Monday 22 July 2013

Askari akamatwa kwa kudhalilisha maiti DRC

19 Julai, 2013 - Saa 14:14 GMT

                                     
Wanajeshi wa DRC wakitoa ulinzi katika eneo la Kanyarucinya, yapata kilomita 12 kutoka mji wa Goma.
Afisa mmoja wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ametiwa nguvuni baada ya kuchafua maiti za wapiganaji wa waasi nchini humo.
Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa DRC, Lambert Mende, ameiambia BBC kwamba Luteni Solomo Bangala alizuiliwa jana Alhamisi na maafisa wa kijeshi baada ya mapigano kuzuka kati ya jeshi na waasi wa M23 katika eneo la mashariki karibu na mji wa Goma.

Kukamatwa kwa afisa huyo kunajiri muda mfupi tu baada ya katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon kuzungumzia madai ya kuwepo dhuluma na mateso dhidi ya wafungwa kutoka makundi ya waasi pamoja na wale waliouwawa zinazotekelezwa na wanajeshi wa Kikongomani.
Kikosi cha kulinda amani cha umoja wa mataifa kinatathmini upya hatua yake ya kuunga mkono vikosi vya serikali ya DRC kufuatia shutuma hizo.
                                       
Waasi wa M23
Mapigano kati ya jeshi la DRC na waasi wa M23 yalianza siku ya Jumapili karibu na mji wa Goma.
Mwandishi wa BBC Maud Jullien aliyepo katika mji wa Goma anasema uwanja wa mapigano ulikuwa takriban kilomita 7 katika vilima kutoka mji huo.
Hapajakuwa na mapigano yoyote katika kipindi cha siku mbili zilizopita na jeshi limesema limefanikiwa kuwafukuza waasi yapata kilomita 6, anasema mwandishi wetu.
Mwezi Novemba, wanamgambo wa M23 waliuteka kwa kipindi kifupi mji wa Goma, kisha wakaondoka baada ya kutimizia msururu wa ahadi ikiwemo kuanzisha mazungumzo na serikali.
Waasi wa M23, ambao kwa wingi wanatoka kabila la Watutsi walijiondoa katika jeshi la serikali mwezi Aprili mwaka 2012, na kuanzisha mapigano yaliyowaacha takrikaban watu 800,000 bila makao katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.
Mazungumzo ya amani yaliyofanyika nchini Uganda mwaka huu ili kushughulikia malalamishi ya waasi hao yamekwama.

chanzo: BBC Swahili