha nne
mwaka 2007, matokeo yanaonyesha kwamba asilimia 69 ya watahiniwa
walishindwa mtihani wa Hisabati.
“Katika zama hizi za sayansi na teknolojia, hali kama hii inatisha na haiwezi kuruhusiwa kuendelea kutokea,” anasema Pinda.
Kutokana na hali hiyo, Serikali imekuwa ikifanya
jitihada mbalimbali za kufungua milango kwa wadau ambao wanaweza
kuchochea maendeleo ya sayansi nchini.
Moja ya njia hizo ni mkutano wa wadau wa sayanasi
‘Smart Partnership Dialogue’ uliohusisha wadau kutoka kwenye mataifa
mbalimbali ya Afrika, lengo likiwa ni kujadili jinsi bara hili
litakavyoweza kutumia teknolijia kuchangia maenedeleo.
Mbali na mkutano huo ambao, wadau mbalimbali
walishauri Serikali kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja
na kutenga fedha za kutosha ili kuwezesha tafiti kufanyika katika vyuo
na taasisi nyingine.
Mbali na mkutano huo, taasisi isiyo ya kiserikali
inayojishughulisha na tafiti zenye mweelekeo wa kisera kwenye masuala ya
Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STIPRO), inawakutanisha wadau wa sekta
ya elimu kujifunza jinsi ya utoaji wa elimu ya uvumbuzi katika elimu ya
juu na vyuo vya ufundi nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa STIPRO, Dk Britrina
Diyamett anasema, mazingira yaliyopo katika elimu ya juu na vyuo vya
ufundi hayakidhi matakwa ya utoaji wa elimu ya uvumbuzi.
“Vyuo vyetu bado havina vifaa vya kujifunzia na
kufundishia, walimu nao hawajaandaliwa kutoa elimu ya uvumbuzi,
wanafundishwa kinadhalia kuliko vitendo. Tutafute vifaa vya kujifunzia
ili mwanafunzi anapomaliza kufundishwa kwa nadhalia, ajifunze pia kwa
vitendo.” Anasema Dk Diyamett
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Aalbolrg Nchini Denmark, Profesa
Palle Rasmussen anasema wanafunzi wanatakiwa kutambua umuhimu wa
uvumbuzi na lengo la kukuza teknolojia.
Profesa Rasmussen anafafanua kuwa kunahitajika
kutumia vitendo zaidi katika kufundisha na kuwashirikisha wadau wa sekta
binafsi ili kuweza kufikia lengo la kuwa na wataalamu wa kutosha.
“Ili kuweza kutengeneza mfumo mzuri wa kuwapata wahitimu bora
ni lazima kuwashirikisha wanafunzi na walimu wao katika utoaji na
upokeaji wa mafunzo hayo ya uvumbuzi,” anasema Profesa Rasmussen.
Profesa Rasmussen anasema kuwa, taasisi za elimu zinaweza kuendesha tasinia ya uvumbuzi pasipo kutegemea serikali.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
Dk Johnson Ishengoma anasema, haiwezekani kujenga vijana kuwa wavumbuzi
wakati miundombinu ya kujifunzia bado haijaimarishwa.
Anaeleza kuwa Serikali inatakiwa kuwekeza fedha za
kutosha katika vyuo ili kuviwezesha kufanya tafiti zitakazosadia
kuvumbua mambo mbalimbali yenye tija kwa taifa.
“Itachukua muda mrefu kutoa elimu bora ya
uvumbuzi kutokana na kutokuwapo kwa walimu wa kutosha wa kutoa mafunzo
hayo,” anasema Dk Ishengoma.
Dk Isengamo anaeleza kuwa elimu hiyo ikitolewa
ipaswavyo, mwanafunzi akihitimu mafunzo yake ya chuo hatasubiri
kuajiriwa na badala yake atajiajiri mwenyewe.
Naye Vera Mugittu kutoka Muvek Development
Solutions Ltd anasema, anasema ni vigumu kutengeneza mfumo huo kutokana
na kutokuwepo kwa sera inayoratibu utoaji wa mafunzo hayo.
“Utoaji wa elimu ya uvumbuzi ni jambo gumu na la
muda mrefu, serikali inatakiwa kutambua umuhimu wake na kuwekeza zaidi
kwa kutenga fedha za kutosha,” anasema Vera.
Mhadhiri wa Kuchuo Kikuu Cha Dar es Salaam,
kitengo cha cha uhandisi na ueknolojia, Profesa Bavo Nyichomba anasema
kukuwa kwa uvumbuzi kunategemea na ongezeko la wanafunzi wanaosoma
masomo ya sayansi.
Anasema ubora wa uvumbuzi umekuwa hauna tija kutokana na viwanda vilivyokuwapo hapo awali kufungwa.
“Ni jambo la aibu hadi vijiti vya meno na viwembe tunategemea kutoka nje, vitu ambavyo kama viwanda vyetu vingeimarishwa na kujengewa uwezo tumepiga hatua katika uvumbuzi,” anasema Profesa Nyichomba na kuongeza:
“Ni jambo la aibu hadi vijiti vya meno na viwembe tunategemea kutoka nje, vitu ambavyo kama viwanda vyetu vingeimarishwa na kujengewa uwezo tumepiga hatua katika uvumbuzi,” anasema Profesa Nyichomba na kuongeza:
“Tuanze kuboresha uvumbuzi kwa kuwarejesha
wataalamu waliopo nje, waajiriwe na kutoa mafunzo sambamba na kutenga
fedha za kutosha kuwezesha elimu ya juu na vyuo vya ufundi kutoa mafunzo
kwa kiwango cha juu.”
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru
Kawambwa anasema, jukumu la kutoa elimu siyo la serikali pekee bali
kila mwananchi ana mchango kwenye suala hilo.
“Ili kutoa elimu iliyo bora ni jukumu la kila
mmoja wetu, suala hili linahusisha nyanja mbalimbali. Kila mtu ana
mchango katika kuhakikisha elimu yetu inakuwa bora. Walimu, wanafunzi
na wazazi kila mmoja akitekeleza wajibu wake ipasavyo tutafikia
malengo,” anasema Dk Kawambwa.
chanzo: Mwananchi news paper
chanzo: Mwananchi news paper