Tuesday 16 July 2013

Dk. Mwakyembe atoa misaada ya milioni 40/- jimboni


                                   

      Na Thobias Mwanakatwe, 13th July 2013

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ametoa misaada yenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 40 jimboni mwake yakiwamo madawati 315 yatakayogawanywa kwa shule za msingi za jimbo la Kyela mkoani Mbeya.

Dk. Mwakyembe alikabidhi misaada hiyo jana mjini hapa ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano jimboni mwake yenye lengo la kuhamasisha maendeleo na kukamilisha ahadi alizoahidi wakati wa uchaguzi mkuu wa 2010.
Shule za msingi 14 zilizonufaika na msaada wa madawati 351  Maendeleo, Ikulu, Mbala, Ipyana, Ndola, Bujonde, Muungano, Lubele, Kasumulu, Malangali, Talatala, Kikuba, Gwato na Mahenge, kila shule itapewa madawati 24.

Dk. Mwakyembe pia alikabidi pikipiki 10 kwa vikundi vya maendeleo bodaboda ambavyo ni Nia Njema, Amani, Stendi, Tenende, Kyeluku, Transifoma, Mshikamano, Nyota njema, Kalumbulu na Ngyeke.

Alisema kikundi vya waendesha bodaboda kitakachoonyesha mafanikio zaidi kwa mradi wake kuwa na mtaji mkubwa kila baada ya miezi sita atakapofanya ziara jimboni mwake atakiongezea pikipiki nyingine mpya.

Dk. Mwakyembe ambaye ni Mbunge wa Kyela, pia alikabidhi vifaa mbalimbali katika Hospitali ya Wilaya ya Kyela ambavyo ni vitanda kwa ajili ya wanawake wajawazito na baiskeli maalum kwa ajili ya kuwabebea wagonjwa.

Pia alikabidhi mashine ya kisasa kwa kikundi cha vijana waosha magari kyela mjini na kuwataka vijana hao kujikusanya eneo moja maalum ya kuoshea magari badala ya kufanya kazi hiyo maeneo mbalimbali katika mji huo hali inayosababisha uchafu wa mji.

Mbunge huyo alisema baada ya siku mbili kuanzia leo atakabidhi gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) litakalotumika kwa ajili ya Hospitali ya wilaya Kyela.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kyela, Dk. Hunter Mwakifuna, alisema misaada aliyoitoa Dk. Mwakyembe haina itikadi ya  vyama badala yake itawanufaisha watu wote wakiwamo wa vyama vya upinzani.

Dk. Mwakifuna ambaye pia ni diwani wa kata ya Ipinda alisema vijana waendesha bodaboda wasikubali kushawishiwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kufanya maandamano yasiyokuwa na manufaa kwao badala yake  wajikite kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali.

  Source: IppMedia