Mwanachi, 2013.
Morogoro. Wasomi nchini wamesema Tanzania inashindwa kupiga hatua ya maendeleo kutokana na Serikali kuwa na sera na mipango mingi ambayo inashindwa kuitekeleza.
Morogoro. Wasomi nchini wamesema Tanzania inashindwa kupiga hatua ya maendeleo kutokana na Serikali kuwa na sera na mipango mingi ambayo inashindwa kuitekeleza.
Walisema kabla ya kukamilika kwa mpango mmoja, unaanzishwa mwingine hali ambayo inafanya kila jambo kufanyika nusunusu.
Mkuu wa zamani wa Mkoa Rukwa, Daniel Ole Njolai,
alisema Serikali iwe sikivu na itekeleze mipango yake ili kuwakomboa
wananchi maskini, ambao asilimia 80 ni wakulima.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mkutano
mkuu wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata) jana,
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua), Dk Damian Gabagambi,
alisema Tanzania inahitaji miaka 240 kuanzia sasa ili kutokomeza
umaskini uliokithiri.
Dk Gabagambi alisema tatizo kubwa ni kutotekelezwa
sera na mipango ya Serikali, huku akitolea mfano Mkurabita, Mkukuta na
Kilimo Kwanza.
Alisema wakati mipango hiyo ikiwa kwenye
utekelezaji, Serikali imekuja na mipango mingine mingi ambayo nayo
itaguswa kidogo na kuanzishwa mingine ukiwamo, Mpango mkubwa wa kutoa
matokeo sasa (Big results now).
“Tangu mwaka 1997 hadi 2011 umaskini umepungua kwa
asilimia 2.1, maana yake ni kwamba tukitaka kupunguza umasikini mpaka
asilimia 10, tutahitaji miaka 169 na ili tuutokomeze kabisa tunahitaji
miaka 240,” alisema Dk Gabagambi.
Naye Profesa Amon Mattee kutoka Sua, aliwashauri
wakulima na wafugaji kuzingatia sera katika masuala yote yanayohusu
kilimo, kujitambua katika kukuza maslahi yao.
Profesa Mattee alisema wakulima wasisubiri kufanyiwa kila kitu, aliwataka kuwa kitu kimoja na kudai maslahi yao.
Mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadam
(LHRC), Anord Sungusia, aliwashauri wakulima kuwa na rasimu ya katiba
na kuisoma kwa kina na baadaye kuijadili, ili kuwasilisha mapendekezo
yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.